Walibamba na kuyeyuka

LADY Jaydee ndiye gwiji wa Bongofleva kwa upande wa kinadada. Ana miaka 21 katika hii gemu tangu alipoachia wimbo wake wa Machozi mwaka 2000.

Amewezaje kudumu katika gemu kwa miaka yote hiyo wakati kuna wasanii wa kike kibao ambao walimkuta akiwa juu na wamefutika akiwa juu? Hili ni swali ambalo ni yeye tu analo jibu lake.

Hawa hapa ni watoto wazuri wa Bongofleva ambao walitamba kisha wakatoweka.


DATAZ

Kibao cha Wajua kilichoimbwa na Dataz akimshirikisha kaka yake Squeezer kilikuwa moto.

Dada huyu alijua kuburudisha watu na alikuja kuwamaliza zaidi mwaka 2012 alipotoka na wimbo wa ‘Mume wa Mtu’, aliomshirikisha msanii Joan.

Tangu alipoachia wimbo huu Dataz akapotea kwenye ramani ya muziki, na sasa ni mfanyakazi wa benki moja kubwa nchini.


PAULINE ZONGO

Pauline Zongo, dada mwenye sauti yake. Huyu alikuwa First Lady katika kundi la muziki wa Bongofleva la East Coast Team.

Kundi hili lilikuwa limesheheni wasanii wakali akiwamo AY, Mwana FA, King Crazy GK, O-Ten na alishiriki katika kuimba nyimbo mbalimbali ikwemo Itikadi.

Msanii huyu alishirikishwa na King Crazy GK katika vibao mbalimbali ikiwemo Nitakufaje, Kosa Langu, Desire na Sister Sister.

Ni kutokana na kipaji chake hicho, bendi ya Tanzania One Theatre (TOT), ilimchukua na kumpa cheo cha kuongoza bendi hiyo.

Akiwa huko alishiriki kuimba nyimbo mbalimbali ikiwemo ya ‘Mnyonge Mnyongeni,’ alichokiimba kwa kushirikiana na kina Badi Bakule na Abdul Misambano.

Hata hivyo, haikueleweka mkataba wake na bendi hiyo uliishaje mpaka pale alipoibuka mwaka 2018 akiwa anahojiwa katika kipindi cha Heshima ya Bongofleva na kueleza kuwa amedhamiria kurudi mchezoni.

Sasa ni mwaka wa tatu kimya tangu Pauline asikike akitoa ahadi hiyo. Pauline mbali ya kuwa mwimbaji ni mtunzi wa nyimbo, pia ni mpiga vyombo vya muziki mzuri ikiwamo gitaa, kinanda na ngoma.


MAUNDA

Maunda Zorro, ni msichana anayetokea kwenye familia ya wanamuziki. Baba yake Zahir Ali Zorro na kaka yake Banana Zorro ni moja ya chachu iliyomsukuma kuingia kwenye muziki.

Enzi zake aliwahi kutesa na vibao mbalimbali ikiwemo ‘Nataka Niwe Wako’ alioutoa mwaka 2008, ukifuatiwa na ‘Mapenzi ya Wawili’ uliotoka mwaka 2009 vibao ambavyo vyote vilifanya vizuri.

Pia msanii huyo alishirikishwa na wasanii mbalimbali akiwemo K-One kwenye Yule, Squeezer kwenye wimbo wa My Wife, Hussein Machozi kwenye Hello na Nay wa Mitego kwenye Talaka.


BESTA

Imepita miaka 14 sasa tangu alipoachia kibao cha ‘Kati Yetu’. Kibao hiki kilikuwa moto wa kuotea mbali hasa msanii huyo alivyochangamka kucheza.

Mdundo wa ‘dancehall’ wa wimbo uliotoka mwaka 2007 ulimfanya Besta aunogeshe kwa mauno ya kufa mtu na kuufanya kuzidi kupendwa.

Hata hivyo, mwaka 2011 Besta alifunga ndoa na msanii mwenzie Marlaw na kuanzia hapo hakuwa akionekana tena kwenye majukwaa ya muziki.

Hadi kufika mwaka 2016, Marlow na Besta walikuwa tayari wamejaaliwa kupata watoto watatu.


RAH P

Huyu naye alivuma kipindi cha kina Besta, akitamba katika muziki wa kufokafoka.

Kibao chake cha ‘Hayakuhusu’ kiliteka macho na masikio ya watu, ukizingatia kuwa ndio usemi ulikuwa ukitamba wakati ule.

Pia kabla ya hapo alishatoa wimbo wa Malkia uliokuwa ukizungumzia mateso mbalimbali anayopitia mwanamke.

Hata hivyo, Rah P alipotea ghafla kwenye gemu, akaja kusimulia alivyoenda Marekani ambako alizaa watoto wawili na mwanaume ambaye alikamatwa kwa dawa za kulevya na kumuacha yeye akiteseka na malezi na akaishia kuwa mlevi na hadi naye kutupwa jela pia.


SISTER P

Ni kati ya wasanii waliokuwa na ushindani kwa watoto wa kike kipindi hicho. Sister P alikuwa akishindanishwa sana na Zay B.

Enzi zake alitesa na vibao mbalimbali ikwemo ‘Achana Nao’ aliouimba na msanii wa muziki wa dansi, Ali Choki.

Nyimbo nyingine ni Hey DJ, Nani Mkali alioimba na Nay wa Mitego.


ZAY B

Kibao cha Niko Gado alichoimba na Inspekta Haroun ndicho kilichompa umaarufu msanii huyu na baadaye kuachia vibao vingine kama Monica, Penzi la Teja alioimba na Rahima wa kundi la Unique Sisters pamoja na Haina Shobo.


HAFSA KAZINJA

Miaka 13 wimbo wa ‘Pressure’ ft Banana Zoro ulikuwa ni kama wimbo wa taifa. Ulifunika kila kona.

Na hata sasa katika YouTube una watazamaji zaidi ya milioni moja.

Hafsa sasa anaimba nyimbo za Injili ukiwemo Wewe ni Mfalme.