FUNGA KAZI: Yaliyojitokeza tamasha la Miaka 30 ya Bongo Fleva
Muktasari:
- Bongo Fleva ambayo ulianza miaka ya mwishoni mwa 1990 na mwanzoni mwa mwaka 2000 unakumbukwa kwa mengi ikiwamo waanzilishi wake na katika kulitambua hilo, baadhi walitambuliwa kwa kupewa tuzo akiwamo Profesa Jay na anatajwa kama msanii aliyesababisha muziki huo kukubalika.
BAADA ya kusubiriwa kwa hamu, hatimaye Tamasha la Miaka 30 ya Bongo Fleva lilifana katika Ukumbi wa Mlimani City na kuacha gumzo kutokana na yaliyotokea, huku mashabiki wakikumbushwa ngoma kali za kitambo zilizoamsha shangwe kila wasanii walivyopanda.
Bongo Fleva ambayo ulianza miaka ya mwishoni mwa 1990 na mwanzoni mwa mwaka 2000 unakumbukwa kwa mengi ikiwamo waanzilishi wake na katika kulitambua hilo, baadhi walitambuliwa kwa kupewa tuzo akiwamo Profesa Jay na anatajwa kama msanii aliyesababisha muziki huo kukubalika.
Pia tuzo ya mchango wa Bongo Fleva ilienda kwa Ruge Mutahaba na Shaban Khamis Taletale kutokana na kuusukuma muziki huo ikiwa ni baadhi na wapo wengi walichangia mafanikio hayo.
Katika tamasha hilo ambalo lilianza saa 2:00 usiku, mashabiki waliiteka shoo na hata kuzuia kuingizwa mamabo yanayohusu siasa ikiwamo utambulisho wa viongozi na walichotaka ni burudani tu kutoka kwa wasanii hao ambao walikuwa wengi na wote walitakiwa kuimba.
Hapa Mwanaspoti lililokuwapo ukumbini hapo linakuchambulia baadhi ya matukio yaliyojitokeza na kubwa zaidi ni shoo kali kutoka kwa wasanii mbalimbali waliopania na kuliteka jukwaa kwa kila dakika tano walizopewa ingawa wapo waliozidisha kutokana na shangwe la mashabiki akiwamo Juma Kassim Nature 'Kiroboto'.
MASHABIKI MAPEMA TUU!
Hakuna aliyetaka kukosa tamasha hilo na hadi inafika saa mbili muda wa shoo kuanza, tayari ukumbi ulikuwa umefurika na kuonyesha wazi mashabiki walikuwa na hamu ya kuona na kusikia midundo ya zamani zilizorekodiwa na maprojuza wakali wakiwamo P Funk, Bony Love, Master Jay, Enricko, Miika Mwamba, Castro Ponela, Marco Chali, Said Comorien na wengine ambao kwa hakika ndio waliowafanya wasanii hao kutamba hadi sasa.
GUMZO SHOO IKIENDELEA
Wakati tamasha likiendela, mashabiki walishindwa kuzuia hisia zao na katika pitapita za Mwanaspoti ukumbini hapo, liliwasikia baadhi wakisifia nyimbo za wasanii, huku wengine wakiimba pamoja na wasanii hao kwa sauti kubwa ikiwamo kupelekewa kipaza sauti na kuimba mistari ya nyimbo na kuonyesha kukatwa kiu yao ya muda mrefu wa kuwashuhudia katika jukwaa wakifanya yao.
JUA KALI, NYOTA NDOGO NDANI
Wasanii wa Kenya waliongeza mvuto wa tamasha ambao ni magwiji wa muziki Jua Cali na Nyota Ndogo. Uwepo wao ulionyesha uhusiano uliokuwapo tangu mwanzo kwa wasanii wa Tanzania na Kenya na hao ni kama wawakilishi wa mastaa wengi wa nchi hiyo na Uganda wakiwamo Nonini, Chamilion, Jaguar, Nameless, Necessary Noise na wengine wengi ambao wamekuwa wakishirikiana na wasanii wa Tanzania.
ALIKIBA ARUKA UTEPE, ATIKISA JUKWAA
Kilichowavutia wengi ni kitendo chake cha kuruka utepe kutoka sehemu alikokuwa amekaa na mashabiki na kupanda jukwaani kuungana na Dully Sykes. Alipoanza kuimba, ukumbi mzima ulilipuka kwa shangwe, huku mashabiki wengi wakiimba nyimbo zake kuanzia mwanzo hadi mwisho, jambo lililoonyesha bado ana mvuto mkubwa na nafasi ya kipekee katika muziki wa Bongo Fleva.
WAKONGWE WAFUNIKA, HARD MAD ASAPRAIZI
Wakati tamasha hilo likiwa katika maandalizi, msanii Hard Mad alijitokeza na kudai ametengwa katika tamasha hilo na kuacha gumzo mitandaoni. Hata hivyo, mwanzo wa tamasha hilo, alipanda jukwaani na kuamsha shangwe na baadhi ya waliojua hatakuwepo kushtuka walivyomwona.
Baada ya hapo, wasanii wengine wengi walipanda jukwaani wakiwamo Hard Blastaz Crew 'HBC' ingawa alikosekana Profesa Jay na aliwakilishwa na wenzake Fanani na Big Willie.
Juma Nature, Gangwe Mob, Chid Benz, Daz Nundaz, TMK Family, Kassim Mganga, Banana Zorro, Jay Moe, Saida Karoli, AY na Mwana FA, King Crazy GK, Saigon ni kati ya walipokelewa kwa shangwe kubwa kutoka kwa mashabiki, wakiwakumbusha enzi ambazo nyimbo zao zilitawala redioni, televisheni na majukwaa mbalimbali nchini.
Wengine waliokiamsha ni Chege, Temba, Mwasiti, Tunda, Stara Thomas, Dully Sykes, Mchizi Mox, Mabaga Fresh, Solid Graund Family, Kikosi cha Mizinga, Nako 2 Nako,Q Chief, Domokaya, Hfasa Kazinja, 20 Per Cent na wengine wengi.
JUMA NATURE AFANYA ALICHOZOEA KUFANYA
Hakuna ubishi kati ya wasanii wa Bongo Fleva waliowahi kutikisa na wanaotiukisa hadi sasa ni Juma Nature. Haijalishi atapanda jukwaa gani lakini mvuto wake kwa mashabiki haujawahi kuisha na ndiye aliyeonekana kuliteka tamasha.
Kama alivyowahi kuujaza Ukumbi wa Diamond Jubilee wakati wa uzinduzi wa albamu yake ya Ugali zaidi ya miaka 20 iliyopita, ameendelea kuwa na mashabiki wengi wa kizazi cha zamani na cha sasa na kuonyesha kukubalika zaidi.
DUDU BAYA ALITAKA KUHARIBU
Licha ya mambo mazuri yaliyotokea na kuwapa watu burudani, lakini katika kila tukio zuri hakukosekani kasoro ndogondogo na katika tamasha hilo msanii Dudu Baya ambaye inadaiwa alikuwa amelewa, alisikika akitoa maneno machafu na nusura tamasha liishie hapo hapo kabla ya kutolewa na shoo kuendelea kwa wasanii waliobaki wakiwamo Fid Q ambaye ndiye aliyefunga kwa kuimba nyimbo zake.
Kwa jumla, tamasha la Miaka 30 ya Bongo Fleva limeonyesha nyimbo za zamani bado zinaishi mioyoni mwa mashabiki na wakongwe wa muziki huo bado wana uwezo wa kujaza ukumbi na kutoa burudani ya kiwango cha juu. Hata hivyo, changamoto za usimamizi wa muda na matukio yaliyojitokeza mwishoni mwa tamasha zimeacha mjadala kuhusu namna ya kuboresha matamasha makubwa ya aina hiyo siku zijazo.