UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Tuna kocha mzawa anayeweza kuifundisha Simba kwa sasa?

Thursday April 22 2021
kaliua pic

KADRI siku zinavyozidi kwenda, ndivyo makocha wetu wazawa wanavyozidi kushuka thamani! Kadri wiki zinavyosonga, ndivyo makocha wetu wazawa wanavyozidi kudidimia! kadri saa zinavyokatika, ndivyo makocha wetu wanazidi kuachwa na ukubwa Simba.

Unakumbuka mara ya mwisho kocha mzawa alipotwaa Ubingwa wa Ligi Kuu Bara? Niandikie meseji yenye jina lake kamili kwenye namba yangu ya simu hapo juu.

Makocha wetu wazawa siku hizi wana kazi mbili tu kubwa, wapo wanaongoza kwa kuzipandisha timu ligi kuu na wale wanaojisifu kwa kuokoa kila siku timu kushuka daraja.

Unamkumbuka kocha mzawa ambaye amewahi kwenda na timu yetu yoyote kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika?

Usinipe jibu! Sio kweli Tanzania hatuna makocha wazuri, wapo kina Charles Boniface Mkwassa, wapo kina Sunday Kayuni, wapo pia kina Abdalah Kibadeni.

Hawa ni miongoni mwa manguli wa soka Tanzania, wameucheza mpira kwa mafanikio makubwa, wameufundisha pia kwa mafanikio makubwa. Lakini wanakwenda sambamba na kasi ya sasa ya Simba? Labda jibu ni ndiyo, labda jibu ni hapana.

Advertisement

Tuko kwenye Dunia ya kujiongeza, tuko kwenye Dunia ya kujiongezea thamani, kila mmoja kwenye eneo lake anatakiwa kujiongeza, kocha wetu wazawa kwa sasa kupewa timu kama Simba, Yanga, Azam FC na timu ya Taifa inaonekana ni kama bahati.

Kama tunapitisha miaka karibu 15 bila kuwa na kocha mzawa aliyewahi kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara, kuna kocha kweli mzawa anayeweza kuiongoza Simba hii inayotaka Ubingwa wa Afrika? Niandikie maoni yako kwenye namba yangu ya simu hapo juu.

Ukitazama uzoefu na elimu, tuna makocha wazawa wenye vigezo vya kufundisha klabu kama Simba hapa nyumbani lakini tukiangalia Kabati la Mafanikio, ni giza tupu! Thamani ya makocha wetu wazawa haiwezi kuongezeka kwa kuwachukia makocha wageni. Itakuja baada ya kujifunza kitu kutoka kwao.

Makocha wetu wazawa kuna wakati wanafanya maisha yao kuwa magumu wenyewe, wamekosa uthubutu, wameshindwa kujiongeza, matokeo yake wamekuwa watu wa kulalamika tu wanadharaulika.

Wachezaji wetu wazawa wanajitahidi sana kupambana na wachezaji wa kigeni kuliko makocha wazawa wanavyogalagazwa na makocha wa kigeni, ni aibu kwa makocha wetu kwenda zaidi ya miaka 15 bila hata mmoja wao kutwaa ubingwa.

Ni kweli Simba na Yanga wamekuwa wakisajili wachezaji bora lakini, hata timu hizo ukiwapa makocha wazawa bado sarakasi ni zile zile. Kadri Dunia ya soka inavyozidi kubadilika, ndivyo makocha wetu wazawa wanavyozidi kupotezwa, kadri Simba inavyozidi kuwa kubwa, ndivyo makocha wetu wazawa wanavyozidi kupoteza sifa za kuiongoza.

Pamoja na kuwa Yanga na Azam bado wanapambana kurejea kwenye ubora wao, lakini ukiambiwa utaje majina ya makocha wawili wanaoweza kwenda kuokoa jahazi kwenye timu hizo lazima utashikwa na kigugumizi. Sio kwamba makocha wazawa hawapo, hakuna mwenye mafanikio hata mmoja katika kipindi cha miaka mitano ya hivi karibuni, makocha wetu wazawa siku hizi wana kazi kubwa mbili, kupandisha timu daraja na kuokoa timu zisishuke daraja.

Hatuna kocha mzawa kwa miaka mitano ya hivi karibuni mwenye uwezo wa kuipa timu ubingwa ligi Kuu. Kila nikiitazama Simba inavyokua kwa sasa, napata wasiwasi mkubwa sana kama tuna kocha mzawa anayeweza kwenda na kasi ya Mnyama.

Napata mashaka kama nchi yetu ina kocha mzawa kwa sasa mwenye malengo ya siku moja kutwaaa ubigwa wa Afrika, huku tunakoelekea, makocha wazawa watakuja kuwa wanatumika kwenye Ligi Daraja la Kwanza na Daraja la Pili.

Makocha kutoka Rwanda, Burundi, Kenya na Uganda wengi wamekuwa wakija Tanzania na kuonyesha kitu.

Makocha wetu wazawa wako hapa hapa, hakuna kikubwa wanachofanya kwenye soka la nyumbani, hakuna kocha yeyote mwenye uthubutu wa kwenda nje.

Wapo baadhi wanaopambana kuzinasua timu na janga la kushuka daraja, wapo wengine pia ambao ni mabingwa wa kuzipandisha timu ligi Kuu. Lakini, tutampata kocha mzawa kweli wa kuifundisha timu kama Simba hivi karibuni? Niandikie maoni yako kwenye namba ya simu hapo juu.

Kwa namna yoyote ile, kocha wa kuifundisha Simba kwa sasa lazima atatakiwa kuwa na mafanikio kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika au Ulaya. Kocha wa timu kwa sasa ni lazima atakuwa mtu mwenye mafanikio kwenye timu ya Taifa. Kocha wa Simba kwa sasa hawezi kuwa mtu aliyebobea kwenye kupandisha timu daraja, hawezi kuwa kocha anayeweza kuiokoa timu na Janga la kushuka daraja. Simba imeshatoka huko, Simba iko Dunia nyingine. Tuna kocha mzawa anayeweza kuifundisha Simba kwa sasa? Nasubiri jibu lako.

Mchezaji aendelee kuwa mshambuliaji bora ni lazima aendelee kufunga mabao, ili kocha aendelee kuwa kocha mkubwa ni lazima aendelee kushinda mataji, ni lazima aendelee kufuzu kwenye michuano mikubwa. Hizi sifa mbili zikikosekana, huyu mtu anapungua ubora, makocha wetu wazawa ni lazima waende sambamba na uhitaji wa sasa wa Klabu kama ya Simba, Yanga na Azam. Lengo la Yanga kwa sasa ni kurudi kwenye zama zao za kutwaa Ubingwa wa VPL ambao wameokosa kwa msimu wa tatu sasa, unamwona kocha yeyote mzawa anayeweza kuwapa taji hilo? Niandikie jina lake kwenye namba yangu ya simu hapo juu.

Azam FC wana zaidi ya miaka 10 kwenye VPL na wametwaa ubingwa mara moja, unamwona kocha yoyote mzawa mwenye uwezo wa kuwapa ubingwa wa mara yao ya pili? Niandikie maoni yako kwenye namba yangu ya simu hapo juu.

Bado tuna kazi kubwa kwenye soka letu, makocha wetu wazawa wanazidi kudidimia na kukosa sifa, hatuwezi kuendelea kama makocha wetu wote wazawa hakuna anayeota siku moja kufuzu michuano ya

Mataifa ya Afrika, kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Afrika Tabia ya makocha wetu wazawa kujisifia kila siku kuokoa timu na janga la kushuka daraja, haitotupeleka popote, tabia ya makocha wetu wazawa kujisifia kupandisha timu daraja, inazidi kuwashusha tu thamani.


Imeandikwa na Oscar Oscar

Advertisement