Dili iliyokufa - 41
ILIPOISHIA
“Sasa itabidi uwaachie wenzako waendelele, wewe shughulikia huyo kuku. Tutamlia ugali mchana”
“Ni kuku wa uganga?” nikajidai kumuuliza.
“Riziki imekuja sasa hivi. Kuna msichana nilimshughulikia shida yake. Ameshaenda”
“Sawa. Ngoja nimimine haya maji nimshughulikie huyo kuku”
Huyu ni mganga gani ambaye ameshindwa kujua kuwa mtu aliyemfanyia uganga huo ni mke wake? Nikajiuliza moyoni mwangu
SASA ENDELEA...
Kwa vile sikuwa nikiamini kuwa nilikuwa nimerogwa na mganga huyo ili nibaki nyumbani kwake, sikuwa na wasiwasi. Nilichokuwa najua ni kuwa nilibaki kwa mganga huyo kwa mapenzi yangu mwenyewe na pia baada ya kuchoka na shida nilizokuwa nikizipata kutoka kwa mume wangu wa kwanza.
Nikaanza kumshughulikia yule kuku. Nilichemsha maji. Yalipokuwa moto nikamtia yule kuku ili kumnyonyoa manyoya yake. Nilipomaliza nilimpasua na kumtoa matumbo, kisha nikamkatakata vipande vipande na kumchemsha.
Sikwenda tena kuchota maji. Wenzangu waliporudi hawakwenda tena. Walikuwa wamechoka. Kule kukaa tu kwenye foleni pia kulikuwa kunachokesha.
Baada ya kuku huyo kuiva nikabandika sufuria ya ugali. Ugali ulipokuwa tayari nikaupakua. Mume wetu nilimtilia chakula kwenye sahani yake. Yeye alikuwa anakula peke yake na sisi tulikuwa tunakula peke yetu.
Siku ile hatukunywa chai. Tulikula ugali. Baada ya kula tukapumzika kidogo, ndipo kila mmoja wetu akaenda kuoga. Kwa vile maji yalikuwa ya shida, kila mtu alioga kwa kutumia nusu ndoo.
Jioni tukaenda kuchota tena. Tulikuta foleni lakini haikuwa ndefu kama ya asubuhi. Tukajaza pipa kisha tukapumzika. Ugali wa usiku aliusonga mwenzangu. Pale tukiamua kula ugali, tunakula mchana na usiku. Kule kwa mume wangu wa kwanza nisingethubutu kula ugali mara mbili. Kama ningekula ugali mchana, usiku ilikuwa lazima nile wali.
Ilikuwa asubuhi ya siku ya pili ndipo nilipoona akili yangu ikianza kubadilika. Tangu nilipoamka nilikuwa nikijiuliza kwanini nilikuja kuishi kwa yule mganga na kwanini nilitoroka kule kwa mume wangu. Kwa kweli sikupata jibu.
Pia nilijiuliza niliwezaje kuishi maisha yale niliyokuwa nikiishi na nilikubalije kulala na yule mganga, mtu ambaye hakuwa na hadhi yangu.
Nikajishangaa sana na kutojielewa. Pale ndipo nilipoanza kugundua jambo lililokuwa nyuma ya pazia ambalo hapo mwanzo sikuwa nikilijua. Niligundua kwamba ni kweli yule mganga alikuwa ameniroga ili nibaki pale nyumbani kwake na niwe mke wake.
Lakini baada ya wifi yangu kuja pale, mganga huyo akafanya uganga mwingine ambao uliharibu ule uganga wake wa kwanza bila kujua kwamba mtu aliyekuwa akimuagua ndiye aliyemroga yeye mwenyewe. Muda ule nilijiona nina akili timamu.
Na hapo nikaamini ule msemo wa wahenga kuwa **kioo hakijioni**.
Sikutaka tena kuendelea kuishi kwa yule mganga. Akili yangu ilinituma kurudi nyumbani kwa mume wangu. Nikajiuliza nitaondokaje kwa yule mganga bila kuleta mashaka.
Baada ya kufikiri nikaona niage safari ya kwenda mjini kununua shanga za kuvaa kiunoni. Wake wenzangu walikuwa na shanga lakini mimi sikuwa nazo.
Nikaingia chumbani kwa mganga na kumuomba pesa.
“Unataka pesa ya nini?” akaniuliza.
“Nataka nikanunue shanga. Wenzangu wana shanga, mimi sina.”
“Shilingi ngapi?”
“Nipe elfu kumi tu.”
Mganga akanipa shilingi elfu kumi.
“Sasa sikiliza. Pengine utakaporudi hutanikuta,” akaniambia.
“Utakwenda wapi?”
“Nataka kwenda shambani kuchimba dawa zangu. Nitarudi jioni.”
“Sawa. Tutaonana hapo jioni.”
Nikaondoka. Nilikwenda kupanda daladala nikarudi mjini. Kusema kweli nilijiona mpumbavu sana kutekwa na yule mganga na kukaa nyumbani kwake kwa siku kadhaa.
Pengine kama si yule wifi yangu kwenda kwa mganga huyo na kufanyiwa dawa iliyoirudisha akili yangu, ningeendelea kukaa kwa mganga huyo kwa siku nyingi.
Tangu nilipoanza kuishi kwa mganga huyo nilikuwa situmii losheni. Mwili wangu ulikuwa umeharibika na uso wangu ulikuwa mweusi. Niliona aibu hata kwenda mjini lakini ilibidi nirudi nyumbani kwangu na nieleze yaliyonitokea.
Niliposhuka kwenye kituo cha daladala nikakodi bodaboda iliyonipeleka nyumbani kwangu. Ilikuwa bahati, siku ile ilikuwa Jumapili. Mume wangu alikuwa nyumbani.
Nilipoujaribu mlango wa mbele haukuwa umefungwa kwa ndani. Ulikuwa umesindikwa tu. Nikausukuma na kuingia nyumbani kwangu kwa uoga, hasa nilivyojua kuwa mume wangu yupo.
Baada ya kuingia ndani niliubana mlango, nikawa naelekea sebuleni. Ghafla nikaisikia sauti ya mume wangu ikitokea chumbani.
“Nani?”
Kabla hata sijamjibu, mlango wa chumbani ukafunguliwa na mume wangu. Aliponiona akabaki ameshangaa.
Mimi ndiye niliyetabasamu lakini yeye hakutabasamu. Bila shaka alikuwa amepatwa na mshangao kwamba mimi ndiye mke wake nimerudi au macho yake yalikuwa yamemdanganya.
“Nani wewe, Sharifa?” akaniuliza.
“Ndiye mimi,” nikamjibu huku nikiketi kwenye sofa.
Kusema kweli, ingawa nilijichangamsha, nilipatwa na aibu kidogo.
Nilipomwambia “ndiye mimi”, akasogea pale nilipokuwa nimeketi, naye akakaa.
Hatukuwa na salamu. Badala yake aliniuliza.
“Unatoka wapi?”
Hilo ndilo swali ambalo nililitarajia kutoka kwake na nilikuwa na jibu.
“Ni makubwa yalinifikia mwenzako. Hivi ulivyoona nimerudi, mshukuru Mungu.”
Nilipomwambia hivyo, ile taswira ya shutuma iliyokuwa kwenye uso wake iliondoka, ikaja sura ya udadisi.
“Hebu nieleze imekuwaje? Mwenzangu umeondoka ghafla hapa nyumbani bila taarifa yoyote…”
“Ndiyo nataka kukueleza hivyo…”
“Hebu nieleze…”
Nilikuwa nimeshapanga nimweleze ukweli lakini kile kipengele cha kwenda kwa mganga kumfanyia yeye dawa za mapenzi niliona nikiacha.
“Tumbo ndilo lililoniponza,” nikaanza kumwambia.
“Tumbo limekuponza? Mbona sikuelewi?”
“Ndiyo, tumbo ndilo lililoniponza. Sasa kosa langu ni kuwa sikukuambia kwamba nilikuwa ninakwenda kwa mganga wa kienyeji ambaye niliambiwa anaagua matatizo ya tumbo ya kina mama wenye matatizo kama yangu.”
“Tumbo lako lina matatizo gani?”
“Matatizo ya kuchelewa kushika ujauzito. Mganga huyo alinipa dawa za kutumia kwa siku tatu hivi, akaniambia zikiisha niende tena. Nikaenda. Kumbe mwenzangu alikuwa akinifanyia dawa nibaki pale nyumbani kwake. Siku ile nilipokwenda ndipo nikapoteza akili nikabaki pale pale mpaka hii leo.”
“Kama ulikuwa unakwenda kwa mganga kufanyiwa tiba ya tumbo, kwanini usinieleze mimi, mume wako?”
“Kwa kweli nilishindwa kukuambia. Niliona utaona kama naleta habari za kishirikina. Niliamua nifanye siri yangu tu. Kumbe mganga mwenyewe naye akawa na ajenda yake ya siri ya kunibakisha kwake.”
“Huyo mganga yuko wapi?”
“Yuko Mwahako.”
“Ni mwanaume?”
“Ndiyo, ni mwanaume. Ana wake zake wawili hapo hapo nyumbani.”
“Hivi juzi si ulikutana na Mudi ukamwambia uko Chumbageni, sijui kwa rafiki yako?”
“Sasa pale nilikuwa nimekuja mjini. Nilikuja madukani. Wakati ule sikuwa na akili kabisa. Nikamdanganya Mudi kuwa ninaishi Chumbageni lakini haikuwa kweli. Nilikuwa kwa huyo mganga.”
Mume wangu akawaza kidogo kisha akaniambia.
“Naweza kuamini maneno yako kwa sababu kila tulipokwenda kutazamia tuliambiwa umerogwa na mganga na uko kwake.”
“Ni kweli. Sasa kilichonisaidia ni kuwa wifi yangu alikuja kwa yule mganga kunitazamia mimi. Nilipomwona nilijificha. Hakuniona. Akamweleza yule mganga matatizo yaliyompeleka. Mganga akamwambia aje siku iliyofuata amshughulikie.”
“Huyo mganga hakujua kama huyo mtu anayetaka kumshughulikia ni wewe?”
“Naona hakujua. Kama angejua asingemfanyia uganga ule. Angemdanganya tu.”
“Sasa huyo ni mganga kweli?”
“Ni mganga. Sema tu mganga hajigangi. Lakini dawa zake ni za kweli kwani alipofanya huo uganga wake, siku ya pili yake, ambayo ni leo, nikaona akili zimenirudia.”
“Huyo wifi yako alikuja juzi akaniambia amekwenda kwa mganga huko Mwahako. Ameambiwa apeleke kuku na nguo yako. Nikampa pesa pamoja na gauni lako. Jana jioni akaja hapa nyumbani akaniambia mke wako atarudi leo. Na kweli umetokea. Kumbe mganga mwenyewe aliyekuroga ndiye huyo huyo aliyekuponya.”
“Ndiyo hivyo mume wangu.”
“Kwa sababu halikuwa kosa lako nimekusamehe, lakini itabidi twende polisi ili huyo mganga akamatwe.”
“Twende. Mimi mwenyewe sikuridhika na kitu alichonifanyia.”
“Sasa ulikuwa unafanya nini hapo kwake?”
“Mume wangu, unaniuliza swali gumu. Sijui nikujibu nini.”
“Swali gumu kivipi? Si unaniambia tu ulichokuwa unafanya.”
“Wakati ule mwenzako nilikuwa sijijui.”
“Kwa hiyo alikuwa akikuchezea tu!”
“Sijui. Leo ndiyo nimerudiwa na akili.”
“Huyo mganga lazima akamatwe tu kwa sababu ni mshenzi. Una maana ndiyo unatoka huko Mwahako?”