Wasanii walivyonogesha jukwaa usiku wa Muungano Dar

USIKU wa kuamkia leo nyota kadhaa wa muzi wa Bongofleva wamelishambulia jukwaa la burudani katika usiku wa Tamasha la Muungano uliofanyika katika viwanja vya Tanganyika Packers, Dar es Salaam.

Burudani kutoka kwa mastaa hao zilitawala huku kukiwa na ubunifu, vionjo na manjonjo ya aina yake kutoka kwa kila nyota aliyepanda jukwaani kukonga nyoyo za watu waliohudhuria.

Wasanii ambao walipata nafasi ya kukiwasha kuanzia kwa Rayvann hadi kwa Nandy, Marioo hadi kwa harmonize na wengineo mambo yao jukwaani yalikuwa bambam wakiwaacha Watanzania waliohudhuria wakiserebuka mwanzo mwisho.

Wafuatao ni wasanii walioingia na ubunifu kwenye jukwaa kama
njia ya kuleta uchangamfu mahala hapo:
 
RAYVANN: Nyota huyu alifanya vizuri kwa jinsi alivyoingia kwenye jukwaa akiwa amevaa nguo zake na juu yake amevaa vazi la jikoni 'aproni' na kofia zenye rangi nyeupe.
Pingine hilo liliashiria ni kwa nini anatambulika kama 'chui`wa muziki wa Bongofleva.

HARMONIZE: Huyu alipanda jukwaani akiwa amevaa suruali ya jinzi, tisheti ya rangi ya zambarau na kofia ya rangi hiyo akaanza kuimba wimbo wake wa 'Amelowa' na katikati ya wimbo huo akavua tisheti na kuvaa nyingine na nyingine juu yake jumla akawa amevaa mbili kwa wakati mmoja.
Baada ya muda akavua tisheti zote akaanza kucheza akiwa tumbo wazi na kumpandisha jukwaani mpenzi wake wa sasa ajulikanaye kwa jina la Posh na kuanza kucheza naye.



NANDY: Mwanadada huyo alipanda jukwaani akiwa amevaa track suit na unaweza kusema ni kutokana na hali ya hewa ya sasa ya mvua, baridi au ni swaga zake za kutaka kuonekana yuko tofauti na wasanii wake ambao aliwavalisha taiti fupi na bodi suti.

Nandy aliimba wimbo wake wa Daah na baada ya hapo akachomekea remix ya wimbo huo ulioimbwa na wasanii wengi akiwemo G Nako kutoka kundi la Weusi, ambaye alipanda jukwaani na kuendelea kutumbuiza nyimbo za Weusi akiwa peke yake huku Nandy akiteremka kwenye jukwaa.

MARIOO: Zamu ya mwamba huyu ilipofika alipanda kwenye steji akiwa amevalia tisheti ya rangi ya orange na suruali nyeusi. Kisha alimpandisha stejini dansa wake wa zamani Chino anayefanya vizuri kwenye nyimbo zake. Sshangwe lilitawala kwenye viwanja hivyo kwani wawili hao siku za karibuni walikuwa na tofauti baada ya Chino kujitoa na kujisimamia mwenyewe. Marioo ndiye mwanamuziki aliyeongoza kuwapandisha wanamuziki wenzake jukwaani na kucheza na madansa wake mwanzo hadi mwisho

Wasanii wengine waliotumbuiza kwenye tamasha hilo ni Dogo Janja, Tunda Man,  Misomisondo, TOT Band, Dulayo na wengine wengi.