Will Smith ajiondoa tuzo za Oscars baada ya kofi kwa Rock
Muktasari:
- Will Smith amejiuzulu kutoka taasisi inayoandaa tuzo za wasanii wa filamu za Oscars, siku tano baada ya kumshambulia jukwaani mchekeshaji Chris Rock wakati tamasha hilo likirushwa duniani moja kwa moja na televisheni.
Los Angeles, Marekani (AFP). Will Smith amejiuzulu kutoka taasisi inayoandaa tuzo za wasanii wa filamu za Oscars, siku tano baada ya kumshambulia jukwaani mchekeshaji Chris Rock wakati tamasha hilo likirushwa duniani moja kwa moja na televisheni.
Muigizaji huyo amesema vitendo vyake, ambavyo vilifunika usiku bora kwa mwaka wa Hollywood, "vinastua na havisameheki."
"Orodha ya wale niliowaumiza ni ndefu na inamjumuisha Chris, familia yake, marafiki zangu wengi na wapenzi, wote waliohudhuria na watazamaji kote duniani waliokuwa nyumbani," amesema Smith.
"Nilisaliti uaminifu niliopewa na Academy. Niliwanyima wateule wengine wa tuzo na washindi fursa ya kusherehekea na kupongezwa kwa kazi yao isiyo ya kawaida. Nimeumia moyoni."
Waalikwa kwenye ukumbi wa Dolby Theatre walimuangalia Smith kwa bumbuwazi akipanda jukwaani na kumpiga kofi Rock shavuni baada ya mchekeshaji huyo kufanyia utani nywele za mkewe zilizokuwa zimenyolewa mithili ya kipara.
Mke huyo, Jada Pinkett Smith anaugua ugonjwa wa alopecia, unaosababisha nywele kunyonyoka.
Alirejea kwenye kiti chake na kutoa maneno machafu kwa Rock, ambaye amesifiwa na wengi kutoka na na kutulia na kuendelea na mambo kama yalivyokuwa.
Nusu saa baada ya tukio hilo, Smith alitangazwa mshindi wa tuzo ya Muigizaji Bora kutokana na nafasi yake katika filamu ya maisha ya kimichezo ya "King Richard."
Kumekuw ana habari tatanishi katika siku za karibuni kuwa waandaaji, Academy of Motion Picture Arts and Science, walimtaka Smith aondoke katika tamasha hilo, lakini alikataa.
Taasisi hiyo imesema wiki hii imeanza hatua za kinidhamu dhidi ya Smith-- ambaye ni mtu mweusi wa tano kutwaa tuzo hiyo kubwa duniani-- na kuonya kuwa anaweza kutimuliwa.
Lakini Smith ameonekana kuwawahi.
"Ninajiuzulu uanachama wa Academy of Motion Picture Arts and Sciences, na nitakubali hatua nyingine zozote ambazo bodi itaona zinafaa," amesema.
"Nataka kurejesha mjadala kwa wale ambao wanastahili kutokana na mafanikio yao na kuiwezesha Academy kuendelea na kazi yao kubwa ya kuunga mkono ubunifu na usanii katika filamu."