SPOTIDOKTA: Kwanini mapumziko dakika tatu Afcon?

MASHINDANO ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 yanayofanyika nchini Ivory Coast yanazidi kusonga mbele mara baada ya kumalizika hatua ya mtoano na kesho inaanza robo fainali.

Hatua ya mtoano ilikuwa nzuri na ya kuvutia ikishuhudia wababe  wa soka barani Afrika Misri, Senegal na Morocco wakitolewa huku mwenyeji Ivory Coast wakifanikiwa kufuzu pasipo kutegemewa.

Mechi za Misri na Senegal zililazimika kuchezwa kwa dakika 120 baada ya dakika 90 kuwa sare ya bao 1-1 na dakika 30 ziliongezwa, lakini  hakuwa na mshindi na hatimaye kuangukia katika penalti.

Katika mechi hizo wachezaji wa timu zote tangu walipokuwa wanapasha mpaka wanamaliza kupiga mikwaju ya penalti walionekana wakiwa wametoka jasho jingi isivyo kawaida.

Hii ni kutokana na ukweli kuwa mashindano yanafanyika katika kipindi ambacho nchi hiyo ambayo iko Magharibi mwa Afrika kuwa na joto la kiwango cha juu cha nyuzijoto 31 wiki hii.

Hali hiyo ya joto kali ndio sababu ya Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) kutoa mwongozo maalumu juu ya mapumziko mafupi kwa kila mechi au mashindano yanayochezwa katika maeneo yenye joto kali.

Ndio maana katika kila mechi inayochezwa katika mashindano hayo inapofika dakika 30 kipindi cha kwanza na ya 75 kipindi cha pili mwamuzi husimamisha mchezo na kutoa mapumziko ya dakika tatu.


Mapumziko hayo ni maalumu kabla ya yale mapumziko ya kipindi cha kwanza cha dakika 15. Lengo huwa ni kujikinga na kukabiliana na madhara ya kiafya kutokana na kupoteza maji mengi na chumvichumvi mwilini kwa njia ya jasho.

Katika jambo hilo timu ya wataalamu wa afya na timu zote zinajua hatua hizo mathubuti ni kwa ajili ya kukabiliana na athari zinazotokana wachezaji kucheza katika joto kali.


HATUA NI HIZI
Kutokana na uelewa mpana walionao wataalamu wa afya ambapo hushikamana na mwongozo wa kukabiliana na madhara ya joto kali na hatua za kuchukua wakati wa dharura zinazotokana na joto kali.

Hapa mchezaji hupatiwa huduma za kukabiliana na upungufu wa maji na kuupoza mwili, huku pia akipewa matibabu salama kwa yale madhara ya wastani yaliyotokana na joto kali.
Ikumbukwe kuwa upungufu wa maji na chumvichumvi mwilini ni tatizo ambalo linapokuwa kubwa linaweza kuwa la kiafya la dharura kwani mwathirika anaweza kuanguka na kupoteza fahamu au kufariki dunia.

Ndio maana nchi wenyeji waandaji wa mashindano hayo na wageni wote wanatambua vyema hatua zote mathubuti za kukabiliana na madhara ya kiafya yanayotokana na joto kali.
Katika mechi ya Jumapili kati ya Misri na DR Congo wakati wakijiandaa kipindi cha nyongeza na kabla ya penalti mabenchi ya ufundi yalitumia barafu zilizovunjwa vunjwa, maji na taulo zenye majimaji baridi.

Haikushangaza kwani ni vitu salama kwa ajili ya kukabiliana hali hiyo ikiwamo kutumika kupoza mwili kwa haraka ili kuusaidia kupoa na hivyo mzigo wa kukabiliana na joto kali hupungua hatimaye mchezaji kurudi uwanjani na nguvu mpya.

Maji wanayopewa kunywa na vinywaji maalumu vya wanamichezo huwasaidia kurudishia maji na chumvi chumvi mwilini zilizopotea kwa njia ya jasho.

Hushauriwa kunywa maji hayo kwa kiasi na si kubugia kwa haraka na kwa mkupuo. Siku mbili kabla ya mechi wachezaji hushauriwa kunywa maji lita 2.5 hadi 3 kwa siku na saa mbili kabla ya mechi hutakiwa pia kunywa maji kidogokidogo angalu lita moja.

Sehemu walizofikia hushauriwa kula matunda na mboga mbichi kwa wingi kila baada ya mechi. Vitu hivyo huwa na maji mengi na chumvichumvi au madini, hivyo kuwapa kiasi cha maji na madini.
Mavazi wanayotumia nje na ndani ya uwanja ni rafiki kwa mazingira ya joto.


MADHARA YA JOTO KWA WACHEZAJI
Kwa sasa hali joto iliyopo katika nchi ya Ivory Coast ni nyuzijoto 31 na kadri joto linavyozidi kuwa juu na ndivyo mwanadamu anavyokuwa katika hatari ya kupoteza maji kwa njia ya jasho.

Upungufu wa maji mwilini ni jambo ambalo linaweza kujitokeza wakati wowote. Kwa kawaida mwili huhitaji maji na chumvichumvi kwa ajili ya kazi mbalimbali za mwili ikiwamo msukumo wa damu na kazi za seli mbalimbali.
Wachezaji wanapokuwa katika mazingira ya joto huku wakifanya mazoezi makali au kucheza mechi zenye ushindani hutokwa na jasho jingi, hivyo kupoteza maji mengi na chumvi mwilini.

Inakadiriwa katika mashindano kama hayo kwa mchezaji anayecheza dakika 120 anaweza kupoteza kiasi cha maji kwa njia ya jasho na kupumua yanayofikia lita 2 - 3.
Ikumbukwe kuwa kadri joto linavyozidi kuwa kali ndivyo mwili unavyotoa jasho zaidi, lengo ni kupunguza joto la ndani ya mwili lisizidi kiwango cha mwisho.

Kuvuja jasho sana huwa ni zaidi wakati wa kucheza katika joto kali. Wakati huohuo kadri jasho linavyotoka kwa wingi na ndivyo pia mwili unavyopoteza maji kupita kiasi.

Matatizo mbalimbali ya kiafya yanaweza kujitokeza endapo tu mchezaji atapata upungufu mkali wa maji mwilini na chumvichumvi kutokana na kuvuja jasho.

Hali hiyo inaweza kuambatana na madhara katika viungo ikiwamo kuuma na kubana kwa  makundi ya misuli ikiwamo ya ile ya nyuma ya paja ambayo ni muhimu kwa mchezaji kama wa soka.

Upungufu wa maji na chumvi mwilini usipokabiliwa kwa kuupoza mwili na kurudishia kiwango cha maji kilichopungua inaweza kuleta madhara makubwa kiafya na hata kifo.

Matatizo hayo ni pamoja na kupata maumivu ya kichwa na mwili kuuma, mchoko mkali, kiharusi kitokanacho na joto kali na kupoteza fahamu.

Madhara mengine ni pamoja na kuona mawimbi, kuishiwa nguvu, kuhangaika, kukosa umakini, udhaifu katika uamuzi na kuchanganyikiwa.

Unaweza ukawa una maji mwilini, lakini kuwepo tu katika hali ya joto nayo inaweza kuleta madhara mbalimbali ya kiafya kwa mchezaji au mtu mwingine yeyote aliyepo katika mazingira hayo.

CHUKUA HII
Upungufu wa maji na chumvichumvi unaotokana na kuvuja jasho katika joto, na unaweza kumuathiri mchezaji akashindwa kucheza kwa kiwango bora na hatimaye kuonekana yupo chini ya ufanisi uliozoweleka kwake.