SIMULIZI YA HADITHI: Jana dume -2
Muktasari:
- Enjo alipompata mwanamme huyo alihisi kuwa alikuwa ameukata. Si muda mrefu akagundua ameingia choo sicho. Juhudi za kumkimbia zikagonga mwamba, kwani jamaa hakuwa mwanaume bali Janadume…!
ILIPOISHIA...
Frank akaagiza ugali kwa kuku. Menyu ilipofika kwangu nikachagua pilau ya kuku na bilauli ya juisi.
“Natoka kazini.” Frank akaniambia mara tu mhudumu alipoondoka. Akaongeza.
“Nimeona muda huu wa kuja kula ndio niutumie kwa mazungumzo na wewe. Nimerudi likizo nimekuta kazi nyingi zilikuwa zinanisubiri. Hapa nikitoka kazini ni jioni kabisa.”
…! SASA ENDELEA...
“Si kuna wenzako wengine?”
“Wapo lakini mafaili yote ni lazima niyakague mimi na kuyasaini.”
“Kwa hiyo likizo si mapumziko ni kurundika kazi. Ukimaliza likizo unajua unakwenda kupambana…”
“Mdogo wangu sijui nikwambie nini…..?”
Mhudumu akatuletea vyakula tulivyoagiza na kutuwekea bili. Baada ya kunawishwa mikonomwenzangu alisali kasha akaanza kula. Na mimi nilisali na kuanza kula.
“Sasa unajua Enjo ule mpango uko tayari. Nilichotaka kukufahamisha ni kwamba andika barua ya maombi ya kazi iambatane na vyeti vyako kasha uielete wizarani.”
“Kwa lini?”
“Kuanzia kesho ila usiicheleweshe sana.”
“Sawa. Baada ya kuileta hiyo barua?”
“Utapata majibu. Utaitwa.”
“Sawa. Nitaiandika.”
“Na utaileta lini?”
“Kesho kabla ya saa sita nitakuwa nimeshaileta.”
“Na mimi nitaipata kesho hiyo hiyo.”
Baada ya kumaliza kula Frank alinileta kwa gari hadi nyumbani kwetu. Wakati tunaagana alitoa shilingi laki moja na kunipa.
“Zitakusaidia mambo mdogo madogo.”
“Asante kaka, nakushukuru.”
Nikashuka kwenye gari na gari hilo likaondoka.
Nilipoingia ndani tu nikakutana na dada sebuleni.
“Oh umesharudi?” Akaniuliza.
“Amenirudisha Frank hapo nje.”
“Amekuitia nini?”
“Ameniita kunifahamisha kuwa ameshafanikisha ule mpango wa kazi. Sasa alichonitaka ni kuandika barua ya maombi ya kazi niiwasilishe kesho wizarani.”
“Sasa usilaze damu, iandike kabisa. Kesho asubuhi uende nayo.”
Naam Sikulaza damu saa nne ya siku iliyofuata nikaiwasilisha barua hiyo wizarani.
Mara tu baada ya kutoka katika jengo la wizara hiyo nikampigia simu Frank. Alipopokea simu yangu nikamsalimia.
“Habari ya asubuhi?”
“Nzuri Enjo. Umeamkaje?”
“Nashukuru niko poa. Nimeleta ile barua.”
“Umefika hapa wazarani?”
“Nimefika na nimekwishatoka.”
“Vizuri. Umeharakisha. Nitaiona. Sasa uko wapi?”
“Ndio naenda zangu.”
“Sawa. Utapata majibu wiki hii hii.”
“Nitashukuru.”
Baada ya kuzungumza na Frank nikarudi nyumbani. Nikamueleza dada kuwa barua nimeshaipeleka.
“Umekutana na Frank?” Dada akaniuliza.
“Sikukutana naye lakini niliwasiliana naye kwenye simu.”
“Amekwambiaje?”
“Ameniambia nitapata majibu wiki hii hii.”
“Mungu atakujalia mdogo wangu utafanikiwa.”
Wiki haikumalizika nikapokea barua ya wito kutoka wizarani iliyonitaka nifike wizarani hapo siku na saa waliyonitajia kwa ajili ya usaili. Siku ile nilipata furaha ya ajabu.
Siku ile niliyoitwa saa tatu asubuhi nikawa wizarani hapo. Nilikutana na afisa niliyelekezwa akanifanyia usaili. Baada ya usaili huo akaniambia nifike siku inayofuata nianze kazi.
Hakuna siku ambayo nyumbani nilikuwa na furaha kama siku hiyo. Siku iliyofuata nikaenda kuanza kazi. Katika chumba cha ofisi niliyokuwemo tulikuwa wasichana wawili. Mimi na msichana mmoja aliyekuwa anaitwa Flora.
Flora alikuwa ndiye rafiki yangu wa kwanza miongoni mmwa wafanyakazi tuliokuwa tunafahamiana. Alinipa ushirikiano mzuri kwenye kazi na akajakuwa rafiki yangu mkubwa.
Baadaye niligundua kuwa alikuwa akiishi Sinza kwenye nyumba ya kupangisha. Nyumba aliyokuwa amepangisha ilikuwa na pande mbili. Upande mmoja alipangisha yeye na upande mwingine alipangisha mwenzake lakini walikuwa wakitumia mlango mmoja.
Jumapili moja akanialika nyumbani kwake. Nilifika nyumbani kwake majira ya saa tano. Kabla ya kushuka kwenye teksi nilimpigia simu.
“Enjo umeshafika?” Akaniuliza mara tu alipopokea simu. Aliniuliza hivyo kwa sababu nilipoondoka nyumbani nilimpigia kumjulisha kwamba ninaondoka.
“Nimeshafika, niko barazani kwako hapa.”
“Okey..nisubiri ninatoka….”
Nikakata simu na kumsubiri.
Baada ya sekunde kadhaa akafungua geti na kunikaribisha ndani. Nilifungua mlango wa teksi nikashuka na kumfuata.
“Karibu Enjo…hapa ndio kwangu.”
“Asante., nimepaona nyumbani kwako.”
Flora akanikaribisha sebuleni kwake. Sebule yake alikuwa ameipamba vizuri mpaka nikaionea wivu.
“Nikupatie kinywaji gani shoga, kinywaji cha moto au baridi?” Flora akaniuliza nikiwa nimeketi.
“Kinywaji cha moto hapana. Nipatie kinywaji cha baridi kama kipo.”
“Sawa.”
Flora akaenda kuniletea jagi la juisi na glasi akaniongezea na sahani iliyokuwa na keki tatu.
“Karibu.”
“Asante shoga.”
Flora akanimiminia juisi kwenye bilauli kasha naye akakaa. Tukaanza kupiga stori. Tulizungumzia mabo ya kazini na mambo ya maisha. Tulizungumza kwa kirefu sana mpaka ikafika saa saba. Flora akaenda kupakua pilau na kuiweka juu ya meza kasha akanikaribisha.
Nikainuka nilipokuwa nimeketi nikaenda kwenye meza tukakaana kuanza kula pilau.
Niliondoka kwa Flora majira ya saa nane. Niliondoka na wazo moja tu kwamba na mimi nitafute nyumba ya kupangisha kama flora nitengeze maisha yangu mwenyewe kwa vile kazi nilikuwa nimeshapata.
Jumatatu tulipokutana kazini nilimwambia Flora kwamba natafuta nyumba ya kupangisha.
“Umefanya vizuri kuniambia mapema. Ile nyumba ninayoishi mimi umeipenda?”
“Nimeipenda sana.”
“Yule mpanhaji mwenzangu anahama mwezi huu. Sasa kama unapataka nimwambie mwenyewe asilete mpangaji mwingine.”
“Malipa kodi kiasi gani?”
“Kila upande tunalipa milioni mbili na laki nne kwa mwaka.”
“Anataka kodi ya mwaka si ya miezi sita.”
“Labda nizungumze naye.”
“Subiri kwanza nifanye huo mpango wa kupata hizo pesa halafu nitakwambia.”
Baada ya mazungumzo hayo na Flora zikapita wiki mbili. Sikuwa nimemueleza kitu kwa sababu bado nilikuwa nafanya mpango huo wa kupata angalau fedha ya pango ya miei sita shilingi laki sita.Mshahara wangu wa mwezi ulikuwa hautoshi kulipia pesa hizo za kodi na kupata nyingine za matumizi yangu.
Baada ya wiki mbili hizo siku moja tukiwa ofisini Flora aliniuliza.
“Vipi ule mpango tuliozungumza, naona upo kimya.”
Nikajua mpango huo ni ule wa pango.
“Mwenzako ndio niko kwenye mipango. Sijafanikisha bado.”
“Mwenzangu una bahati sana.”
“Bahati gani shoga?”
“Frank ameshanipa shilingi milioni moja na laki mbili za pango.”
Nikagutuka na kumkazia macho Flora.
“Mliongea nini?” Nikamuuliza kwa mshituko.
Flora akacheka. Mimi sikuwa na kicheko lakini nilitoa kicheko cha uongo ili asione nimefadhaika sana.
“Katika mazungumzo yetu asubuhi nikawa mbeya kidogo nikamtamkia kwamba unataka uhamie pale kwangu lakini umesita kwa sababu ya kodi. Akaniuliza kwani kodi ni bei gani? Nikamwambia kodi ni shilingi milioni moja na laki mbili. Akatoa hizo pesa na kunipa akaniambia nikakulipie.”
“Umenishitua kidogo lakini nashukuru sana.”
Flora akafungua mkoba wake na kunitolea hizo pesa.
“Hizi hapa shilingi milioni moja na laki mbili.”
“Unataka unipe?”
“Ameniambia nikakulipie kwa vile mimi ndiye ninayemjua mwenye nyumba.”
“Kanilipie dada. Hizo pesa ndizo zilizokuwa zinazungusha akili yangu.”
Flora akazirudisha pesa hizo kwenye mkoba.
“kumbe wewe mwenyewe hajakwambia?”
Nikabetua mabega yangu.
“Hajaniambia.”
“Lakini atakwambia tu.”
“Namshukuru sana huyu kaka.”
“Frank ni mtu mzuri sana.”
“Ni mtu mwenye moyo wa ubinaadamu sana.”
Nikaanza kumueleza nilivyomfahamu Frank kabla sijaajiriwa hapo wizarani.
“Alikuwa rafiki yake baba yangu na hata mipango ya kupata kazi hapa alichangia sana.”
“Amekuchukulia kama mdogo wake.”
“Bado nasema namshukuru sana.”
Wakati Flora akiendelea na kazi yake nilitoa simu yangu nikamtumia Frank meseji iliyosema.
“Asante sana.”
Baada ya muda kidogo akaniuliza.
“Mmezungumza na Flora?”
Nikamwandikia tena.
“Ndiyo tumezungumza. Amenipatia. Nakushukuru sana.” Nilipoituma akarudisha jibu.
“Nitakupigia baadaye tuzungumze. Hivi sasa nimetoka kidogo.”
Nikamtumia meseji nyingine.
“Sawa.”
Jioni tulipokuwa tunataka kutoka kazini Flora akampigia mwenye nyumba wake.
“Ningekuomba uje nyumbani jioni hii kama utaweza.”
”Una ishu muhimu?”
“Ni kuhusu nyumba. Kuna dada yangu anataka kupangisha ule upande wa pili.”
“Anayo kodi ya mwaka mzima.”
“Ndiyo anayo.”
“Kwa hiyo nije na mkataba wa pango?”
“Ikiwezekana njoo nao.”
“Sawa. Nitakuja saa kumi na mbili jioni. Si utakuwa umesharudi kutoka kazini?”
“Kazini ndio tunataka kutoka sasa hivi.”