KIJIWE CHA SALIM SAIDI SALIM: Da silva baiskeli ya Brazil iliyoacha maufundi kibao

MAZISHI duniani kote na hata hapa kwetu yanachukua taswira tofauti kutokana na imani za dini, mitazamo ya jamii, makabila na utamaduni wa watu. Baadhi ya mambo yatayokushangaza huwa ya kawaida kwa jamii nyingine na kama ukistaajabu ya wenzako na wao watapigwa na butwaa na unavyomuaga maiti kwa safari ya mwisho hapa duniani.

Lakini mazishi mengine naamini kwa Watanzania wengi yanaonekana sio ya kawaida kwa vile huwa na vituko vya aina yake. Njia salama ni kuyakubali kuwa wanaofanya hivyo wanaona ni njia sahihi ya kumuaga mwenzao aliyemaliza mkataba wa kuishi duniani. Hali hii pia tunaiona anapoagwa mwanamichezo maarufu.
Sasa ni miaka 19 tangu mchezaji kandanda maarufu wa Brazil, Leonidas da Silva kuiaga dunia, lakini yaliyotokea siku ya mazishi yake yanazungumzwa kama sio ya kawaida. Hii ni kwa sababu vijana wengi waliokwenda makaburini kumzika walipanda baiskeli yenye mipira iliyokuwa inaning’inia pembeni.
Vijana hao walifanya hivyo kukumbuka ustadi wake wa kufunga mabao kwa makombora yaliyojulikana kama bicycle kicks (mipira inayopigwa kama ya mtu anayeendesha baiskeli). Wakati wa uhai wake alipata umaarufu kama mchezaji mwenye mbwembwe na chenga zilizowaudhi wapinzani na mashabiki waliofika uwanjani.

Da Silva aling’ara miaka ya 1920 na 1930 kwa kufunga mabao kwa michomo ya baiskeli, kichwa chake kikielekea goli la wapinzani na kuupiga mpira uliopita juu ya kichwa chake au mabega na kutikisa nyavu. Alifunga mabao mengi kwa staili hii kuliko namna nyingine.

Wataalamu wa kandanda wa zama zile walisema Leonidas ndiye aliyebuni kionjo hiki katika kandanda na wanaamini mpaka leo si Brazil tu atatokea mchezaji mwenye ustadi mkubwa wa kupiga mipira kwa staili hii na kufunga kama yeye, bali duniani kote.
Alijulikana kama Black Diamond (Almasi Nyeusi) kutokana na rangi yake. Baba yake alikuwa baharia wa Kireno na mama alikuwa mzaliwa wa Brazil mwenye asili ya Kiafrika. Mwenyewe alikataa kuitwa Mreno, bali Mbrazili wa Kiafrika (Afro Brazil), lakini wengi Brazil walipenda kumuita Magia Negra yaani Mchawi Mweusi. Wakati alipotamba Brazil haikuwa maarufu kwa kandanda kama ilivyo sasa.
Brazil ilipoanza kuwa na wachezaji wa kulipwa 1930 Da Silva aliajiriwa na klabu kubwa moja baada ya nyingine kila msimu ulipoanza.

Japokuwa alikuwa na umbo dogo alihimili vikumbo vya wababe na alikuwa mwepesi kukwepa mateke na kuwapenya mabeki. Alipata umaarufu alipojiunga na klabu ya Bonsuccesso ya Rio de Janeiro 1931. Rio ilipocheza na Sao Paolo ili kuamua klabu itayochukua ubingwa alifunga mabao mawili yote kwa baiskeli na kuiwezesha timu yake kushinda kwa mabao 3-0.
Baada ya mchezo alichaguliwa kujiunga na kikosi cha Brazil kilichokutana na Uruguay katika mashindano ya Kombe la Rio Branco.
Wakati huo alikuwa mchezaji wa akiba, lakini baada ya  mwaka mmoja akawa mchezaji wa kutegemewa na alifunga mabao yote mawili Brazil ilipokutana na Uruguay na kushinda 2-1 katika Jiji la Montevideo, Bolivia.

Baada ya mchezo alisema: "Nimefunga bao moja na nusu kwa sababu lile la kufunga kwa kuupiga mpira unaomgusa mchezaji mwingine ninalihesabu kama nusu bao." Hapo ndipo klabu ya Panarol ya Uruguay ilipoamua kumsajili 1933 na mwaka uliofuata alirudi Brazil na kuchaguliwa katika kikosi kilichocheza Kombe la Dunia.
Kabla ya kuchomoza kuwa mchezaji nyota wachezaji wa Brazil walikuwa wanabaguana, lakini kwa vile yeye alikuwa mseto wa Mzungu na Mwafrika na wote walimpenda, ikawa ndio kiungo kati ya pande hizi mbili kumaliza ubaguzi uliokuwepo. Silva alikuwa kivutio kwa mchezo wake Ulaya zilipofanyika fainali za Kombe la Dunia 1938 nchini Ufaransa.

Katika mchezo wa kwanza wa Brazil ilipopambana na Poland, Silva alifunga mabao yote matatu katika kipindi cha kwanza. Mvua kubwa ilinyesha kipindi cha pili na hali hiyo ilimpa shida na kuamua kuvua viatu na kucheza peku, lakini mwamuzi alimkatalia. Brazil ilishinda mabao 11-4 na baadaye ikatoka sare na Czechoslovakia.
Kilichowashangaza watazamaji ni kocha kumfanya mchezaji wa akiba katika mchezo uliofuata na Italia. Brazil ilifungwa na kocha ilimlazimu kumrudisha katika mchezo na Sweden na Brazil kushinda, lakini matokeo hayakuisaidia Brazil kubeba kombe. Silva alifunga  mabao manane katika fainali hizo na kupokewa Brazil kama shujaa wa timu hiyo iliporudi nyumbani.

Mwaka 1941 aliingia matatani kwa kughushi hati ya kuzaliwa ili asijiunge na jeshi na alifungwa miezi minane jela. Alipotoka gerezani alijiunga na Flamengo na kuchezea miaka yote ya 1940 na kuwa klabu bingwa miaka mitano kati ya saba aliyoichezea. Mwaka  1942 alisajiliwa na Sao Paolo ambayo aliifungia mabao 14 na kuisaidia kutwaa ubingwa. Alijiuzulu 1949 na kwa muda mfupi alikuwa kocha wa Sao Paolo.
Vilevile alikuwa mtangazaji wa mpira wa kituo cha redio na alipostaafu wachezaji wengi duniani waliigiza mfumo wa kupiga mashuti ya baiskeli, lakini hakuna aliyefikia utaalamu na ustadi wake. Katika siku za mwisho za maisha yake alifurahia kupanda baiskeli huku akiugua kisukari na kuwa mtu mwenye kusahau. Wakati mwingine ilimchukua muda kukumbuka jina lake. Siku moja alisahau nyumba yake ipo wapi na vijana walimsaidia kumpeleka nyumbani. Alifariki dunia Januari 24, 2004 akiwa na umri wa miaka 90 na mazishi yake yalivyofanyika huzungumzwa mara kwa mara Brazil.

Da Silva anakumbukwa kwa mchezo wa kufunga mabao ya baiskeli na kusaidia kuvunja ukuta wa ubaguzi kati ya watu wenye asili ya Kizungu na wenye asili ya Kiafrika. Alipofariki, Mfalme wa Kandanda, Pele wa Brazil alisema: "Brazil imepoteza baiskeli ya dhahabu na aliyeiendesha”. Nyimbo maarufu ya Da Silva isemayo: "Sote ni wamoja… sote ni watoto Brazil na sote ni watoto wa Adam na Hawa” huimbwa katika viwanja vya mpira vya Brazil.