Dili iliyokufa - 42
ILIPOISHIA
“Sasa ulikuwa unafanya nini hapo kwake?”
“Mume wangu unaniuliza swalli gumu. Sijui nikujibu nini?”
“Swali gumu kivipi. Si unaniambia tu ulichokuwa unafanya”
“Wakati mwezanko nilikuwa sijijui”
“Kwa hiyo alikuwa akikuchezea tu!”
“Sijui. Leo ndio nimerudiwa na akili”
“Huyo mganga lazima akamatwe tu kwa sababu ni mshenzi. Una maana ndio unatoka huko Mwahako?”
SASA ENDELEA...
“Ndiyo, nimeshuka kwenye daladala sasa hivi.”
“Sasa umetoroka au umeaga?”
“Nimeaga kuwa ninakwenda mjini mara moja. Wao wanajua kuwa nitarudi.”
“Sawa. Sasa pumzika kidogo halafu twende kituo cha polisi tukatoe taarifa, kwani taarifa zako ziko kule.”
“Ulikwenda kunishitaki?”
“Hapana. Nilikwenda kutoa ripoti kuwa mke wangu ametoroka na sijui yuko wapi.”
“Nilivyokutana na Mudi pia aliniambia kuwa ulikwenda polisi.”
“Kwa kweli nilihangaika sana kukutafuta. Unaponieleza kuwa kuna mganga alikuzuia nyumbani kwake, nitakufa naye. Kama ni mchawi kweli, aniue, lakini sitamuacha.”
“Kwa sababu nimejifanya ninaenda madukani, hata nguo zangu sikuzichukua.”
“Na hizo nguo ulikwenda nazo lini?”
“Siku ile nilipofikiria nikaishi kwake ndipo nikachukua nguo kabisa.”
“Kweli alikuharibu akili.”
“Nakwambia nilikuwa sijielewi. Alikuwa akinitumisha kazi kama mtumwa.”
“Nakuona umekuwa mweusi kama kijungu!”
Hapo nilitoa tabasamu la huzuni kwa kuamini kuwa nilikuwa natisha kama alivyonieleza mume wangu Mashaka.
“Nimekuwa mweusi kama kijungu?” nikamuuliza ili nione kama atabadilisha usemi wake.
“Chukua kioo ujitazame.”
Kwa vile nilikuwa nimepatwa na udadisi, nikainuka kweli na kuingia chumbani. Nikasimama kando ya kioo cha kabati na kujitazama.
Nikauona uso wangu haukuwa kama ule wa mwanzo. Ulikuwa umechakaa na kuonekana kama wa mzee.
Mume wangu akafungua mlango na kuingia mle chumbani.
Macho yake yalionesha kunionea huruma baada ya kumweleza ukweli wangu.
“Unajiona jinsi ulivyoharibika?” akaniuliza.
“Ni kweli. Nimekuwa kama kinyago, sijui…”
Mashaka akakaa kwenye kitanda.
“Kwani ulikuwa unafanya kazi gani?”
“Kule tulikuwa watatu. Alikuwa na wake zake wawili. Kazi yetu ilikuwa kupika, kuchota maji na kufanya kazi nyingine za nyumbani.”
“Hayo maji mnayachota wapi?”
“Ni mwendo mrefu kutoka hapo nyumbani tunapokaa. Ndoo sita asubuhi, ndoo sita jioni.”
“Huyo mganga anastahili adhabu kali sana.”
Aliposema hivyo Mashaka alitoa simu yake, akatafuta namba aliyokuwa ameiweka kisha akaipiga.
Baadaye nilimsikia akisema:
“Vipi Mudi...?”
Akasikiliza kidogo kisha akasema:
“Shemeji yako amerudi.”
Sikuweza kusikia Mudi alimwambia nini, ila nilimsikia Mashaka akisema:
“Amesema ni kweli alikuwa kwa huyo mganga... juzi wifi yake alikwenda kwa mganga huyo huyo kumfanyia dawa za kumrudisha. Hizo dawa nafikiri ndizo zimesaidia... ameniambia alimuona alipokwenda lakini alijificha ili asikutane naye... sasa leo asubuhi ndipo akili zikamrudia akatoroka... anasema huyo mganga hakujua kama mtu anayemfanyia dawa ni yeye, vinginevyo asingefanya...”
Akanyamaza kwa muda akisikiliza maelezo ya simu ya upande wa pili kisha akasema:
“Ndiyo, tunajiandaa twende polisi kutoa ripoti ili akakamatwe... sawa... basi wewe njoo hapa jioni utamkuta.”
Mume wangu akakata simu na kupiga tena. Safari hii alimpigia mdogo wake.
“Habari ya huko?”
Akasikiliza kisha akasema:
“Marahaba. Wifi yako amesharudi.”
Akasikiliza tena na kusema:
“Amerudi sasa hivi. Kumbe alikuwa kwa mganga yule yule ulikokwenda wewe... amesema ulipokwenda alikuona akajificha... ndiyo yupo hapa.”
Mume wangu akanipa ile simu. Bila shaka aliambiwa na mdogo wake anipe simu ili aongee na mimi.
Nilipoishika simu niliisogeza sikioni na kusema:
“Hello, wifi...!”
“Sharifa, ndiye wewe?”
“Ndiyo mimi. Nimerudi kwa mume wangu.”
“Ulikuwa wapi?”
“Nilikuwa kwa yule mganga. Juzi ulipokuja nilikuona.”
“Kule Mwahako?”
“Ndiko huko huko.”
“Kumbe uliniona nilipokwenda? Wewe ulikuwa wapi?”
“Nilikuwa pale pale nyumbani, lakini nilipokuona nilijificha. Wewe hukuniona.”
“Una maana yule mganga ndiye aliyekuzuia?”
“Ndiyo, huyo huyo. Nilikwenda kwa shida zangu za uzazi, kumbe mwenzangu alikuwa na lake. Kaniroga nikabaki kule kule. Sasa ile dawa aliyokufanyia ndiyo ikanizindua.”
“Sasa yeye hakujua kama ni wewe anayekufanyia dawa?”
“Naona hakujua.”
“Mh! Mganga gani anateka wake za watu! Tutakuwa tunawaogopa waganga wa siku hizi...”
“Mimi ndiyo nimekoma. Sitakwenda tena kwa waganga.”
“Hivi mume wako alikuwa anajua kama ulikwenda kwa mganga?”
“Hajui. Nilimficha. Nilikuwa ninakwenda mwenyewe. Mara nyingi ukimwambia habari ya kwenda kwa waganga anakataa, anataka twende kwa madaktari. Ndiyo maana sikumwambia.”
“Sasa kaka amesemaje baada ya wewe kurudi?”
“Amesema twende polisi tukatoe ripoti ili yule mganga akakamatwe.”
“Na wewe umekubali?”
“Nisikubali kwa nini wakati alikuwa ameharibu akili yangu?”
“Ina maana kama mimi nisingekwenda kwa mganga yule ungekuwa kule kule hadi leo?”
“Ndiyo hivyo. Ningebaki. Mngenitafuta mpaka mchoke.”
“Makubwa! Basi mtakavyoambiwa huko polisi mtanifahamisha.”
“Tutakufahamisha.”
Nikamrudishia simu kaka. Akaagana na mdogo wake kisha akakata simu.
Mimi nilikwenda kuoga ili kuusafisha mwili wangu na kuondoa harufu ya mafusho. Baada ya kutoka kuoga nikajipaka losheni mwili mzima, kisha nikavaa nguo nyingine.
Nilipokuwa tayari nikamwambia mume wangu tutoke twende huko polisi. Tukatoka.
Tulikodi bajaji iliyotufikisha kituo kikuu cha polisi. Tuliingia ndani ya kituo hicho, mume wangu akajitambulisha na kuonesha RB aliyokuwa amepewa mwanzo.
Polisi wakaliona faili langu na kumuuliza kama mke wake hajamuona hadi siku hiyo.
“Mke wangu amerudi leo nyumbani na ndiye huyu hapa niliyenaye,” Mashaka akawaambia polisi hao.
“Amekwambia anatoka wapi?” polisi mmoja akamuuliza.
“Ni hadithi ndefu kidogo,” mume wangu akamwambia.
“Ndiyo tunataka uanze wewe kutueleza, halafu na yeye atatueleza.”
Mume wangu akawaeleza kama nilivyomweleza mimi. Polisi hao waliposikia kisa kile walishtuka sana. Wote wakanitolea macho.
“Ni kweli alivyotueleza mume wako?” mmoja wa polisi hao akaniuliza.
“Ni kweli. Nilikuwa nimewekwa kwa huyo mganga aliowaambia,” nikawaambia.
“Na ni kwa nini ulikubali kukaa kwa mganga huyo huku ukijua wewe ni mke wa mtu?”
“Sikukaa kwa akili yangu. Nilikuwa sijielewi. Leo asubuhi ndipo akili ilinirudia nikaondoka.”
“Mganga gani anaroga wateja wake, tena wake za watu, na kuishi nao yeye!” polisi huyo aliuliza huku akimtazama polisi mwenzake, ambaye naye alimjibu:
“Huyo anatakiwa kukamatwa na kushitakiwa.”
“Unajua huku kurogana hakukubaliki katika sheria.”
“Yeye atashitakiwa kwa kuharibu akili, kutorosha mke wa mtu au kumteka na kuishi naye. Hilo ni kosa la jinai.”
Polisi aliyeambiwa maneno hayo akanitazama.
“Umesema huyo mganga yuko sehemu gani?”
“Yuko Mwahako.”
“Mwahako ni sehemu gani?”
“Ni nje kidogo ya jiji. Hicho kijiji kiko katika barabara ya kuelekea Pangani,” mume wangu akamwambia.
“Kama kilometa ngapi?”
“Kama kilometa kumi hivi.”
“Sasa inabidi muandikishe maelezo yenu. Baada ya hapo huyo mganga akamatwe.”
Nilichukuliwa maelezo yangu. Nilieleza mwanzo hadi mwisho. Kisha yakachukuliwa maelezo ya mume wangu. Baada ya hapo polisi wakapanga mkakati wa kwenda kumkamata mganga huyo.
Nilishangaa kwamba polisi walilichangamkia suala hilo la kwenda kumkamata mganga huyo.
Kwa upande wangu nilipata hofu kidogo. Niliona kama mganga huyo akikamatwa ataona nimemgeuka na anaweza kunifanyia madhara. Lakini hata hivyo, kutokana na ushenzi alionifanyia, nilijiambia lolote litakalotokea, mganga huyo lazima akamatwe kwani alinidhalilisha sana.
Wakati polisi wakiendelea na mkakati wa kwenda kumkamata mganga huyo, ulizuka mjadala miongoni mwao. Kuna waliotaka mganga huyo akamatwe moja kwa moja na kuna waliotaka nirudi mimi kama nilivyomuahidi kuwa nitarudi, halafu polisi waje watukamate pamoja.
Waliotoa hoja kwamba mganga huyo akamatwe moja kwa moja walisema kuwa, kwa vile mlalamikaji yupo na maelezo yapo, kinachofuata ni mganga huyo kukamatwa tu na kufikishwa mahakamani.
Wale waliotaka mimi niende kwanza halafu polisi waje watukamate pamoja walitaka kuwe na ushahidi kuwa nilikutwa nyumbani kwa mganga huyo.