Wapenzi 10 wa Mondi na walivyoachana

UKIACHANA na muziki wake, ukweli unabakiwa kuwa umaarufu alionao Diamond Platnumz pia unachagizwa kwa asilimia kubwa na kuwa na uhusiano na wanawake mbalimbali maarufu kutoka kiwanda cha mitindo, muziki na filamu.
Kwa kipindi cha miaka 12 jina lake limehusishwa kuwa na uhusiano na wanawake zaidi ya 10 maarufu nchini Tanzania, Uganda na Kenya, katika mataifa hayo Diamond amezaa na walau mwanamke mmoja wa huko. Kwa sasa Mondi inadaiwa anakula nma kupakua na Zuchu.
Hata hivyo, ukosefu wa fedha, habari za usaliti, kazi na migororo ya ndani ya kifamilia imechangia kwa asilimia kubwa kwa Diamond kuachana na wanawake hawa 10 ambao wanafahamika hadi sasa;


1. SARAH
Pengine huyu ndiye msingi wa mafanikio aliyonayo leo Diamond katika muziki, Sarah aliuvunja moyo wa Chibu hadi kupelekea kuandika wimbo 'Kamwambie' uliomtoa kimuziki mwaka 2009 na uliobeba jina la albamu yake ya kwanza.
Diamond alidai alishuhudia Sarah akichukuliwa na mwanaume mwenye fedha aliyekuwa anafanya kazi Mizani, Kibaha, kwake magari mapya ya kifahari haikuwa shida, hivyo akajikuta akimpoteza Sarah wake.
"Alikuwa mwanamke wangu lakini sikuwa na mbele wala nyuma, basi akawa na watu tofauti tofauti, ulifika muda akaniona mzigo, akaniacha!, basi ile hasira ilinifanya nikaandika wimbo mzuri, Kamwambie ndio nikatoka," alisema Diamond.
Na hata nyimbo zake za awali za kuumizwa kama 'Mbagala' msingi wake ni kutendwa na Sarah, kwa mujibu wa Diamond, alipenda kiasi kwamba hata kipindi yupo na Wema alijikuta akimzungumzia kitu ambacho Wema hakupendezwa nacho.


 
2. WEMA SEPETU
Baada ya Mr. Blue, TID, Steve Kanumba na Chazz Baba, Diamond akawa mwanaume mwingine maarufu Bongo aliyefaidi penzi la Miss Tanzania 2006 na msanii wa filamu, Wema Sepetu ingawa drama zilikuwa ni nyingi sana.
Walishakutana Club hapo awali, wakaendelea kuwasiliana Facebook kipindi Wema yupo Marekani na aliporudi wakaanza kuishi pamoja, hata hivyo, walikuwa kila mara wanachaana na kurudiana, Diamond alisema chanzo kilikuwa ni usaliti wa Wema.
"Mwenzangu alikuwa yupo na mtu mwingine, nikamuuliza ananiambia ndiyo, kule anataka na kwangu anataka, nikaja nikasikia kuna mtu mwingine tena ukiacha yule, nikachunguza nikaona kweli, baada ya kugundua nikaona sipati ushirikiano kama wa mwanzo," alisema Diamond.
Hata hivyo, Wema alidai hakuna kipindi alikuwa na uaminifu katika uhusiano kama alivyokuwa na Diamond, alimpenda sana, na alianza kuvutiwa naye pale alipokuwa akimfariji baada ya kutendwa na Chazz Baba.


3. JOKATE MWEGELO
Ni Miss Tanzania namba mbili 2006, ametokea kwenye video ya wimbo wa Diamond 'Mawazo', kwa mujibu wa Wema, wakati video hii inafanyika inadaiwa ndipo penzi la Diamond na Jokate lilichipuka kitu ambacho kilipelekea kuachana kwao kwa mara ya kwanza.
"Tuliachana baada ya yeye kunisaliti na Jokate, tulikuwa tunapenda sana, kwake nilikuwa nimesharidhika na maisha ambayo nipo nayo hata kama sio mazuri. Nadhani pia inagharimu mwanaume akishajua anakutawala, kwa hiyo ni shetani au ibilisi alimuuingilia," alisema Wema.
Hata hivyo, inadaiwa baadaye Diamond aliachana na Jokate kisha kurejea kwa Wema, lakini Diamond anasema kurudi tena kwa Wema ni kitendo kilichomuumiza Jokate.
"Jokate alikuwa hana hatia, hawakuwahi kunikosea kitu chochote kabisa, halafu nikamuingiza kwenye matatizo watu wakamchukulia tofauti, kuna muda nikikaa naona nilimkosea. Sijui hata nilirogwa, sijui!," alikaririwa akisema Diamond.


4. PENNY
Uhusiano huu wa Diamond na Penny ulikuwa na drama nyingi licha ya kuonyesha wanapendana, walikuja kuachana baada ya kusambaa picha za Diamond na Wema wakiwa Hong Kong ambapo walidai wanafanya movie lakini kumbe ndio ulikuwa mwanzo wa kurudiana tena!.
Hilo lilimuumiza Penny, sio tu kuondoka kwa Diamond, bali Wema alikuwa amemshinda vita kutokana wakati yupo na Diamond, Wema angepiga simu usiku akimtaka Diamond na Penny angechukua simu na kumjibu Wema; tuache tulale.
"Watu wanaachana kwa sababu nyingi, nilihisi kwamba nahitaji kumpa nafasi, wote ni vijana na wakati mwingine tunahitaji nafasi kugundua vitu vipya, kuona kipi hasa unachokihitaji katika maisha, hivyo nilihisi wote tulihitaji hicho, hivyo nikampa nafasi na mimi kuchukua nafasi," alisema Penny.  
Kabla ya kuachana kwao, ilidaiwa Penny alikuwa ni mjamzito hadi Diamond kumnunulia gari la kwenda kliniki lakini ujauzito huo ulikuja kuharibika. Hata hivyo, Diamond katika wimbo wake 'Sikomi' anasema kuna mwanamke (bila kutaja jina) alitoa ujauzito wake licha ya kumuhonga na gari.


5. JACQUELINE WOLPER
Uhusiano na Diamond na Jacqueline Wolper ulikuwa wa muda mfupi sana na hakuzungumzwa wala kuandikwa kama ilivyokuwa kwa Wema na Penny zaidi ya tetesi hadi pale Wolper mwenyewe alipokuja kuthibitisha kuwa waliwahi kuwa wapenzi.
"Niliwahi kuwa Diamond, tulikuwa na uhusiano lakini alikuwa mshirika wa kibiashara, alikuwa hawezi kulala bila kuniona ila tulikaa kama mwezi mmoja, na sasa amebaki kama rafiki yangu," alisema Wolper.
Miaka michache mbele, Wolper alikuja kuzama kwenye penzi jipya na Harmonize, msanii aliyekuwa anachupukia chini ya WCB Wasafi, lebo yake Diamond jambo liloacha maswali. Inakuwaje tena!?.
Ikumbukwe Jacqueline Wolper amewa
hi kuwa na uhusiano na Mastaa maarufu Bongo kama Jux na Alikiba, sasa amefunga ndoa na Mwanamitindo, Rich Mitindo, huku wakiwa tayari wamejaliwa watoto wawili ambao walizaliwa kabla ya ndoa yao.


6. IRENE UWOYA
Kwa mujibu wa aliyekuwa mume wa Irene Uwoya, Marehemu Hamadi Ndikumana, ni kweli Diamond alikuwa na uhusiano na mkewe, huku akiwataja na mastaa wengine kama Msamii na Jaguar kutokea nchini Kenya.
"Ni mara ngapi nilikuuliza kuhusu kulala na Diamond ukaapa kufa?, ila mwisho wa siku mwenyewe ukasema kwanini ulifanya vile" ni sehemu ya ujumbe alioandika Ndikumana Instagram  Agosti 2017.
Hata hivyo, tayari Diamond alikuwa amekanusha vikali jambo hilo ambalo liliriporiwa na magazeti ya udaku Tanzania kwa ushahidi wa picha za CCTV Camera, Chibu alisema yeye na Irene ni kama Kaka na Dada, hamna lolote!.
"Ujue Irene mimi namheshimu sana, kwa sababu hata siku ukinikuta nazungumza naye unaweza kusema inawekena na mimi na yeye tumezaliwa tumbo moja," alisema Diamond.


7. NAJ
Penzi lao lilikuwa la siri sana na ni mara moja tu waliwahi kuonekana pamoja, Kaka wa Diamond, RJ The DJ aliwahi kuthitibisha kuwa mdogo wake walikuwa anatoka na Naj, ni kipindi anakaribia kuachia wimbo wake 'Bora Iwe' ambao kamshirikisha Barakah The Prince aliyekuwa na uhusiano na Naj kwa wakati huo.
Pengine Diamond aliamua kufanya siri kutokana Naj aliwahi kuwa mpenzi (ex) wa Mr. Blue kama ilivyo kwa Wema Sepetu, Mr. Blue alisema inabidi amtafute Diamond amueleze kwanini kila mwanamke anayeachana naye anamchukua!.
"Nilijiuliza kitu kwa Diamond, kwanini anafuatilia watu ambao nimepita, mwisho wa siku nikampigia simu Diamond, nilitaka nijue kwanini msichana niliyekuwa naye, huyu wa pili sasa, nilitaka nimuulize," alisema Mr. Blue.


8. ZARI THE BOSSLADY
Hadi sasa hakuna uhusiano wa Diamond uliokuwa na drama nyingi kama huu, Zari alikuwa akipigana vita na timu Wema na timu Hamisa, Diamond alitoka kuachana Wema akatua kwa Zari ambaye amemzaliwa watoto wawili.
Kuachana kwao ni sababu za usaliti, tukio la Diamond kuzaa na Hamisa Mobetto wakati wapo pamoja ni chanzo, ila tukio la kusambaa kwa picha na video za Diamond na Wema wakikumbatiana, ndilo lilimfanya Zari aseme imetosha.
"Nimeamua kusitisha uhusiano wangu na Diamond, tumetengana kama wapenzi lakini si kama wazazi, nitawafundisha wanangu wanne  kuwaheshimu wanawake kila wakati, na kumfundisha binti yangu maana ya kujiheshimu." sehemu ya jumbe wa Zari Februari 2018.
Cha kushangaza ni kwamba Diamond naye alikuja kusema ana uthibitisho wa Zari kumsaliti, alidai Zari aliwahi kuchepuka na mkufunzi wake wa mazoezi pamoja na mwimbaji wa Nigeria, Peter wa kundi la P Square.


9. HAMISA MOBETTO
Licha ya kuonekana pamoja katika kazi, ila mapenzi yao yalikuwa ya siri sana hadi pale Hamisa alipojifungua mtoto wa pili ndipo ikathibitika ni kweli, waliachana baada ya Hamisa kudaiwa kushindwa kutunza siri hiyo wakati anajua Chibu alikuwa na Zari.
"Nilimwambia Hamisa mimi ni Baba mwenye familia yangu, inabidi jambo hili libaki kati yangu mimi na wewe, sikupenda kuikana mimba ni damu yangu na kila siku iendayo kwa Mungu nilikuwa nampatia matumizi," alisema Diamond.
Hata hivyo, Hamisa alisema alikuwa yupo tayari kuwa mke wa pili kwa Diamond kama angemuoa Zari na walishakaa na kujadili hatima ya uhusiano wao wa siri na Chibu alisema dini yake inamruhusu kuoa wanawake wawili.
“Wakati nakutana na Diamond nilijua kuna Zari na nilimuuliza, akasema mimi ni Muislam na uwezo wa kuoa hata wanawake wawili, na mimi nipo tayari hata kama ningekuwa nimeolewa halafu mume wangu anataka kuoa mke wa pili ningemruhusu,” alisema Hamisa.


10. TANASHA DONNA
Tangu Diamond kuachana na Tanasha Donna kutokea Kenya mwanzoni mwa 2022, hajaweka wazi tena uhusiano wake licha ya kuwepo tetesi za kuwa na Zuchu, msanii aliyemsanii WCB Wasafi kipindi kifupi baada ya kuachana Tanasha.
Kwa mujibu wa Tanasha, sababu ya kuachana kwao ni kutokuwa na maelewano mazuri na Mama mzazi wa Diamond, Bi. Sandra maarufu kama Mama Dangote ambaye anadai alikuwa anaingilia sana uhusiano wao na vikwazo vingine.
"Nilihukumiwa sana kwa vitu vingi kwa sababu mimi sio mwanamke mwenye tamaduni za Kitanzania; sibaki nyumbani, kuamka na kupika, ninapenda kupika lakini ikiwa naweza kuajiri mpishi kwanini hivyo?. Nilikumbana na vikwazo vingi, watu wengi hawakuta tuwe pamoja wakiwemo timu yake na familia," alisema Tanasha.
Ikumbukwe hadi wanachana tayari walikuwa wamejaliwa mtoto mmoja ambaye ndio wa mwisho kwa Diamond, huku wakiwa wameshirikiana katika wimbo mmoja 'Gere' kutoka kwenye EP ya Tanasha, DonnaTella EP yenye nyimbo nne alizowashirikisha wasanii wengine kama Mbosso na Khaligraph Jones kutokea Kenya.