Kwanini Derby ni ngumu kwa Niyonzima?

Sunday July 18 2021
niyo pic

KUNA waandishi wa habari wawili ambao nilikuwa napata starehe kuwasikia wakimsifu nahodha wa zamani wa Yanga, Haruna Niyonzima, wakati akiwa kwenye ubora wake takribani miaka saba au nane hivi iliyopita.

Waandishi hao Hemed Kivuyo wa ITV na Khatimu Naheka wa MwanaSpoti, walipenda sana kumwita kwa majina manne; Haruna Fadhili Hakizimana Niyonzima. Nadhani ndiye mchezaji pekee wa soka hapa Tanzania ambaye majina yake yote manne yalikuwa yakitajwa kwa wakati mmoja; mara moja.

Niyonzima alikuwa mchezaji ambaye sisi wapenzi hasa wa kabumbu tunaoitwa romantics, yaani wale tunaoamini kuna aina fulani ambayo soka inatakiwa ichezwe tungependa awe kwenye timu yetu.

Ni jambo la furaha kwamba amekaa Tanzania nasi kumwona wakati akiwa katika kiwango cha juu cha kusakata soka. Mimi ni shabiki wa Simba na wakati nikiwa kiongozi miaka nane iliyopita, nilikuwa mmoja wa waliokuwa wakitamani siku moja avae uzi mwekundu wa Mtaa wa Msimbazi.

Baadaye alikuja kuvaa jezi nyekundu lakini sidhani kama aliweza kuwachota washabiki wa Simba kwa kiwango alichokuwa anapendwa na washabiki wa Yanga. Mfalme wa Simba alikuwa Emmanuel Okwi wakati huo na majeraha labda na sababu nyingine za kisaikolojia, zilimnyima Haruna fursa ya kung’ara sana akiwa Simba.

Hata hivyo, moyoni mwangu, sina shaka yoyote kwamba Haruna ni miongoni mwa wachezaji wa kigeni waliokuja kucheza Tanzania na kutuonyesha thamani halisi ya wachezaji wa kulipwa.

Advertisement

Na wala sishangai kwamba wakati Rwanda ikiwa imetokea katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 na ikianza kujenga upya taifa lisilo na ubaguzi kwenye miaka ya 2000, Haruna alikuwa ni mmoja wa wachezaji waliofanikisha hilo.

Niyonzima alikuwa kiungo wa wachezaji wa viungo. Kwenye ubora wake alikuwa anajua nini cha kufanya na mpira, madoido na pasi zake za mwisho hazikuwa na mfanowe Rwanda na hata alipokuja Tanzania.

Wakati mwingine wala hakuhitaji kutoa pasi. Katika mechi ya kukumbukwa zaidi kwake wakati akiwa na Simba, nadhani katika pambano dhidi ya Nkana Red Devils ya Zambia, Niyonzima alipika bao la Wekundu la Msimbazi kwa kuachia mpira uburuzike kwenye miguu yake bila kuufanya kitu (faint) ili kutoa nafasi kwa Meddie Kagere aliyekuwa katika nafasi nzuri zaidi kupachika bao.

Kitaratibu haiwezi kuhesabika kuwa ni pasi ya goli kwa sababu mpira haukutoka kwake lakini alichokifanya kiliwapoteza maboya walinzi wale wa Zambia na kipa wao. Kazi ya mfungaji ikawa ni kupasia tu nyavu. Alichofanya Niyonzima pale kilihitaji kufikiri kwa haraka na kufanya uamuzi hapo hapo. Si sifa ndogo kwa wachezaji.

Enzi nikiwa kiongozi wa Simba, nakumbuka kwamba Yanga ilikuwa na wachezaji wawili hatari; Niyonzima na Simon Msuva ambaye sasa anakipiga nje ya nchi. Wawili hawa ndiyo waliokuwa wanaifanya icheze kwa staili yake yenyewe.

Msuva alikuwa na kasi kubwa na Niyonzima alikuwa anajua ni wakati gani wa kukaa na mpira na upi wa kuachia kwa uzito na ukali upi, ili pasi imfikie Simon katika eneo la hatari.

Kwenye mechi nyingi za Watani wa Jadi, nilikuwa nikiona namna walimu wa Simba wa nyakati hizo walivyokuwa wakitengeneza mipango na mikakati maalumu ya kuzuia Msuva na Niyo wasiwe na madhara langoni kwao. Kwa makocha mahiri, lilikuwa ni jambo la kusisitiza mazoezini wakati wote.

Faida moja ya kucheza na timu kama Simba, Yanga au Azam ambazo zina makocha wa kiwango cha kuridhisha ni kwamba mtaalamu anakuwa anajua namna zinavyocheza. Kwa sababu hiyo, ni rahisi kwa mpinzani kutengeneza namna ya kupambana na mbinu hizo.

Dhidi ya Yanga ya Msuva na Niyonzima, makocha wa Simba walikuwa wanazuia ngome isiache nafasi kubwa ya nyuma ambayo Msuva anaweza kumzidi mtu spidi na Niyonzima alikuwa anapewa mtu wa kutembea naye na mfumo mzima wa kuzuia pasi zake.

Kila timu ya Tanzania ilikuwa inaweka mtu wa kutembea na Niyonzima. Tofauti ya Simba na timu nyingine ni kwamba mchezaji wa Wekundu wa Msimbazi anayepewa jukumu hilo anakuwa bora kuliko wengi wa klabu nyingine lakini pia anakuwa amefundishwa vizuri kuhusu jinsi ya kumkaba Haruna.

Kuna tofauti ya kuambiwa tu nenda kamkabe Niyonzima na kufundishwa namna ya kumkaba. Wachezaji wa timu kubwa walikuwa wakiambiwa namna ya kumkaba lakini wengine waliambiwa tu wamkabe.

Haikuwa ajabu kwamba Msuva na Niyonzima hawakuwa na madhara sana wakati wa mechi za watani wa jadi. Haikuwa kwamba walikuwa na mahaba makubwa na Simba kiasi cha kushindwa kufanya makubwa lakini sababu ilikuwa walikuwa wanakabwa sana kimbinu.

Ni kama Simba ilikuwa ina mfumo wa kumzuia yeye na Msuva wasicheze. Na wakati huo, kama Msuva na Niyo hawafanyi kazi, maana yake ni kwamba Yanga inakuwa haina madhara.

Kina ‘Mzee Mpili’ walikuwa wanachukua sifa kwamba wao ndiyo huwazuia kina Niyo wasicheze, lakini ukweli ni kwamba mbinu za kuwazuia zilikuwa zinatokea viwanja vya mazoezi na wachezaji wenyewe kufanya kazi hiyo.

Kila la kheri kwa Haruna Fadhili Hakizimana Niyonzima kwa lolote atakalopanga kulifanya katika maisha yake kuanzia sasa.

Natamani sana kwamba kama klabu zetu zinaamua kwenda nje, basi watuletee kina Niyonzima. Si akina, aaargh, Sarpong.


IMEANDIKWA NA EZEKIEL KAMWAGA

Advertisement