Prime
KASONGO: Wachezaji, maofisa wanaobeti kazi wanayo!

Muktasari:
- Kauli hiyo ya kushtua ya Mtanda ambaye pia ni mshauri na mlezi wa Pamba Jiji aliitoa jijini Mwanza wakati wa hafla ya chakula cha usiku na wachezaji, benchi la ufundi na menejimenti ya klabu hiyo.
UNAKUMBUKA kauli iliyotolewa hivi karibuni na mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda kuwa kuna wachezaji wa timu ya Pamba Jiji wanaowachunguza kuhusika katika michezo ya kubashiri (betting) na kupanga matokeo?
Kauli hiyo ya kushtua ya Mtanda ambaye pia ni mshauri na mlezi wa Pamba Jiji aliitoa jijini Mwanza wakati wa hafla ya chakula cha usiku na wachezaji, benchi la ufundi na menejimenti ya klabu hiyo.
"Hivi vitu vipo na vinatokea. Sasa wewe tunakulipa mshahara Sh3 milioni mpaka Sh4 milioni halafu unabashiri Pamba ipoteze.. sasa nimepeleka namba zenu TCRA (Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania) yeyote atakayebeti nitaona na ni rahisi kwangu,” alisema Mtanda.
“Kuna mchezaji mwenzenu nilimwambia mlipokwenda kucheza na Namungo alikuwa anashawishi wenzake muuze mechi na ukitaka ushahidi nitakupa, nikamkanya aache. Nawaonya muache kwa sababu ushahidi ninao na sitaki mambo haya yaendelee."
"Sitaki kutaja majina, lakini nimeshaongea na baadhi yenu wengine wanatumia simu za wake zao kupokelea hiyo miamala. Hivyo nawaonya hii ni timu ya taasisi ya serikali ambayo fedha nyingi zinatumika ambazo zingeenda kwenye miradi mingine."
Kutokana na madai hayo, Shirikisho la Soka Duniani (Fifa), limepiga marufuku watu mbalimbali wanaohusika na klabu kujihusisha na masuala ya kubashiri na kuna kanuni zinazoonyesha ni watu gani hawaruhusiwi kubeti na iwapo watafanya hivyo, hatua gani zitachukuliwa kama ilivyowakuta baadhi ya mastaa wa soka waliowahi kufungiwa au kutozwa faini na kufungiwa kujihusisha na mchezo huo kwa kipindi fulani.
Kule Italia, Juventus iliwahi kushushwa daraja kutokana na tuhuma hizo kuwaandama maofisa na hata wachezaji, huku wa hivi karibuni kabisa ni Sandro Tonali anayekipiga Newcastle United kwa sasa. Lakini kwa England, nyota kadhaa wameshaadhibiwa kwa kujihusisha kubeti akiwamo Ivan Toney aliyekuwa Brentford ambaye alifungiwa kwa miezi minane.
Kwa sasa nyota anayekabiliwa na mashtaka ya kubeti ni Lucas Paqueta ni wa West Ham United.
Kutokana na tuhuma hizo kudaiwa kuwepo katika soka la Tanzania, Mwanaspoti limefanya mahojiano na ofisa mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi (TPLB), Almas Kasongo ambaye amezungumza mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na namna walivyoanza kuifanyia kazi kauli ya Mtanda kwa kuunda kamati ya uchunguzi.
KUBETI? KAMATI IMEUNDWA
Kasongo anasema TPLB imeamua kuanza kuchunguza tuhuma mbalimbali zinazohusiana na wachezaji au maofisa wa klabu kujihusisha na ubashiri wa matokeo katika michezo ya soka nchini.
"Tuna kanuni na kanuni ni kali, na inaeleza ni watu wa aina gani hawapaswi kujihusisha (kubashiri), lakini ipo minong'ono na mazungumzo yanazungumzwa kwamba kuna watu kutoka ndani ya mpira wanafanya hivyo," anasema Kasongo.
"Tumeunda kamati ambayo inashughulikia, tumelichukulia kwa uzito kwa sababu ni jambo baya. Tukiliacha litaharibu taswira ya mpira wetu ambao upo kwenye nafasi ya nne kwa ubora."

Anasema kamati hiyo inafanya kazi kimyakimya ili kubaini kinachozungumzwa na kama yanayozungumzwa ni kweli, Bodi inatoa onyo kali kwa sababu wanaofanya hivyo wakibainika hawataachwa salama.
"Kimya kingi kina mshindo kama yanayozungumzwa ni tetesi tu ni vizuri kwetu. Lakini kama yana ukweli, hilo jambo halina afya wala halina tija kwao wanapoteza fani zao, vipaji vyao na yale ambayo wangeweza kuwa sehemu ya kusaidia familia zao," anasema Kasongo.
Anasema wanaendelea kufukuza mwizi kimyakimya na watakapofanikiwa kuwanasa wataviita vyombo vya habari kuzungumzia jambo hilo kuanzia walipoanza na walipopata uthibitisho.
"Kwa kweli tutawapoteza kama ambavyo kanuni zinatukata kufanya. Kamati iliyoundwa inaendelea na mchakato wa kufanyia uchunguzi, tutakapotoka ndio kishindo kitakaposikika."
UBORA WA LIGI
Ligi Kuu Bara inatajwa kuwa namba nne kwa ubora Afrika 2025 kutoka namba sita, na Kasongo anaeleza sababu za ubora huo huku akizitaja Simba na Yanga kuwa ndizo zimechangia kukua kwa ligi.
"Kutoka nafasi ya sita hadi ya nne ni kazi kubwa imefanyika. Kila mdau amefanya kazi yake na Bodi ya Ligi tumesimamia kwa umakini kusimamia kanuni. Tumefanya hivyo kusimamia ratiba, pia tumefanya kazi hiyo. Lakini pia wadhamini wamefanya kazi kubwa," anasema mtendaji huyo wa TPLB.

"Wadhamini ndio kiunganishi muhimu kwenye rasilimali fedha, nawashukuru wadhamini wote wametimiza yale tuliyokubaliana kwa wakati bila kukwamisha vitu sambamba na Serikali ambao ndio wadau wetu namba moja.
"Pia ushindani wa ndani kwa timu na timu wameweza kuwa sehemu ya ubora wa ligi, lakini Simba na Yanga zimekuwa chachu nje ya Ligi Kuu Bara, uwakilishi wao kwenye mashindano ya kimataifa.
"Kigezo kikubwa ni mafanikio ya uwakilishi wa klabu zetu kwenye mashindano ya kimataifa ambayo yana pointi nyingi kuliko vigezo vingine vyote. Msimu uliopita mashindano ya Ligi Kuu Tanzania pekee ndio ilitoa timu mbili kushiriki hatua ya robo fainali nchi nyingine kama Morocco, Misri, Tunisia, Afrika Kusini hazikutoa."
Kasongo anasema klabu zinawaheshimisha kufanya kazi nzuri akizishukuru kwa kuwa wamekuwa wakisikilizana kwa pamoja kanuni na ratiba wanazitekeleza na kwamba wanaamini wakiendelea hivyo siku moja Ligi Kuu Bara itakuwa namba moja.
KIPA MMOJA WA KIGENI
Ukiondoa kanuni iliyopo ya kila timu kusajili nyota wa kigeni wanne hivi karibuni pendekezo lingine limeibuka kwa kuzitaka timu hizo kwenye eneo la kipa zinasajili mchezaji mmoja tu, kama anavyodai Kasongo.
"Kauli ya rais Wallace Karia (wa TFF) kwetu tunatakiwa kuifanyia utekelezaji tu kwa sababu ndiye kiongozi wetu. Yote tunayoyafanya tunatekeleza mipango yake kama ilivyomnukuu akizungumza na chombo cha habari kuhusiana na kuzitaka klabu kusajili kipa mmoja, basi sisi tutahakikisha tunalifanyia kazi hilo," anasema na kuongeza:
"Alichozungumza ni maelekezo, sisi watendaji majukumu yetu ni kuhakikisha tunatekeleza katika misingi ya kanuni na utaratibu, ni namna gani tunaliweka katika hizo sura ili liweze kutekelezeka na klabu."

Anasema suala hilo lina manufaa makubwa kwa makipa ambao wapo kwenye timu kwa sasa kipa aliyecheza mechi nyingi za taifa hadi sasa ni Aishi Manula na hana nafasi kikosi cha kwanza cha Simba.
"Kuna Beno Kakolanya, Metacha Mnata, Ally Salim, Yona Amos, Abuutwalib Mshery ukiondoa hao wote ni Amos tu wa Pamba ndio hana changamoto ya kipa wa kigeni, lakini wengine wote wana changamoto, hivyo naamini kauli ya Karia kuna kitu kimelengwa," anasema.
"Sisi tumepokea kauli ya kiongozi wetu mkuu ambaye maono yake ndio yametufikisha hapa tulipo sasa. Kwa hiyo kama watendaji hatuna namna isipokuwa kuchakata ili iweze kutekelezeka na wadau wengine."
Kasongo anasema ni muumini wa ushindani na anaamini ndio unaomkuza mtu ili kufanya vizuri kwani ukiondoa ushindani unamlegeza mtu lakini kupunguza idadi sio kupunguza ushindani, ila kutoa nafasi moja akifikiri bado makipa watatoa changamoto.
"Katika kila timu ambayo itasajili makipa wachache, basi itasajili watatu kati ya hao watatu... wawili wa ndani wanatakiwa kupambana na kipa wa kigeni ili kupata nafasi ya kucheza na kujitengenezea nafasi ya kuaminiwa kwa kupewa nafasi ya kucheza."
KIPIMO USAJILI MIAKA MITANO
Kanuni ya ligi inaruhusu timu shiriki kusajili wachezaji 12 wa kimataifa ambao kati yao sita ndio wanatakiwa kuanza kikosi cha kwanza, lakini sasa kuna mpango wa kulazimisha kusajili kipa mmoja wa kigeni kama anavyothibitisha Kasongo.
"Msimu ujao kutakuwa na kanuni mpya ya kuichakata kwa kuangalia usajili wa wachezaji wa kigeni kusajiliwa kwa kigezo cha kucheza ndani ya miaka mitano ya karibuni kwenye vikosi vya timu zao za taifa tofauti na ilivyo sasa," anasema.
"Mchezaji anasajiliwa kwenye timu kwa kigezo kwamba alishawahi kuitwa timu ya taifa miaka mitano nyuma au timu za taifa za vijana miaka ya nyuma, hivyo tutawasilisha kanuni mpya na kuwapa wawakilishi wa klabu ili waijadili."
Kasongo anasema klabu zilete wachezaji wa kigeni ambao zimejiridhisha pasipo na shaka ili kuwapa changamoto wachezaji wazawa na kuisaidia timu kupata matokeo mazuri na ni vyema zinaposajili wenye hivyo vigezo.
"Mchezaji kucheza timu ya taifa ni sehemu ya kigezo kati ya vigezo vingine na kinatazamwa na kinazingatiwa katika ufanyaji wa usajili, lakini pia kwa nchi zilizoendelea kimeanza kupotea kutokana na ukuaji wa soka," anasema.
"Wachezaji ambao wapo kwenye timu zetu hasa Simba na Yanga wamekuwa wakikidhi vigezo kutokana na wengi kuitwa na wapo kikosi cha kwanza timu ya taifa, na kama kuna klabu ambayo haizingatii hicho kigezo basi inajiangusha yenyewe.
"Ligi yetu inafuatiliwa sana kwa sababu ya wachezaji kutoka mataifa mbalimbali kufuatiliwa baada ya kuja kucheza ligi namba nne kwa ubora Afrika."
LIGI KUU MAREFA 74
Akizungumzia suala la marefa katika ligi, mtendaji huyo anasema: "Siwezi kusema tuna waamuzi wangapi, lakini kanuni inasema waamuzi wanapaswa kuwa 32 wasaidizi 42 ukijumlisha inakuwa 74. Hawa ndio waamuzi kwa mujibu wa kanuni, wanatakiwa kusimamia Ligi Kuu sawa na Championship na First League.
"Lakini siwezi kusema ni waamuzi wangapi wa kati na wasaidizi waliochezesha mechi hadi sasa ikiwa ni mzunguko wa 18 kwa sababu sio sehemu yangu ya kuzungumzia, labda uitafute Kamati ya wWaamuzi wao ndio wanafahamu ni wangapi wamechezesha mechi," anasema Kasongo.

Anasema anachozungumza ni kwa mujibu wa kanuni hao ndio wanaotakiwa kusimamia michezo na kuhusu changamoto katika uamuzi kujirudia mara kwa mara wamekuwa wakizisikia kutoka kwa wadau wa mpira ambao hawapendezwi na wao wanazifanyia kazi.
"Masikio yetu yanasikia na macho yetu yanaona. Ni mijadala yenye tija kwenye mpira, nimekuwa muumini wa kufanyia kazi mijadala yenye tija na nimependa mijadala na kuipokea na kuifanyia kazi.
"Lakini eneo la uamuzi duniani kote limekuwa likizungumzwa kwenye ligi zote sio Tanzania tu. Ni changamoto kubwa kwenye mpira wa ushindani, mfano mzuri La Liga - Real Madrid walicheza na Espanyol walifungwa bao 1-0 baada ya mechi walilalamikia uamuzi wa waamuzi kwenye mechi zao na kuiandikia barua LaLiga, nakala walipeleka Baraza la Michezo Hispania kwa maana chombo cha Serikali.
"Walijaribu kuonyesha sababu mbalimbali waamuzi hawapo upande wao, hii yote ni kujaribu kuonyesha kwamba changamoto ya waamuzi sio Tanzania tu, bali ni duniani kote."
CHAMPIONSHIP KUTORUKA LIVE
Kasongo pia ametia neno kuhusiana na urushaji 'live' wa mechi za Ligi ya Championship akidai mwenye haki ya matangazo ana changamoto zilizomfanya ashindwe kuonyesha.
"Lakini bado tunaendelea kulizungumza ndani, hatujafikia kukata tamaa tunaamini hizo changamoto wanaweza kuzitatua na wakarudi kuendelea kimkataba," anasema.
Anasema taasisi yenye haki ya kuonyesha hiyo michezo mubashara imekubwa na changamoto za kiuendeshaji na kufikia hatua ya kushindwa kuendelea kuonyesha mechi.