#WC2018: Cheki makocha wanaolipwa pesa nyingi Russia 2018

Muktasari:
Kocha, huyo aliyekuwa mchezaji wa zamani wa Simba wa Teranga, analipwa Euro 200,000 kwa mwaka.
MOSCOW, RUSSIA. KOCHA wa Senegal, Aliou Cisse ndiye kocha mwenye mshahara mdogo zaidi kati ya wale waliopo kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia.
Kocha, huyo aliyekuwa mchezaji wa zamani wa Simba wa Teranga, analipwa Euro 200,000 kwa mwaka.
Unataka kujua ni makocha gani wanaolipwa pesa ndefu za mishahara kwenye orodha wa wale watakaokuwa na timu kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia. Cheki hawa hapa.
Oscar Tabarez- Uruguay, Euro 1.7milioni
Akiwa na kikosi chenye mastaa kibao wa maana akiwamo Luis Suarez na Edinson Cavani, Tabarez ni mmoja kati ya makocha wanaolipwa mishahara mikubwa kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia na ndiyo maana anabeba matumaini makubwa kwa taifa hilo kwamba atakwenda kufanya vizuri. Tabarez alikuwa mwalimu wa shule ya msingi. Analipwa Euro 1.7milioni kwa mwaka.
Jorge Sampaoli- Argentina, Euro 1.8milioni
Kupata fursa ya kukinoa kikosi cha Argentina chenye staa wa maana kabisa duniani, Lionel Messi si jambo dogo. Argentina inakwenda kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia ikiwa moja ya mataifa yanayopewa nafasi ya kunyakua ubingwa. Kutokana na hilo ndilo maana Sampaoli anakuwa mmoja kati ya makocha wenye mishahara mikubwa kati ya wale waliopo kwenye fainali hizo, ambapo mshahara wake wa mwaka ni Euro 1.8 milioni.
Gareth Southgate- England, Euro 2milioni
Mtihani mmoja unaomkabili Southgate kwamba anakwenda kwenye fainali na timu yenye kelele nyingi, ambayo kila mtu ni mjuaji.
Hukawii kusikia magazeti yakipanga kikosi cha kuanza. England wenyewe wanajiamini kwamba watakwenda kubeba ubingwa wa fainali hizo licha ya kuwapo na ukweli kwamba kubeba taji hilo la dunia si rahisi kama wanavyofikiri. Kocha wao anavuna Euro 2 milioni kwa mwaka.
Carlos Queiroz- Iran, Euro 2milioni
Ni kocha mwenye rekodi zake kwenye mchezo wa soka, akianzia kuwa msaidizi wa Sir Alex Ferguson huko Manchester United kabla ya kwenda kuwa kocha mkuu Real Madrid na aliwahi kuinoa pia Timu ya Taifa ya Ureno. Queiroz atakuwapo kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia akiwa na kikosi cha Iran na kitendo cha kuwafikisha tu kwenye fainali hizo kumemfanya Mreno huyo kuvuna pesa nyingi na hakika ni mmoja kati ya makocha wanaolipwa mshahara mkubwa, Euro 2 milioni kwa mwaka.
Fernando Santos- Ureno, Euro 2.25milioni
Santos anaiongoza Ureno yenye matumaini ya kwenda kubeba ubingwa wa dunia huko Russia miaka miwili kupita tangu walipobeba ubingwa wa Ulaya. Silaha yake kubwa kikosini ni supastaa Cristiano Ronaldo, mmoja kati ya wachezaji mahiri kabisa na wanaolipwa pesa nyingi kwenye soka kwa sasa. Jambo hilo limemfanya hata kocha wake anayemnoa kwenye timu hiyo ya Ureno kuwa na mshahara mzuri ambapo amekuwa akipokea Euro 2.25 milioni kwa mwaka.
Stanislav Cherchesov- Russia, Euro 2.6milioni
Russia ni wenyeji wa fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu na hakika timu yao itaingia uwanjani ikiwa na matumaini ya kufanya vizuri na kubeba ubingwa huo kama walivyofanya Ufaransa kwenye fainali za Kombe la Dunia 1998.
Katika kuhakikisha kwamba ubingwa unabaki nyumbani, Russia imeamua kumpa mshahara mkubwa kocha wake kama motisha vile ya kufanya vyema ambapo Cherchesov, anapokea mshahara wa Euro 2.6 kwa mwaka.
Julen Lopetegui- Hispania, Euro 3milioni
Lopetegui ndiye kocha wa Hispania kwa sasa akichukua mikoba hiyo kutoka kwa Vicente del Bosque, aliyeachia ngazi baada ya michuano ya Euro 2016.
Ukweli kocha huyo mpya ana shughuli pevu katika kurudisha makali ya La Roja kufuatia kufanya vibaya kwenye michuano mikubwa miwili iliyopita, kwenye Euro 2016 na Kombe la Dunia 2014. Katika kumfanya kocha huyo anasumbue akili yake kutafuta mbinu za kibingwa na ndio maana imeamua kumlipa mshahara mkubwa, Euro 3 milioni kwa mwaka
Didier Deschamps- Ufaransa, Euro 3.5milioni
Ufaransa inaripotiwa kuwa na timu nzuri ya mastaa wa maana na uwezo wa kutwaa Kombe la Dunia huko Russia.
Lakini, wasiwasi mkubwa upo kwenye uwezo wa kocha wake, Didier Deschamps na ndiyo maana ilionekana kuwa ni kitu cha kawaida Zinedine Zidane kuhusishwa na mpango wa kuinoa timu hiyo. Deschamps hatakuwa na sababu ya kufeli huko Russia kutokana na kuwa na wachezaji wazuri na analipwa mshahara mkubwa, Euro 3.5 milioni kwa mwaka.
Tite- Brazil, Euro 3.5milioni
Brazil, mabingwa mara tano wa ubingwa wa dunia na ni wakali wanaopewa nafasi kubwa ya kwenda kufanya kweli kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia.
Brazil inaundwa na mastaa wa maana sana akiwamo Neymar, ambaye mshahara wake si mchezo na jambo hilo linamfanya hata kocha wa Wacheza Samba hao kulipwa mshahara mkubwa, Euro 3.5 mil kwa mwaka. Tite hatakuwa na sababu ya kikosi chake kushindwa kufanya hivyo kwenye fainali hizo kwa sababu ana wachezaji wakali na ana mshahara mzuri.
Joachim Low- Ujerumani, Euro 3.85milioni
Miaka minne iliyopita, Low aliisaidia Ujerumani kubeba ubingwa wa dunia wakati fainali za Kombe la Dunia zilipofanyika Brazil.
Mwaka huu ataiongoza tena timu hiyo kwenda kujaribu kubeba taji hilo huko Russia. Low, ametaja kikosi imara zaidi licha ya kwamba kitendo chake cha kumwaacha Leroy Sane kimezua taharuki kubwa. Low ndiye anayelipwa mshahara mkubwa zaidi kati ya waliopo huko Russia. Analipwa Euro 3.85 milioni kwa mwaka.