P Diddy asikilizia hukumu, akutwa na makosa mawili

Muktasari:
- Mwanamuziki huyo wa hip hop amesomewa uamuzi jioni hii, huku akifanikiwa kupangua mashtaka matatu kati ya matano yaliyokuwa yanamkabili.
NEW YORK, MAREKANI: WAKATI jopo la majaji wa Mahakama ya Shirikisho New York, Marekani, likitumia saa 13 ndani ya siku tatu kujadiliana kutoa hukumu kwa Sean Combs 'P Diddy', limemtia hatiani kwa makosa mawili kati ya matano.
Mwanamuziki huyo wa hip hop amesomewa uamuzi jioni hii, huku akifanikiwa kupangua mashtaka matatu kati ya matano yaliyokuwa yanamkabili.
Mapema leo asubuhi alisomewa maelezo ya mwenendo wa majadiliano wa majaji ambao hata hivyo hawakueleza kilichokuwa kimefikiwa isipokuwa walikuwa wamekubaliana katika makosa manne kati ya matano.
Hata hivyo, baada ya mapumziko jioni Diddy alisomewa uamuzi akitiwa hatiani katika makosa mawili - uhalifu wa kupanga na usafirishaji wa binadamu kwa ajili ya biashara ya ngono.
Adhabu ya makosa hayo inaweza kuwa Kifungo cha miaka 10 gerezani.
Katika uamuzi wao majaji wamesema wamemtia hatiani mwanamuziki huyo kwa kutenda kosa la usafirishaji wa wanawake kwa ajili ya ukahaba waliotajwa kwa majina ya Cassie Ventura na Jane.
Siku chache zilizopita wanawake hao ambao waliwahi kuwa wapenzi wa Diddy, walitoa ushahidi mahakamani kuhusiana na matukio yaliyotajwa, ambapo kipindi hicho walikuwa wakipewa wanaume waliolipwa ili kufanya nao ngono, huku Diddy akiwatazama na wakati mwingine akirekodi au kuwaelekeza nini wafanye.
Hukumu hiyo inaonekana kuwa ni ushindi kwa Diddy na timu yake, kwani makosa ya usafirishaji wa binadamu kwa ajili ya ukahaba yana adhabu ndogo ikilinganishwa na yale matatu aliyokuwa akikabiliwa nayo awali ambayo iwapo angepatikana na hatia kwayo angefungwa maisha.
Wakati akisomewa maelezo hayo Diddy alikuwa mtulivu na kabla ya hapo alikuwa alisali na watoto wake na kuwakumbatia mawakili waliokuwa wakimtetea.
Kabla kusomewa maelezo hayo jioni, majaji walitoa maelekezo kwa watu waliokuwa ndani ya mahakama kuwa watulivu.
Hata hivyo, chumba kingine ambacho kilikuwa na waandishi wa habari na wafuasi wa Diddy kililipuka kwa kelele kila hukumu iliposomwa.
Pia wafuasi wake waliokuwa nje ya mahakama walisikia wakishangilia.
Ingawa Diddy amepatikana na hatia ya makosa hayo, bado hajajua ni kifungo cha muda gani atapewa japokuwa adhabu ya juu kabisa ni miaka 10 gerezani. Hukumu hiyo itatolewa siku yoyote.
Mwendesha mashtaka wa Shirikisho la Marekani, Maurene Comey amesema anatarajia kupendekeza mwanamuziki huyo apewe kifungo cha miaka 20 gerezani akisema, “ni wazi kwamba mshtakiwa ni mtu hatari.”
Haijajulikana kama ataendelea kubaki gerezani hadi wakati wa hukumu, lakini upande wa mashtaka umeomba aendelee kushikiliwa mahabusu wakati mawakili wake wakitaka aachiwe kwa dhamana.
Kwa sasa upande wa utetezi unapambana ili mwanamuziki huyo aachiwe, na mmoja wa majaji anasikiliza hoja kutoka kwa mawakili wa pande zote ambapo wakili wake, Marc Agnifilo amependekeza apewe dhamana kwa kutoa Dola 1 milioni.
Diddy amekuwa rumande tangu alipokamatwa Septemba, mwaka jana.