ABDUL USANGA: Mtunzi wa Kombolela anayekataa kufananishwa

Muktasari:
- Kombolela inayorushwa na chaneli ya Sinema Zetu katika king’amuzi cha Azam Tv, ilibeba tuzo ya Tamthilia Bora Tanzania kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na waigizaji na utunzi mahiri.
KAMA ni mfuatiliaji wa tamthilia za Kibongo, bila shaka unaijua ‘Kombolela’. Ile inayohusu maisha ya uswahilini. Ile iliyoteka hisia za wengi na zaidi ya hilo, imebeba tuzo katika Tamasha la 28 la Kimataifa la Filamu la Zanzibar (ZIFF) mwaka 2025.
Kombolela inayorushwa na chaneli ya Sinema Zetu katika king’amuzi cha Azam Tv, ilibeba tuzo ya Tamthilia Bora Tanzania kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na waigizaji na utunzi mahiri.
Wengi wanaifuatilia sana lakini hawajui aliye nyuma ya stori hii tamu. Basi kama hujui ni utunzi mahiri wa Abdul Juma Usanga.
Usanga ni kijana mdogo lakini hakuna ubishi anafanya kazi kubwa kwenye sanaa hiyo na amekuwa akitunga tamthilia zake kama ni watu wa kijijini basi kijijini kweli, kama ni wa uswahilini basi uswahilini kweli mwanzo mpaka mwisho na hapo ndipo utamu wa tamthilia zake ulipo. Sasa amekutana na Mwanaspoti na kupiga stori ndani ya dakika 5 kuhusu masuala ya kazi yake ya sanaa.

Mwanaspoti: Kwanza hongera sana kwa kuchukua Tuzo ya Tamthilia bora ya Kombolela mwaka 2025.
Usanga: Asante sana na naimani tuzo nyingi zitakuja kupitia hawa waigizaji wa Tamthilia ya Kombolela.
Mwanaspoti: Ilikuwaje ukapata wazo la Tamthilia ya Kombolela?
Usanga: Hili wazo bana ni tangu mwaka 2015 wakati nipo chuo mwaka wa pili, niliandika Kombolela kama filamu haikuwa Tamthilia, lakini ilikuwa kila nikiiandika siimalizi mwishowe nikaamua kuiweka pembeni, nikaendelea kuandaa tamthilia nyingine Saluni ya Mama Kimbo ndipo baadae ndiyo nikaileta Kombolela.
Mwanaspoti: Una namna ya uandishi wako wa tamthilia mazingira hasa yanakuwa ya vijijini au uswahilini, kwa nini inakuwa hivi?
Usanga: Ok, nafanya hivyo kwa sababu huko ndiko kwenye simulizi nyingi zinazogusa tabaka la chini na la kati, pia watu hao ndio wateja wetu na huwa wanafurahi wakiona unawagusa kwa ukubwa na kwa upana ambao ukiwagusa wanafurahi.”
Mwanaspoti: Unayaonaje mapokezi ya Kombolela?
Usanga: Nafurahishwa sana wadau jinsi walivyoipokea Tamthilia ya Kombolela na kuonyesha ni kweli inasadifu maisha halisi ya baadhi ya familia za Kitanzania Kwa jinsi wanavyoishi.

Mwanaspoti: Hawa waigizaji huwa unawapataje kukamilisha tamthilia yako?
Usanga: Mimi huwa napenda sana kuangalia kazi za wenzangu, hivyo waigizaji wanaoigiza kwenye tamthilia zangu huwa nawatoa kwenye tamthilia za wenzangu na kuja kuwapa vipande vya kuigiza na ndiyo maana unaona mule kuna wasanii wengi wameigiza tamthilia zingine za waandishi wengine.
Mwanaspoti: Katika tamthilia ya Kombolela inaonekana umechukua watu maarufu na wasanii wa muziki kuingia kwenye tamthilia, hii imekaaje?
Usanga: Hakuna namna kwa sasa, huku ndiko kunakolipa. Unajua kwenye tamthilia ni mahali mtu anaweza kuonekana muda mwingi na pengine kwenye muziki kuna foleni kubwa kwa hiyo anataka muendelezo na ndio tasnia inayotoa mastaa wenye muendelezo.”
Mwanaspoti: Ni msanii gani ulipata tabu kumweka kwenye nafasi anayocheza sasa?
Usanga: Hakuna msanii ambaye nilipata tabu kwenye nafasi zao kuwaweka sababu wasanii wote wanaoigiza kwenye tamthilia ya Kombolela wako vizuri sana wanafit na hadi naandaa tamthilia najua kabisa hapa atakuwa nani ana fiti nani hafiti, ila kuna nafasi ya Mzee Kikala hii nafasi nilipata ugumu wa kumwekea plan B, yaani hata kama ingetokea kitu niambiwe nani badala ya Mzee Kikala, basi ningesema hakuna anayeweza fiti nafasi yake, sababu niliona anaiwezea na kuifaa kutoka na umahiri wake wa kuigiza, ukweli anaitendea haki sana.”

Mwanaspoti: Huwa unatumia muda gani kuandika Script?
Usanga: Mimi Kombolela huwa naandika muda wowote tu, nikilala nikiamka naandika yaani kichwani mwangu kuna asilimia 75 ya mawazo yangu ambayo huwa nayatumia kila napoifikiria Kombolela na nafasi ya mhusika ninpoiwaza huwa naandika kwenye simu.
Mwanaspoti: Ni mwandaaji gani wa tamthilia kwa sasa ambaye unamhofia kukuzidi?
Usanga: Hakuna ninayemhofia hata mmoja, sababu mimi sifanani na wao, mimi niko kipeke yangu, hivyo ni tofauti sana iliyopo.

Mwanaspoti: Umeandaa tamthilia ya Mama Kimbo, Kombolela na zahanati ya kijiji, ipi ambayo unaona ni kali sana kwako?
Usanga: Daah hata sijui niseme nini, maana naona zote kali mapokezi ya Mama Kimbo yalikuwa makubwa, lakini ya Kombolela ni makubwa zaidi, nafarijika kuona napata maoni mbalimbali kuwa wanachokiona kinagusa maisha ya watu hata ya Zahanati ya Kijiji nayo ni balaa.
Mwanaspoti: Unapenda nini kwenye Tamthilia ya Kombolela?
Usanga: Mimi napenda kuwatumia wasanii wachanga na ambao hawajawahi kuigiza kabisa sehemu yoyote, ili waje kuungana na wengine wenye uzoefu, ila kubwa zaidi ni kuibua vipaji vipya napenda sana.”
Mwanaspoti: Ilikuwaje Kombolela ikarudi Sehemu ya pili (part 2)?
Usanga: Ukweli ni jambo la kumshukuru Mungu, hii ni kutokana na mashabiki kutaka irudi, maana ‘part one’ ilivyoisha ndiyo inaishia pale stori, lakini vilio vingi vya watu kutaka mwendelezo basi imebidi kuwaletea na inaendelea kama kawaida hadi sasa na yajayo ya furahisha zaidi.