Mume wa mtu kanipa ujauzito

Muktasari:

ANKO Lao, kijana miaka 22 kuna binti nampenda sema nikimwambia suala la kufunga ndoa hataki. Nifanyaje?

Plumber Jr, Pwani

Jibu: Hizo gia ulizoingia nazo kwa bibie ndo zinazokufelisha kwani amekushtukia ni saundi tu. Kama kweli unahitaji ndoa si ufuate taratibu kwenda kujitambulisha kwao kwa kuposa na kuharakisha kuoa uone kama ndoa haitafungwa... wee vipi.

1. ANKO Lao, binti miaka 20, shida yangu nilikuwa na mpenzi aliyenipa ujauzito na kuukataa na kibaya sikujua kama alikuwa na mke. Nifanyeje?

Janeth Ngabali, Dodoma

Jibu: Kiherehere gani kilichokufanya uneng’eneke kabla ya kuolewa? Hii ndio tabu yenu mabinti wa zama hizi hampigiwi mnacheza, mnavagaa hadi waume za watu bila kujua. Ulichotafuta umekipata. Kwa sasa zungumza na jama’ako ujue atakusaidiaje, kwani kama hakuna ushahidi ni ngumu kukubali mzigo hadi dogo azaliwe na mkapime DNA. Kazi kwako kwani kila mchuma janga...!


2. ANKO Lao, kuna demu nimeishi naye miaka mitatu, lakini kabadilika na ananiona kama takataka. Nifanyaje?

Rodri Palace, Iringa

Jibu: We’ miaka mitatu unaishi na mtoto wa watu bila ya ndoa unaona freshi. Bibie kakubadilikia baada ya kugundua unamfuja bila kuharakisha kumuoa ili awe na heshima mbele ya jamii. Hutakiwi kupaniki, kwani kosa ni lako. Harakisha kuoa uone kama mahaba hayatarudi kama zamani...we vipi?


3. ANKO Lao, binti wa miaka 17 na nina mpenzi ninayempenda ila shida iliyopo rafiki yangu anasema amewahi kutongozwa naye. Nifanyeje?

Loveness Elihaki, Kilimanjaro

Jibu: Kwa umri huo ningekushauri ungepambana kuitafuta kesho yako, kwa maana kama unasoma komalia kitabu badala ya kujipa stresi katika malavidavi, kwani akili na mwili havijakomaa kubeba jukumu la ishu hizo. Hivyo tu, hata kama sijui shogaa’ko alishatokewa na jamaa..potezea tu.


4. ANKO Lao, kijana miaka 24 kuna binti huwa tunashauriana mambo mengi ila nikimwambia masuala la mapenzi huwa hataki kabisa. Nifanyaje?

Jaden Jr, Moshi

Jibu: Hili ndilo kosa linalowaangusha mayanki wengi wa zama hizi tangu awali ulipaswa kuonyesha nia yako kwake na sio kuishi kilokole kumbe unampigia hesabu, kisha kuja kumshtukiza, huenda tayari jimbo linamilikiwa na mtu ndio maana anakuotezea wakati ulishamzoesha we’ ni mshauri nasaha.


5. ANKO Lao, binti miaka 23, nina mpenzi nampenda sana ila kuna muda mwingine nakosa hisia naye. Naomba ushauri wako.

Anitha Athuman, Dar

Jibu: Sijajua kama mnaishi pamoja au kila mtu kivyake, lakini kama anapika na kupakua pamoja ni wazi kuna stresi zinazokusumbua, labda kwa kutarajia makubwa kutoka kwa jamaa na kutoyaona au kuchoshwa na kazi unazofanya kutwa. Jengeni mazoea ya kutoka pamoja mara moja moja kukumbushia enzi mnatokeana. Pia kujenga upya penzi lenu badala ya kubanana kila siku nyumbani tu, inachosha! 


6. ANKO Lao, binti miaka 24 nimeolewa na nina watoto wawili ila kuna wanaume wameshanitongoza na siwataki. Nifanyaje?

Fadhila, Tanga

Jibu:Sina hakika kama umeolewa kweli au unaishi tu na mtu uliyezaa naye hao watoto, kwani kwa mke wa mtu tena anayejiheshimu akatongozwa na kushindwa kuweka wazi uhusiano alionao nahisi hujatulia ndio maana unaruhusu wakutokee. Ushauri wangu kama kweli umeolewa, jitulize!


7. ANKO Lao, kijana miaka 19 napenda kuwa kocha mkubwa nje ya nchi ila familia yetu ni afadhali ya jana. Nifanyaje?

Ibrashua, Musoma

Jibu: Sina hakika hata kama unajua unachokitaka maana ishu ya ukocha na mambo ya familia vinaigilianaje? Kama kweli unatamani ukocha komaa kwanza kucheza mpira ili uujue kwani umri unakuruhusu, kisha ukishajua ei bii sii za boli, kasomee ubobee, huwezi shiba kwa kutamani bila ya kula chakula. Hivyo tu.


8. ANKO Lao, kijana miaka 26 nimeoa na nina watoto wawili lakini mke wangu ana changamoto hataki nishike simu yake hata kidogo. Nifanyeje?

Dulla, Tanga

Jibu: We’ simu ya mkeo ya kazi gani kama tayari ameshakueleza hataki uiguse...jiamini braza. Tabia ya ung’ang’anizi itamlazimisha naye kuiganda simu yako utaweza kushikilia bomba? Halafu hadi mmeoana na kuzaa watoto ni wazi mnapendana na kuheshimiana. Acheni kuchunguzana mtatibuana.


9. ANKO Lao, binti miaka 20 kuna mtu ananipenda sana, ila simpendi kwa sababu sioni kama ananifaa. Nifanyeje?

Moynee Ivan, Masaki

Jibu:Unachokifanya ni sawa na kupiga teke fuko la pesa na ujue mapema siku zote mchagua nazi hupata koroma...unaweza kumpotezea, ila utakuja kumkumbuka pale utakapozeekea nyumbani bila ndoa kwa mashauzi uliyonayo. Dunia ya sasa inahitaji anayekupenda na sio kutumiwa. Shauri yako.


10. ANKO Lao, kijana miaka 22 kuna binti tunapendana ila nikiomba mzigo anasema hadi amalize masomo naye ni mwanachuoni. Nifanyaje?

Kandolo Gomsi, Iringa

Jibu:Huyo bibie ni mtu anayejielewa, kwani anajua kosa moja atakalofanya itakula kwake na kukatisha ndoto alizonazo. Kama kweli una ni ya dhati muache amalize masomo na ufanye chapu umuoe ujipakulie pilau nyama nyingi na sio staili unayotaka kuitumia ya kisela sio sawa. Sawa sawa?

11. ANKO Lao, kijana miaka 22 kuna binti nampenda sema nikimwambia suala la kufunga ndoa hataki. Nifanyaje?

Plumber Jr, Pwani

Jibu:Hizo gia ulizoingia nazo kwa bibie ndo zinazokufelisha kwani amekushtukia ni saundi tu. Kama kweli unahitaji ndoa si ufuate taratibu kwenda kujitambulisha kwao kwa kuposa na kuharakisha kuoa uone kama ndoa haitafungwa... wee vipi.


12. ANKO Lao kuna binti nampenda ila shida kubwa ni kwamba haniamini. Nifanyeje?

Athuman Kimbo, Arusha

Jibu: Inategemea na nyendo zako na pia namna ulivyomtokea wakati unampigia misele. Kitu muhimu ni kuzungumza naye na kumueleza we’ ni wake na atulize moyo, lakini kama una macho mia mia ni wewe jitathmini tu. Vinginevyo utaachwa solemba.


13. ANKO Lao, binti miaka 21 nilikuwa na mchumba aliyenipa ujauzito na nilipomwambia alikataa na kwa sasa hapatikani na mtoto ananisumbua. Nifanyeje?

Magreth, Sengerema

Jibu:Ulibugi mwenyewe kwa kupanda mtumbwi wa vibwengo kama ungejituliza hadi uposwe na kuolewa usingejilengesha kwa msela ambaye hakuwa na mipango  wala kulea mtoto. Cha kufanya kama unawajua nduguze jipeleke mtoto atulie.


14. ANKO Lao, kijana miaka 23, kuna msichana nampenda ila wakati tunasoma alikuwa anaongoza na mimi nilikuwa nashika nafasi za mwisho sasa naogopa isije kunitokea hadi mapenzini. Nifanyeje?

Pablo Almas, Dar

Jibu: Acha woga wa maisha wewee kwani kuongoza darasani ndo kitu gani buana.Wapo tuliowaongoza darasani, lakini leo wanatuongoza kimaisha kitu cha muhimu ni wewe kujiamini ukiendekeza fikra hizo za kiduwanzi mapenzini utaburuzwa kweli. Shuri yako.


15. ANKO Lao, binti miaka 18 naishi na mwanaume aliyenizidi umri ila mambo anayofanya ni kama ana mtu mwingine. Nifanyeje?

Treasure Edson, Mafinga

Jibu: We’ mwana una kiranga katika umri huo tayari umeanza kuneng’eneka hadi kujipeleka gheto la mbabu? Kama umeshagundua ana mademu wengine we’ unasubiri nini kumtema au unataka upewe kijidudu ukahangaike nako kwenu. Nilidhani kwa umri huo ungepambana kuitafuta kesho yako.


16. ANKO Lao, kijana miaka 24 nina mpenzi ila tunagombana mara kwa mara sababu ya simu yaani hataki kuona nikichati. Nifanyeje?

Miraji Athuman, Dodoma

Jibu:Hili ndilo tatizo la kuvamia malavidavi kabla ya maandalizi, we’ ushajua mwenzako hapendi jambo hilo kitu gani kinakufanya uendelee kumkera au braza bibie kalazimisha kuzama getoni kwako na sasa unataka kumtoa kiaina kwa kuchati hovyo?


17. ANKO Lao, kuna kijana niko naye katika uhusiano na kaniahidi kunioa ila shida ni dini, yeye Mwislamu nami Mkristo. Nifanyeje?

Enata, Mwanza

Jibu:Ishu za dini hazijawahi kuwa kikwazo kwa wapendanao ...ni wazi nyie mlibebana kwa ajili ya kupiga deiwaka na sio malengo ya kuishi pamoja nd’o maana sasa mnatafuta visingizio. Kaeni chini mjadiliane ili mjue moja kama mlisongeshe jahazi au kila mtu ashike lake. Hivyo tu.


18. ANKO Lao, kuna mwanamke nilizaa naye mtoto ila akaninyima akidai si wangu, lakini kwa sasa anataka kunipa. Nifanyaje?

Amisi Almas,  Morogoro

Jibu:Kwani wewe unasemaje? Dogo ni wako kweli au umepakaziwa? Huenda bibie alikukataa kwa jinsi ulivyopokea taarifa za ujauzito au kushindwa kumhudumia. Hao wenzetu wana hasira na uamuzi wa haraka bila kutafakari...Na kwa sasa akili zimemkaa sawa na kugundua alikuwa anajikomoa na sio kukukomoa, kaamua kurudisha mpira kwa kipa. Kazi kwako kapimeni DNA ujiridhishe maisha yaendelee kama ulihusika kufunga.


19: ANKO Lao, kijana mwanafunzi wa mwaka wa pili na kuna msichana chuo ana ujauzito wangu, lakini naogopa kuutoa. Naomba ushauri wako.

Jerrad Nzalu, Namanga

Jibu: Nyie nd’o mnaofanya vijana wote waonekane watu wa hovyo yaani badala ya kukomalia kitabu kilichowapeleka chuo nyie mnaenda kubebeshana mizigo msiyoweza kuibeba. Kibaya zaidi mmeshindwa kujali gharama na fedha za wazazi wanaojinyima ili kuwasomesha. Kwa taarifa yako hilo unalo...mwanakulitafuta, mwanakulipata ni aibu kwa usomi wako kushindwa kutumia zana katika dunia hii ya maradhi. Ujue mapema tu kuflashi ni dhambi na kosa kisheria. Kazi kwako.


20. ANKO Lao, binti miaka 18 nina boy nampenda sana, ila tatizo lake kila nikimuomba pesa hanijali. Nifanyeje?

Masesa Juma Shabaan

Jibu: Hilo ndilo tatizo lenu mabinti wa zama hizi, yaani mkipendwa tu mnataka mpendwe na shida zenu kana kwamba hamna wazazi wa kuwahudumia. Huyo jama’ako ana haki ya kukuchunia kukupa hela kwani sio mzazi wako. Pia kama unaona pesa zinapatikana kirahisi tafuta zako upunguze makasiriko.