Happy Magese: Wala haikuwa rahisi

Muktasari:
- Magese anaanda shindano hilo kwa mara ya kwanza msimu huu kupitia kampuni ya Millen Preve $ Co. Lifestyle.
UNAMKUMBUKA Happiness Magese, mshindi na Miss Tanzania 2001? Bibie huyu ambaye kwa sasa anafahamika zaidi kwa jina la Millen Magese amefichua namna alivyoulizwa maswali mara baada ya kujitosa kuandaa shindano la urembo nchini la Miss Universe.
Magese anaanda shindano hilo kwa mara ya kwanza msimu huu kupitia kampuni ya Millen Preve $ Co. Lifestyle.
Kisura huyo alisema, wengi walihoji imekuwaje mrembo aliyewahi kutwaa taji la Miss Tanzania aende kuandaa Miss Universe?
“Wengi waliniuliza maswali kwanini umekwenda huko? jibu langu lilikuwa ni jepesi tu, kwamba naangalia urembo kama sehemu ya kum-empower (kumjemgea uwezo) mtoto wa kike na Miss Universe ni jukwaa hilo,” alisema Magese.
Alisema hata yeye na warembo wengine wengi walitumia jukwaa hilo kujengewa uwezo, hivyo kile walichokipitia wao ndicho anahitaji kukifanya kwa wengine.
“Nakumbuka ugumu niliopitia wakati nimeingia kwenye fainali ya Miss Tanzania, ugumu huo ulianzia kwenye familia, mimi hadi naingia fainali nilikuwa navaa kama msomali (kujistri mwili wote).
“Wazazi wangu hawakuelewa, ilikuwa ngumu kuwashawishi hadi kunielewa, mpaka nakuwa Miss Tanzania na kuiwakilisha nchi yangu kwenye Miss World,” alisema Magese akikumbuka tukio la miaka 24 iliyopita alipotawazwa kuwa Miss Tanzania.
Magese aliwakumbuka watu baadhi waliomsapoti na kuwashukuru mmoja mmoja, huku akieleza namna ambavyo hakuwa na mavazi ya kambini, lakini watu hao walimtia nguvu na kumsapoti kwa hali na mali.
“Nilichojifunza wakati ule ni kwamba tunahitaji kuwa-empower watoto wa kike, hicho ndicho kinakwenda kufanyika kwenye shindano la Miss Universe kuanzia mwaka huu,” alisema.
Akizungumzia mchakato na taratibu za shindano la Miss Universe 2025, Magese alisema fainali itakuwa Agosti 23, kwenye ukumbi wa The Super Dome, Dar es Salaam.
Alisema mchakato wa kupata warembo umeanza na utafanyika kwenye mikoa sita ya Arusha, Mwanza, Mbeya, Dodoma, Zanzibar na Dar es Salaam na Agosti 6 itakuwa ni siku ya mchujo ili kupata warembo 15 watakaoingia kwenye fainali,” alisema.
Akielezea vigezo vya kushiriki, Magese alisema binti yoyote kuanzia miaka 18 na kuendelea mwenye sifa za u-miss ni fursa kwake kujitokeza.
“Miss Univerese haiangalii umri wako, kama una miaka 18 na kuendelea bila kujali umewahi kuzaa au kushiriki na hata kushinda taji jingine la urembo huko kwingineko, hii ni fursa kujitokeza,” amesema
Alisema katika shindano la mwaka huu, kama waandaaji wameboresha zaidi na hakutakuwa na vazi la ufukweni kwa warembo.
Mbali na urembo, Magese alisema washiriki watakaoingia kambini kwa siku 21 pia watafundishwa mambo mbalimbali ya maendeleo, ujasiriamali na uchumi ambayo yataendelea kuwajengea uwezo hata baada ya shindano hilo.
Katika uzinduzi wa msimu mpya wa shindano hilo ulioongozwa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Dk Kedmon Mapana, mtendaji huyo alieleza namna ambavyo Baraza lima matarajio makubwa na waandaji kulifikisha shindano la Miss Universe kwenye kilele cha mafanikio.
Alisema muandaaji Happiness ana historia na mashindano ya urembo, anajua nini afanye ili lizidi kuwa bora na kuwasihi wadau kuendelea kumsapoti katika kila hatua.
Awali katika hafla ya uzinduzi huo iliyohudhuriwa na wadau mbalimbali ikiwamo warembo wa Miss Universe wa misimu tofauti na wale waliowahi kushiriki Miss Tanzania, washiriki walisimama kwa dakika kadhaa kumuombea aliyekuwa mwanzilishi wa Miss Tanzania, Hashim Lundenga aliyefariki miezi kadhaa iliyopita.