Wadau wapishana kumuunga au kutomuunga mkono Diamond, tuzo za BET

Thursday June 03 2021
diamond pic
By Mwandishi Wetu

Dar es Salaam. Pamoja na wasanii kumuunga mkono msanii mwenzao Diamond Platnumz katika kile kinachoendelea kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kumpigia kura katika tuzo za BET alizochaguliwa kushiriki, baadhi ya wadau wanaona hastahili kuungwa mkono.

Wadau hao wamemkemea waziwazi kupitia mitandao ya kijamii wakidai kuwa hajalitumia vema jina lake la msanii mkubwa kukemea maovu, badala yake amekuwa akifanya mambo yake binafsi.

Baadhi ya wachangiaji suala hilo katika mtandao wa Twitter wamekwenda mbali zaidi kwa kudai kuwa watawaunga mkono wasanii wa Nigeria anaoshindana nao kuwania tuzo hiyo katika kipengele cha ‘Best International Act’ wakiwamo  Wizkid, Burna Boy, Emicida, Headie, Aya Nakamura, Youssoupha na Young T & Bugsey.

Hata hivyo  mshindi wa tuzo hizo  anachaguliwa na jopo la majaji 500 wa BET na hapatikani kwa kupigiwa kura.

Baadhi ya wasanii wamemuunga mkono wakitaka apigiwe kura, huku wengine wakimkumbusha ajiulize kwa nini watu wanahamasishana kutompigia kura (ingawa hakuna kura zitakazopigwa kutoka kwa wananchi katika tuzo hii).

Mwimbaji Ray C amemtaka Diamond kujiuliza kwa nini wakati huu wa tuzo za BET ndio mambo hayo yanatokea na sio kipindi cha nyuma ambapo ameshinda tuzo nyingi kubwa.

Advertisement

Ray C alidai kipindi cha katikati Diamond alikuwa msanii mwenye majivuno sana na kubeza wenzake, pia kitendo chake cha kucheka hadharani mara baada ya kuahirishwa tamasha la Fiesta Novemba 2018 ambalo linawahusisha wasanii wengine, ndipo alipotengeneza huo mpasuko unaonekana kwa sasa.

"Yanayoendelea mitandaoni hasa Twitter nadhani hata wewe (Diamond) huelewi mbona watu wameanza kubadilika ghafla wakati miaka kama mitano nyuma watu tulikuwa hatusikii wala hatuambiwi kitu kuhusu wewe, nadhani hapo katikati ulikuwa unatuchamba sana kama una fedha nyingi au zile ‘Interview’ za madongo unadai kusanya wasanii wote Tanzania wafanye shoo na mimi nifanye shoo tuone nani atajaza? Aliandika Ray C.

"Kuna muda unakaa unajiuliza huyu dogo mbona hivi tena, vichambo vyako vingi vimewagawanya mashabiki, huo ni ukweli. Tafadhali kuwa mpole sasa, na pia punguza machawa wa ajabu wanaropoka sana wanakera. Anza kufanya makolabo pia na wenzio hapo Bongo na simaanishi wasanii wa WCB tu, bali wengine ambao wanapambana na wanafanya vizuri kwenye game, washike mkono wenzio," ameandika Ray C anayeishi Ufaransa kwa sasa.

Kwa upande wa mtayarishaji muziki wa siku nyingi Joseph Kimario, maarufu  'Master Jay' amesema watu wanapaswa kujua wakati gani wanapaswa kufanya nini na wakati upi wanapaswa kuacha kufanya kitu gani.

Amesema kinachoendelea mitandaoni kuhusu Diamond na tuzo za BET ni umasikini wa fikra.

“Mkiwa wanafamilia mnaishi katika nyumba moja, baba na mama lazima wagombane au walumbane kwa sababu ni binadamu, lakini wanapotoka nje wanakuwa kitu kimoja, wakirudi ndani wanaendelea na malumbano yao, hapa wanaangalia ni wakati gani na wanapaswa kufanya nini,’ amesema na kufafanua.

“Inawezekana Diamond kuna mambo alifanya hayako sawa na aliwaudhi Watanzania, lakini huu siyo wakati wa kuyasema tena kwa kutangaza kuwaunga mkono watu wengine, badala yake ni kuficha aibu zetu kwa kukaa kimya kama hutaki kumuunga mkono, akirudi ama na tuzo au laa ndipo useme unachofikiria, lakini muhimu kwa sasa ni kuwa kitu kimoja kama Taifa,” ameandika na kuongeza.

“Diamond, haendi kuwania tuzo hiyo kama mwanaume, Mwislamu, Mkristo, mwanachama wa chama fulani, anayejidai, kujisikia na asiyesaidia jamii, anakwenda kuwakilisha nchi, hivyo ni wajibu wa Watanzania kumuunga mkono,”ameandika.

Ameandika kuwa kinachofanyika sasa na wanaompinga ni kuididimiza nyumba wanayoishi “Ni sawa na kunywa sumu ili afe mtoto wa jirani uliyegombana naye, tunajiua wenyewe.

Master J ameandika kuwa kwake Diamond kuchaguliwa tu kuwania tuzo hizo kubwa ni heshima kwa nchi, bila kujali ameshinda au laa kwa sababu majina ya wasanii yanapita katika mchujo mkali kabla ya kutangazwa.

Hata hivyo Rapa Wakazi amesema kufanya hivyo si kumkomoa Diamond, bali ni kuinyima fursa Tanzania, hivyo kuwataka wadau na mashabiki kuweka itikadi zao pembeni.

"Ukisema kisa aliunga mkono CCM, unakuwa huna tofauti na ambao wanamnyima fursa Wakazi, Jhikoman, Vitali Maembe na  Baba Levo kisa nao walikuwa Upinzani. Basi ningewaona bora zaidi kama mtatusapoti sisi tuinuke, na sio kutumia nguvu kumshusha mwingine, hata kama yeye kaongea mbovu ni sawa kama humsapot ila kufanya kampeni kabisa waziwazi sio vizuri," alisema Wakazi.

Kwa upande wake Professa Jay amesema ni vizuri wasanii, mashabiki na wadau kuiga mfano wa Nigeria ambao linapokuja suala la tuzo za wasanii wao, wanaungana na kuwa kitu kimoja kuhakikisha ushindi unakuja nyumbani.

"Anaposimama Mtanzania yeyote kugombea tuzo jambo lolote duniani ni lazima tusimame naye pamoja bila kujali makundi, itikadi, dini wala makabila yetu maana hapo inasimama Tanzania na sio mtu mmoja mmoja," amesema Professa Jay.

Irene Paul

Kupitia ukurasa wake wa Instagram ameandika “Ifike mahali tuthamini juhudi za mtu binafsi katika kuleta heshima kwa Taifa letu na tuache mengine yote pembeni.

 “Pamoja na mengine yote yanayoendelea, wengi watafuata lakini ni baada ya yeye kuchora ramani ya jinsi inavyofanyika. Ninatamani tumpigie kura kwanza huko kwa BET halafu turudi nyumbani tuongee tunayojisikia maana mwisho wa siku tumeshatambulika zaidi na kujulikana kama Tanzania,”ameandika mwigizaji huyo.

Batuli

Mwigizaji wa filamu Nobesh Yusufu, maarufu ‘Batuli’, ameandika “Siyo tuzo yake ni tuzo yetu, sio nchi yake peke yake ni nchi yetu sote, kama tulivyoweza kujifunza chuki, tunaweza pia kujifunza upendo walau wa muda mfupi, umoja ni nguvu, tumpigie kura aliyechaguliwa kuipeperusha bendera ya Tanzania, tumpe furaha na zawadi hii Rais wetu wa kwanza mwanamke Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Fred Vunjabei

Mfanyabiashara maarufu, Fred Vunjabei aliandika “Unakuwa mzalendo kama mapigo ya moyo wako yanaelekea kwenye Taifa lako, ndugu zangu wafanyabiashara tumuunge mkono mfanyabiashara na Mtanzania mwenzetu, A True African Giant is Diamond Platnumz.”

Kwa mara ya kwanza Diamond kuwania tuzo hizo ilikuwa 2014 na kuwa msanii wa kwanza Tanzania kufikia hatua hiyo, ambapo aliwania kipengele cha ‘Best International Act Africa’ akishindana na Mafikizolo, Sarkodie, Tiwa Savage na Davido aliyetangazwa mshindi.

Mwaka 2016 akawania  kipengele hicho hicho akishindana na  Wizkid, Yemi Alade, AKA, Cassper Nyovest na Black Coffee aliyeshinda.

Tuzo za BET zilianzishwa Juni 19, 2001 na kituo cha TV cha Black Entertainment Television, lengo ni kusherehekea mafanikio ya kazi za Wamarekani weusi katika burudani ikijumuisha muziki, uigizaji na michezo.

Imeandikwa na Peter Akaro, Mwananchi

Advertisement