Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

UKWELI MCHUNGU... Harusi ya Jux ilibamba, ila tulikosa utambulisho kitaifa

JUX Pict

Muktasari:

  • Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kusema kuwa ‘Taifa lisilo na utamaduni ni sawa na taifa mfu’. 

KILA taifa makini hujipambanua kwa lugha na mavazi mbali na mambo mengine. Huo ndiyo utamaduni. Mila na desturi tunazosema ndizo mhimili mkubwa au alama kubwa kwa mwanadamu yeyote anayejitambua.

Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kusema kuwa ‘Taifa lisilo na utamaduni ni sawa na taifa mfu’. 

Kauli hiyo inasadifu ukweli, kwani hadi leo Tanzania imeshindwa kuwa na vazi la Taifa.

Hii imeonekana kwenye matukio mengi hasa ya sanaa na ambako ndiko hasa kunakoweza kuonyesha utamaduni wa Mtanzania.

Mfano mzuri ni hivi karibuni ulimwengu ulishuhudia ndoa iliyotikisa kutoka kwa msanii wa kizazi kipya cha Bongo Fleva, Juma Mussa Mkambala a.k.a Jux na Priscilla Ajoke Ojo (Hadiza) sherehe zilianzia Jiji la Dar es Salaam na kumalizika Nigeria na sherehe hiyo kufana.

Hapo ndipo unapoona tofauti ya nguvu ya utamaduni kati ya Tanzania na Nigeria.

JU 001

Hakuna ubishi katika sherehe ya Nigeria, hakuna ambaye angehisi kuna Watanzania bali wote waliokuwepo ni Wanigeria.

Kwa nini? Ni kwa sababu ndugu zetu waliokwenda huko, waoaji na wasindikizaji waliingia kwenye mfumo wa Wanaigeria kwa kuvaa mavazi kama yao. Ni bora hata wangevaa vazi la kikoloni, suti.

Hii ingethibithisha tu hatuna vazi la Taifa na tumekwama kubuni. Ni fedheha, kwani kilichoonekana ni kuwa na vazi tofauti na sio la kipekee litakalomtambulisha mtu anatokea wapi.

Mfano mzuri, ni mataifa madogo kama Rwanda. Wana mavazi yao, ukiwaona tu katika shughuli zao unajua ni Wanyarwanda.

Pamoja na ucheleweshaji kwa wabunifu wetu kukwama, tulitarajia watu pekee ambao wangetubeba na kuanzisha vazi ambalo lingezoeleka ni wasanii, matokeo yake amebaki msanii mmoja tu Mrisho Mpoto pekee.

JU 03 (1)

Msanii huyu amekuwa mbunifu wa mavazi ya kiasili na kuwa na mwonekano wa kipekee.

Kwa bahati mbaya sana pamoja na kuwa na wasanii wenye ushawishi na kukubalika na mashabiki lakini wameshindwa kutangaza na kuporomoti aina ya mavazi ambayo pengine yangekuwa ni mavazi ya Kitanzania, kwani wanavyovaa mavazi ya kimagharibi mashabiki zao huwaiga.

Wasanii na wasindikizaji kama Mc maarufu Gara B walikuwepo katika msafara huo, unajua kwa nini nimemtaja huyu? Ni mmoja wa watu wanaofuatiliwa na  awali niliwahi kuongea na kiongozi mmoja wa taasisi moja inayoshugulika na sanaa na kunieleza, moja kundi linalofifisha juhudi za ukuaji wa sanaa ni washereheshaji, ambao katika sherehe nyingi huendesha kwa nyimbo za kigeni.

JU 03

Ninapoongelea suala la kiutamaduni ni kama alama na njia kuu katika kutengeneza ajira na masilahi kwa taifa lolote linaloshiriki na kujitambulisha kwa lugha yake, mavazi yake, mila na desturi kwa watu wake na si utamaduni wa kuazima kutoka kwa wengine.

Awali niliitaja Rwanda ambao walijipatia Uhuru wake nyuma yetu mwaka 1962.

Wao wamejitanabaisha kwa kuwa na vazi la kwao iwe katika sherehe za kitaifa, harusi na nyingine.

Hapa kwetu, wale ambao jamii inawaangalia kama sehemu ya mabadiliko baada ya taasisi yenye dhamana kukwama, ambao ni wasanii, amebaki Mrisho Mpoto pekee na vazi lake la ubunifu.

Sio kama tunawasakama wasanii, hapana, ila tunaamini kwa nguvu mliyonayo, mkiitambua ni rahisi kupata vazi la Taifa, kwani waliochaguliwa kufanya hivyo, walishindwa na sasa tunadhalilika.

JU 04

Tunawakumbusha wasanii, kazi yenu siyo kuburudisha tu, pia kuimarisha na kujenga utamaduni kwa kujitangaza kimataifa ikiwamo matumizi ya lugha ya Kiswahili.

Inawezekana kupata vazi la taifa ni ngumu kwani kumekuwapo na ukinzani katika kukubaliana jambo hilo.

Mkurugenzi wa zamani wa Utamaduni,  Profesa Herman Mwansoko, aliwahi kusema anapata wasiwasi kama katika  makabila makubwa zaidi ya 120 Taifa limeshindwa kupata vazi la kiasili.

Aliona utekelezaji ni mgumu kwa sababu kuna makabila mengi na kila kabila lina utamaduni na mila zake, hivyo kusiwe na shinikizo na kila jamii iwe huru kuvaa mvazi yake.

Aliongeza, kama vazi moja litaonekana kushamiri, basi  ndiyo liwe la Taifa.

Mbunifu wa mavazi, Ndesumbuka Merinyo alisema hatuwezi kusema tuna vazi letu wakati tunatengeneza vazi kwa vitambaa kutoka nje, lakini tukiistawisha pamba yetu tukawa na vitambaa bora, vazi litatengenezwa na wabunifu wetu.

Aliongeza, kitenge na khanga inaonekana ndiyo vazi la kitanzania, hata hivyo, khanga ni bidhaa kutoka  India.

Hata hivyo, wakati wabunifu wakiamini kupata vazi la Taifa kunahitaji vitambaa vya ndani, mbunifu maarufu mzaliwa wa Zanzibar, Farouque Abdela ameifanya khanga kuwa vazi maarufu kwa kuwavalisha viongozi na watu maarufu duniani wakiwamo Bill Clinton na mkewe Maya Angelou, Miriam Odemba, Princess Diana,  Nina Simone, Magreth Chacha, ni wazi yeye anakinzana na fikra za vazi la taifa lazima litokane na vitambaa vyetu.

JU 05

Pia amebuni nguo za wanamitindo kwa kutumia  mifuko ya plastiki, mkeka na ngozi na anasema wabunifu wa Tanzania wanaiga mitindo ya nje na wanatumia vitambaa vya Afrika.

Kwa kauli yake, ni wazi wabunifu wetu wanapingana wenyewe kwani inaonekana tatizo siyo upatikanaji wa malighafi, bali ubunifu wa vazi lenyewe ambalo litawafikiwa wengi na kwa bei nafuu ili kila mzalendo alivae.

Abdela anaungana na Prof. Mwansoko kwa kusema Taifa kama Tanzania lenye makabila 120, kinachotakiwa ni kukubaliana na kuifanya khanga kuwa vazi la taifa na kuruhusu makabila yaliyo na mavazi yao yaendelee nayo badala kupendekeza vazi lingine.

Wamang’ati wanapatikana Hanang, Kaskazini mwa Manyara. Vazi lao ni Agwadabadaida ambalo anavaa mwanamke na hutengenezwa kwa kutumia ngozi ikinakshiwa na  Shanga.

Miaka ya nyuma vazi hili lilikuwa likipewa heshima sana, hata hivyo, kutokana na hali ya utandawazi na mwingiliano wa kiutamaduni, kasi ya uvaaji wa vazi hilo umeshuka na sasa wanavaa ya kawaida.

Yapo pia makabila yenye mavazi yao lakini huvaa kwa nyakati tofauti kulingana na tamaduni zao.

Kwa sehemu za mijini ni nadra kuwaona watu wakiwa katika mavazi yao ya kitamaduni na mara chache hutumika wakati wa sherehe za kitamaduni za kabila husika ikiwamo kwenye harusi.

Hata hivyo, Serikali bado haijaachana na jambo hilo na kazi kubwa ipo kwa wabunifu wetu kulifanikisha.

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliwahi kusema tangu mwaka 2017, Wizara ya Utamaduni ilisema vazi la taifa litabatikana haraka, lakini hadi sasa bado kimya.

Aliyasema hayo baada ya msanii wa vichekesho vya jukwaani, Eliud kukumbushia wakati akifanya kazi yake ya uchekeshaji.

Tunamshukru waziri mkuu kwa kulipa nafasi jambo hili ili liweze kukamilika nasi tuwe na vazi letu la Taifa.

Tunaamini baada ya kukamilika, litakuwa na mvuto na kutambulika kila mahali na kutufanya tuudumishe utamaduni wetu kuanzia mavazi, lugha ya Kiswahili na Mtanzania ajivunie kuongea kila anapokwenda.