Billnass, Nandy: Ndoa inavyozidi kuwaimarisha kimuziki
Muktasari:
- Wawili hao ambao walianza kuwa pamoja tangu mwaka 2016, kati ya nyimbo sita walizoshirikiana hadi sasa, tano kati ya hizo wanazungumzia uhusiano wao tu.
MASTAA wanandoa Billnass na Nandy wanaendelea kuyaimba mapenzi yao kwa uzuri, kitu ambacho ndiyo hasa mashabiki wao wanapenda kuisikia kutoka kwao.
Wawili hao ambao walianza kuwa pamoja tangu mwaka 2016, kati ya nyimbo sita walizoshirikiana hadi sasa, tano kati ya hizo wanazungumzia uhusiano wao tu.
Kwa sasa Billnass na Nandy wanatamba na wimbo wao mpya, Hallo (2026) uliotayarishwa na S2kizzy, huku video yake ikiongozwa na Director Kenny, mshindi wa tuzo za AFRIMMA 2021.
Hallo ni wimbo wa mapenzi uliochanganya ladha ya Bongo Fleva na Afrobeats ukiwa unazungumzia uhusiano wa kweli wenye uvuto wa aina yake, huku ukionyesha jinsi wanamuziki nao walivyoshibana kimuziki.
Video yake ya awali (visualizer), imeonyesha nyakati mbalimbali nzuri walizofurahia pamoja ikiwemo tukio la kuhadhimisha miaka miwili ya ndoa yao hapo Julai 2024.
"Na kama ukinimiss please just call me, Hallo. Nishafumba macho kwengine sioni, Hallo. Ukiwa karibu moyo unautuliza, Hallo...," anaimba Nandy mwanzoni kabisa mwa wimbo huo.
Kwa mujibu wa Billnass ambaye ndiye amemshirikisha Nandy, hiyo ndio itakuwa kolabo yao ya mwisho, huku akisisitiza anaamini itafanya vizuri hadi kushinda tuzo za Grammy ambazo ndizo zenye hadhi zaidi katika muziki duniani.
"Kwa pamoja tumefanya nyimbo nne, pamoja na mapokezi mazuri ya nyimbo zote hizo lakini hakuna wimbo bora tuliowahi kufanya ukafikia viwango vya Hallo, na hii ndio itakuwa kazi yetu ya mwisho kushirikiana," alieleza Billnass.
Kwa jumla nyimbo walizoshirikiana wao wawili tu ni Bugana (2019), Do Me (2020), Party (2021), Bye (2022), Totorimi (2024), na Hallo (2026), huku Party (2021) wakishirikiana na Mr. Eazi kutokea Nigeria.
Wimbo wao wa tatu kuachia, Bye (2022) ulikuwa maalum kwa ajili ya ndoa yao ambayo ilifungwa hapo Julai 2022 katika kanisa la KKKT Mbezi Beach, Dar es Salaam.
Video yake iliyosimamiwa na Director Hanscana, imeonyesha matukio mbalimbali kuelekea ndoa yao kuanzia sendoff, wakiapa kanisa hadi sherehe yenyewe iliyofanyika Ukumbi wa Mlimani City.
Ikumbukwe wawili hao walikuwa wanasoma pamoja CBE ila hawakuwa na ukaribu hadi pale wote walipokuja kufanya vizuri kimuziki. Mwaka 2016, waliitwa katika tamasha la Fiesta, wakaenda kutumbuiza Sumbawaga ila wakaenda kulala Mbeya na huko ndipo mambo yalipoanzia.
Kipindi tetesi za uhusiano wao zimepamba moto, ndipo Nandy aliingiza sauti za chini (back vocal) katika wimbo wa Billnass, Sina Jambo (2017) ambao ulifanya vizuri kwa wakati huo.
Lakini uhusiano wao waliendelea kuufanya siri mbele ya mitandao na vyombo vya habari hadi mwaka 2020 walipochumbiana na kuja kufunga ndoa Julai 2022, na sasa wana mtoto mmoja huku wakishirikiana katika nyimbo sita zilitoka kati ya 2019 hadi 2026.
Mnamo Agosti 2022, ndipo walijaliwa mtoto wao wa kwanza, Kenaya (Naya Bill), ila waliamua kumficha mtoto huyo mbele ya mitandao ya kijamii hadi alipotimiza umri wa mwaka mmoja. Agosti 2023, ndipo sura yake ilionekana mtandaoni kwa mara ya kwanza.
Mastaa hao walipoutambulisha ukurasa rasmi wa Naya kwa mashabiki wao katika mtandao wa Instagram, ndani ya siku moja tu uliweza kupata wafuasi (followers) zaidi ya 100,000 na sasa wamefikia 834,000.
Hiyo ni kwa sababu Nandy ni miongoni mwa wanamuziki 10 kutokea Tanzania wenye wafuasi wengi Instagram akiwa nao milioni 10.6, huku Billnass akiwa na milioni 5.9.
Mbali na hilo, wasanii hao wamepingana na hata kuishinda ile dhana kuwa wanamuziki wanapooa au kuolewa ushawishi wa sanaa yao hushuka kutokana na kupoteza mvuto kwa mashabiki wengi, lakini kwao nyimbo kubwa zaidi zimetoka baada ya ndoa.
Mathalani, Billnass ameshinda tuzo za muziki Tanzania (TMA) kwa mara ya kwanza na kutoa nyimbo zilizopata namba kubwa katika majukwaa ya kidijitali kuliko zote za mwanzo akiwa bachela.
Ikiwa ni miaka zaidi ya 10 tangu alipotoka na wimbo wake, Raha (2014), Billnass alishinda tuzo ya TMA kwa mara ya kwanza katika kipengele cha Msanii Bora wa Kiume wa Hip Hop 2022.
Katika TMA 2015 na 2021, hakushinda ila baada ya kuingia tu katika ndoa, basi ikawa baraka kwa kushinda mbele ya wakali wa Hip Hop kama Fid Q, Joh Makini, Country Wizzy na Kala Jeremiah.
Utakumbuka ushindi huo ulikuja baada ya Billnass kufanya vizuri na wimbo wake, Puuh (2022) ulioweka rekodi kama wimbo wa Bongo Fleva uliosikilizwa zaidi Boomplay kwa mwaka 2023 ukiongoza chati kwa wiki sita.
Nandy ambaye alikosolewa na Baba Levo aliyedai baada ya kufunga ndoa ameshindwa kutoa wimbo uliofanya vizuri zaidi, alijibu kwa vitendo kauli hiyo kwa kuachia wimbo wake, Dah! (2024) akimshirikisha Alikiba.
Wimbo ulipokelewa vizuri na kwa sasa unashikilia rekodi kama wimbo wa Nandy uliofanyika vizuri YouTube na video yake imeshatazamwa mara milioni 32, huku remix yake ikiwa na milioni 8.
Kabla hajaolewa hakuna wimbo wa Nandy ulioweka rekodi kama hiyo, hata ule wa kwanza kumshirikisha Alikiba, Nibakishie (2020) uliotoka miaka mitano liyopita hadi leo haujafikia hata nusu ya namba hizo.