NYUMA YA PAZIA: Mbappe, Haaland na msiba mzito wa El Clasico

NYUMA YA PAZIA: Mbappe, Haaland na msiba mzito wa El Clasico

WAKO wapi waliokuwa wanasema watu wafupi wanaongea sana na ni waongo? Alikosea sana! Mtu mmoja mrefu mwenye futi 6’5 mapema wiki iliyopita alikuwa amekaa mbele ya vipaza sauti akidanganya watu. Nilicheka sana.

“Nimekuwa shabiki wa Manchester City kwa maisha yangu yote. Nadhani naweza kujiendeleza zaidi hapa chini ya Pep Guardiola na kufunga mabao mengi. Napenda zaidi staili yao ya mchezo.” Alikuwa akisema mtu huyu.

Namzungumzia Erling Haaland, baada ya kukamilisha uhamisho wake wa kwenda Manchester City mapema wiki hii. Nilitabasamu. Alishindwa tu kuongeza kwamba; “Dau lao la mshahara lilikuwa kubwa lakini dau lao la kusaini mkataba wao lilikuwa halikataliki.”

Hayo maneno hakusema; lakini ndio ukweli wa moyoni kuliko kile ambacho alikuwa anakisema. Pesa ni sabuni ya roho. Zimepita zama ambazo watu walikuwa wanaendeshwa na mapenzi. Kwa sasa pesa mbele. Kabla ya kila kitu unazingatia kwanza dau kubwa lililopo mezani kwako. Kwamba yeye ni shabiki wa Man City inawezekana ni kweli kwa sababu baba yale, Alf Inge Haaland aliwahi kucheza Manchester City kwa miaka mitatu.

Lakini zamani kidogo Haaland aliwahi kutuambia kwamba yeye ni shabiki wa Leeds United na angetamani siku moja kucheza Leeds. Kisa? Alizaliwa katika jiji la Leeds wakati baba yake akicheza hapo kabla hajaenda Manchester City.

Hili la kwamba yeye ni shabiki wa City limechochewa na dau alilopewa na City nyakati hizi. Wakati yeye akitudanganya hivi, katika jiji la Paris nchini Ufaransa, staa mwenzake wa soka la kisasa, Kylian Mbappe naye pia alikuwa akitudanganya kwamba ana mapenzi na PSG, ndio maana ameamua kubakia klabuni hapo na hataki kwenda Real Madrid.

Mastaa wa kisasa wanachoangalia ni pesa tu. Kama ingekuwa miaka kadhaa nyuma basi Haaland alikuwa anakwenda Barcelona halafu Mbappe alikuwa anakwenda Real Madrid. Kulikuwa na mambo mawili kwa mpigo hapo nyuma. Madrid na Barcelona zilikuwa na majina ya heshima na ya kihistoria, pia walikuwa na pesa. Hawa Mbappe na Haaland wote wangependa kucheza Madrid na Barcelona.

Na kama ingekuwa nyuma kidogo hawa Mbappe na Haaland wote wangependa kucheza Manchester United. Hata hivyo kibao kimegeuka. Kuna pesa za Mwarabu zimewachukua na hivyo na wao wanafuata mkumbo wa mastaa wa kiwango cha dunia (World Class) ambao wamekacha historia kwa sababu ya pesa.

Uliwahi kudhani mchezaji kama Kelvin de Bruyne angecheza Manchester City katika kipindi kirefu cha ubora wake bila ya kugusa Real Madrid wala Barcelona? Vipi kuhusu David Silva? Vipi kuhusu Vincent Kompany?

Zamani mastaa wote wakubwa walikuwa wametengenezewa hatma ya kucheza Barcelona au Real Madrid. Sasa hivi kibao kimebadilika. PSG wamekufuru kwa Mbappe katika namna ambavyo Mbappe ameachana na kila kitu kwa ajili ya PSG.

Mbappe anajua kwamba angekuwa katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa wa Ulaya akiwa na Real Madrid. Anajua kwamba angekuwa katika nafasi nzuri ya kutwaa tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia akiwa na Madrid kuliko PSG. Hata hivyo, amechagua kubakia PSG kwa sababu ya pesa.

Kwa upande wa rafiki zangu Barcelona wamechoka kiasi kwamba wala hawakujisumbua sana kwa Haaland. Sawa walimtamani, lakini hesabu zao za pesa haziwaruhusu kuwa na Haaland. Kama walishindwa kumbakiza Lionel Messi wangewezaje kwa Mbappe. Vitabu vyao vya mambo ya pesa haviruhusu kuwa na mastaa wakubwa.

Na sasa ni kama vile mechi ya El Clasico itaendelea kuwa ya kawaida tu. mechi hii inajengwa zaidi kwa mvuto wa mastaa wakubwa. Zamani mechi hii imewahi kuwa na akina Ronaldo de Lima, Cristiano Ronaldo, Romario, Luis Figo, David Beckham, Roberto Carlos, Rivaldo, Raul Gonzalenz, Ilker Casillas na wengineo wengi.

Leo wachezaji wanaostahili kuikuza El Clasico wanacheza katika timu za matajiri wa Kiarabu. Baada ya kuondoka kwa Messi na Ronaldo, El Clasico nayo imezidi kupoteza mvuto. Mastaa wa El Clasico walipaswa kuwa hawa hapa kina Haaland, Mbappe, Kelvin de Bruyne na wengineo.

Haishangazi kuona La Liga walikasirika na kwenda kulia UEFA baada Mbappe kuamua kubakia Paris. Ilishangaza na kuchekesha. Ni kweli Mbappe alishakubaliana maslahi binafsi na Madrid lakini hakusaini mkataba wao. La Liga waliumia kwa sababu gani?

Wanajua kwamba ndani ya bidhaa yao adimu inayoitwa La Liga wanahitaji bidhaa nyingine za kuiuza Ligi yao kwa walaji waliosambaa duniani kote. Miongoni mwa bidhaa hizi ni kama vile Mbappe na Haaland.

Lakini kwa sasa ni wazi kwamba wameumia. Wataendelea kuwa na mtu kama Karim Benzema ambaye ni mchezaji mkubwa na wanaweza pia kumpata Roberto Lewandowski. Lakini England ina mastaa wakubwa zaidi kina Haaland na Ronaldo hata kama siku zake za kucheza soka katika kiwango cha juu zinakaribia kumalizika.

Kama hauna Messi au Ronaldo basi walipaswa kuwa na Haaland na Mbappe lakini hadithi imekwenda tofauti. Majuzi nimecheka tena baada ya La Liga kuzishtaki zote kwa pamoja PSG na Man City kwamba zinakiuka misingi ya utumiaji pesa kwa mujibu wa kanuni za Uefa. Hii nayo imenichekesha.

Nadhani wote tunafahamu kwamba City haijawahi kuziba pengo la Sergio Aguero. Lakini ni wazi kwamba Gabriel Jesus anakwenda Arsenal. Ina maana mishahara yao inaweza kwenda kwa Haaland. Lakini City hawajavunja benki kumchukua Haaland. Dau lake la kuondoka klabuni hapo lilikuwa kidogo tu.

Hata hivyo ni wakati pia wa kukumbuka jinsi klabu mbalimbali duniani zilivyoteseka na pesa za Florentino Perez katika zama za Galactioz. Wakati ule La Liga ikikusanya kina Zinedine Zidane kwa lazima kutoka katika pande nyingine za Ulaya La Liga walikuwa wamekaa kimya tu. leo wanataka tulie pamoja.

Manchester United ni miongoni mwa wahanga waliowahi kukumbana na makali ya pesa za Real Madrid. Nyakati zile walipolazimishwa kuachana na Cristiano Ronaldo kwa dau lililoishtua dunia mwaka 2009. Rafiki zangu La Liga walikuwa wanakenua tu. Leo pesa za Waarabu zimeharibu kila kitu na zimeharibu hata mechi yenyewe ya El Clasico.