Huu ndio utajiri unaomuweka matatani Abramovic

LONDON, ENGLAND. WIKI iliyopita mmiliki wa Chelsea Bilionea kutoka Urusi, Roman Abramovic alitangaza kujiondoa kwenye timu hiyo kama kiongozi na badala yake amewaachia kazi hiyo taasisi ya Chelsea’s Charitable Foundation ikiwa ni baada ya kuhusishwa na kuunga mkono kitendo cha rais wa Urusi, Vladimir Putin kuishambulia Ukraine.
Washirika wa Ukraine wanamhisi Abramovic kuwa anatoa misaada wa kipesa kwa Putin ili azidishe mashambulizi kwa Ukraine.
Pengine unaweza ukajiuliza kwa nini jamaa anaingia kwenye shutuma za aina hii? Je ana utajiri wa kiasi gani? Songa nasi hapa.
CHANZO CHA PESA ZAKE
Jamaa kwanza ni mwanasiasa lakini mbali ya siasa ambayo imechangia kufikia utajiri huo, chanzo chake kikuu cha mapato kuwa mmiliki wa viwanda kadhaa vya mafuta nchini Urusi. Anamiliki hisa nyingi kwenye Kampuni ya Gazprom Neft ambayo ni maarufu Duniani kwenye uuzaji wa mafuta.
Kwa sasa bilionea huyu mbali yakuwa na hisa kwenye kampuni hiyo amewekeza pia kwenye makampuni kadhaa ya masuala ya teknelojia na chuma. Jumla ya utajiri wake ni Bilioni 13.4 bilioni.
MICHORO
Jamaa anamiliki michoro ya thamani na amekuwa mdau mkubwa wa kudhamini matamasha mbali mbali ya kuonyesha michoro hiyo hadharani.
Mwaka 2018 alinunua mchoro wa Francis Bacon kwa Dola 86 milioni. Pia anamiliki mchoro wa msanii Lucian Freud wenye thamani ya Dola 33.6 milioni.

BOTI
Huku nako hashikiki, anatajwa kuwa tajiri anayetumia kiasi kikubwa cha pesa kwenye kununua maboti ya kifahari ambapo kwa sasa anamiliki boti aina ya Eclipse, ambayo ilitengenezwa jinsi anavyotaka yeye na ilimgharimu Dola 400 milioni.
Sasa ndani ya boti hiyo kuna mabwawa mawili ya kuogelea na viwanja viwili kwa ajili ya kushuka helkopta.
Hapo zamani alikuwa akimiliki boti nyingine aina ya Pelorus, ambayo ilimbidi kumpa mkewe baada ya kuachana na unaambiwa ilikuwa na thamani Dola 300 milioni.
NDEGE
Roman anamiliki ndege yenye thamani kubwa aina ya Boeing 767-33A/ER ambayo thamani yake ni Dola 170 milioni. Ndani ya ndege hiyo kuna chumba cha kulia chakula, bafu kwa ajili ya kuogea na sehemu nzuri ya kupumzikia.
MAGARI
Jumla ya magari yake yote yanakadiriwa kuwa na thamani ya Dola 11 milioni, moja kati magari yake yenye thamani zaidi ni 190-mph Ferrari FFX ambazo Dunia nzima zipo 29 tu, pia anamiliki ndinga nyingine aina ya Pagani Zonda Roadster ambazo zipo 15 tu Duniani kote, pia anamiliki gari nyingine ambazo ni Bugatti Veyron, Mercedes AMG GT3 na Aston Martin Vulcan.

NYUMBA
Ukijumlisha nyumba na hoteli zake jumla anamiliki nyumba zenye thamani ya Dola 340 milioni. Ana mjumba hotel huko Manhattan.
Hoteli nyingine ipo kule nchini Ufaransa maeneo ya Cote d’Azur ambayo thamani yake ni Pauni 17 milioni. Nyingine anayo kule London yenye thamani ya Pauni 125-million, pia hapo hapo London ana mjengo mwingine wenye thamani ya Pauni 30 milioni.
Hajaishia hapo mwaka 2020 aliripotiwa kujenga hoteli yenye thamani ya Dola 65 milioni ambayo ndio imevunja rekodi yakuwa hoteli yenye thamani zaidi nchini humo.
Bilionea huyu pia anamiliki hoteli nyingine kadhaa huko nchini Israel na Urusi.
MSAADA KWA JAMII
Kati ya mwaka 2009 hadi 2013 alichangia jumla ya Dola 2.5 bilioni kwa ajili ya kujenga hospitali na shule huko Chukotka nchini Urusi ambapo yeye alikuwa anahudumu kama gavana.
Mbali ya msaada huo jamaa amekuwa akisaidia vituo mbali mbali vya watoto yatima na amekuwa akisaidia nchi mbali mbali yanapotokea maafa ikiwa pamoja na vita.
MAISHA NA BATA
Starehe yake kubwa ni Chelsea na ndio maana huwa anatoa pesa nyingi kuhakikisha timu hiyo inapata matokeo ili furaha yake iendelee kudumu. Amewekeza Chelsea kwa sababu anahitaji furaha na sio pesa.