Zuchu: Mama amenistiri kwa mengi

Muktasari:
- Akizungumza na Mwanaspoti, eneo ya Kawe jijini Dar es Salaam juzi kati Zuchu alisema kuna kipindi mama yake pekee ndiye aliyemuona ana thamani wakati watu wengine wakimwona ni mchafu wa maneno na hafai kabisa kwa vitendo.
STAA Bongo Fleva, Zuchu amesema hakuna wa kumthamini na kumheshimu hapa duniani kama mama yake, kwani ndiye aliyempa faraja ya kweli katika maisha magumu aliyopitia.
Akizungumza na Mwanaspoti, eneo ya Kawe jijini Dar es Salaam juzi kati Zuchu alisema kuna kipindi mama yake pekee ndiye aliyemuona ana thamani wakati watu wengine wakimwona ni mchafu wa maneno na hafai kabisa kwa vitendo.
“Iko hivi, kuna watu walinibeza kwa maneno machafu na kuniona sifai kabisa katika dunia hii lakini mama yangu alinikingia kifua na amekuwa zaidi ya faraja kubwa.
“Kila kukicha baadhi ya watu hawanitoi jina langu mdomoni au akilini mwao na hii tangu yawekwe wazi mahusiano yangu na Diamond, nimepewa kila aina ya majina, nafuatiliwa sana maisha yangu hasa ya mahusiano yangu, watu hawana huruma na mimi kabisa, walianza kunisema hadi sasa wanaendelea kunisema, mama yangu hajaniacha kamwe kunisapoti kwa yote yanayotokea, japo wapo baadhi ya mashabiki wanakuwa nami ila mama yangu anakuwa na mimi kutoka moyoni na wakati mwingine hadi anatukanwa sababu yangu,” alisema Zuchu.
“Si umeona kwa sasa ninavyowakaushia tangu wameanza kuongea. Mimi niko kimya hadi wamekuwa hawana jipya la kuongea, wanafanya kurudia maneno yale yale, sasa hii ni dawa ila wasizidishe mipaka wakanivuruga akili yangu, kwa maana hakuna hata mtu mmoja ninayemuogoa bali naheshimu tu wakati mwingine sio kila kitu kuongea,” alisema.