Rekodi sita Simba zinavyoitesa Yanga

YANGA msimu huu imeonekana haitanii kwani kuna jambo inalitaka kutokana na mwendo ilionao kwenye Ligi Kuu.
Hakuna kingine ambacho kinawafanya Yanga kupambana zaidi uwanjani chini ya kocha Nasreddine Nabi isipokuwa kuteswa na rekodi ambazo Simba wameziweka kwa misimu minne mfululizo.
Gazeti hili linakuletea rekodi tano za Simba zinazoitesa Yanga kwa kipindi hicho.
Ubingwa wa ligi kuu
Tangu 2018 Simba imechukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara nne mfululizo jambo ambalo linawaumiza Yanga. Licha ya kwamba Yanga iliwahi kuchukua ubingwa mara tatu mfululizo msimu wa 2014/2015 hadi 2016/2017 lakini wapinzani wao hao kuwapokonya tonge kisha kuchukua mara nne mfululizo inawatesa.
Rekodi ya mabao
Achana na hiyo rekodi ya ubingwa mara nne mfululizo ambayo Yanga inatakiwa kuivunja dhidi ya Simba, lakini kingine Wekundu wa Msimbazi wanaongoza kwa mabao ya kufunga na kuruhusu machache kwenye ligi kwa miaka minne.
Msimu wa 2017/ 2018 ambao Simba iliwapokonya Yanga ubingwa ilimaliza ikiwa imefunga mabao 62 na kuruhusu 15 wakati Yanga ilimaliza ligi katika nafasi ya tatu ilifunga mabao 44 na kuruhusu 23. Msimu uliofuata (2018/2019) Simba waliibuka mabingwa wakiwa wamefunga mabao 77 na kuruhusu 15 wakati Yanga iliyokuwa ya pili ilifunga 56 na kuruhusu 27 na msimu wa 2019/2020 Simba walitwaa ubingwa wakifunga mabao 78 na kuruhusu 21 wakati Yanga walimaliza kwa kufunga mabao 45 na kuruhusu 28 huku msimu uliopita Simba walimaliza kwa kufunga mabao 78 na kuruhusu 14 wakati Yanga walifunga mabao 52 na kuruhusu 21.
Ufungaji Bora
Rekodi nyingine inayoitesa Yanga ni hii ya ufungaji bora wa Ligi Kuu Bara kwani tangu Simon Msuva alipopeleka tuzo hii Jangwani msimu wa 2016/2017 hakuna mchezaji mwingine wa timu hiyo aliyeweza kunyakua tena kiatu cha dhahabu.
Tangu Msuva afanye hivyo miaka minne iliyofuata tuzo hiyo imekwenda Simba akianza Emmanuel Okwi msimu wa 2017/2018 alipoibuka mfungaji bora kwa kufunga mabao 20 kisha msimu uliofuata 2018/2019 akafuatia Meddie Kagere aliyefunga mabao 23, huku pia akichukua tuzo hiyo msimu wa 2019/2020 kwa kualiza ligi na maabo 22 wakati msimu uliopita tuzo hiyo ilibebwa na John Bocco aliyefunga mabao 16.
Ubingwa wa ASFC
Yanga ilikuwa timu ya kwanza kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) mara tu baada ya mashindano hayo kurejeshwa msimu wa 2015/2016 na baada ya hapo haikuchukua tena.
Timu hiyo ina kibarua kingine msimu huu na ijayo cha kuvunja rekodi ya Simba kwa kuchukua ubingwa wa michuano hiyo mara mbili mfululizo. Simba imebeba ubingwa wa ASFC mara mbili mfululizo msimu za 2019/2020 na 2020/2021, hivyo kama itafanya hivyo msimu huu itakuwa mara ya tatu, lakini watoto wa Jangwani wanatakiwa kuchangamka ili kuharibu rekodi hiyo na kuanza kuitengeneza yao.
Hata hivyo, kabla ya michuano hiyo kubadilishwa jina kutoka FA, Yanga ndio iliyokuwa wababe kwa kutwaa taji hilo mara nyingi kuliko klabu yoyote ikibeba mara nne ikifuatiwa na Tanzania Stars iliyobeba mara mbili, Simba ilibeba mara moja tu kabla ya kucharuka michuano ikifahamika ASFC.
Robo Fainali Afrika
Kwa miaka minne mfululizo Simba haijatisha kwenye Ligi Kuu tu, bali hata michuano ya kimataifa imeng’ara na kuweka rekodi kadhaa.
Ndani ya misimu hiyo imetinga robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika mara mbili na makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu. Licha ya kwamba Yanga 1998 ilifika hatua ya makundi ya michuano hiyo pia iliwahi kutinga robo fainali 1969 na 1970 wakati ikifahamika kama Klabu Bingwa Afrika kabla ya kubadilishwa jina 1997 na kuitwa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Hata hivyo, Simba waliwahi kufika nusu fainali ya michuano hiyo 1974 na kutinga robo fainali 1994 na hatua ya makundi 2003, huku ikitinga fainali ya Kombe la CAF 1993.
Licha ya kipindi hicho Yanga nayo kuwahi kutinga kwenye hatua hizo, lakini bado ina deni la kuzilipa rekodi za Simba walizoweka miaka minne ya karibuni.