Vya Kale Dhahabu in Dar Hadija Kopa naye yumo

Vya Kale Dhahabu in Dar Hadija Kopa naye yumo

Dar es Salaam. Wanamuziki wa taarabu, Afua Suleiman, Patricia Hillary na  Hadija Kopa ni moja ya wasanii watakaotumbuiza katika tamasaha la muziki wa taarabu la 'Vya Kale Dhahabu' litakalofanyika Disemba 10, 2021 ukumbi wa Mlimani City  jijini Dar es Salaam.

Hayo yamesema leo Jumatatu Novemba 8, 2021 na Mkurugenzi wa kampuni ya Chocolate Princes, Mboni Masimba katika mkutano na waandishi wa habari.

Mboni amesema wasanii hao ni kati ya watakaopamba tamasha hilo ikiwa ni shamrashamra kusheherekea miaka 60 ya uhuru na pia kuanzia sasa litakuwa likifanyika kila mwaka ifikapo Disemba.

Wasanii wengine aliwataja kuwa ni Mwanamtama, Abdul Misambano na Ally Star.

"Usiku huo wa Vya Kale Dhahabu pia tutautumia katika kuwaenzi wasanii wetu wa muziki huu waliotangulia mbele ya haki akiwemo Bi kidude, Issa Matona, Shakira, Bi Leila na wengine" amesema Mboni.

Aidha amesema siku hiyo kutakuwa na vyakula mbalimbali vitakavyopatikana kwa watu wa Pwani ikiwemo urojo na supu ya pweza, huku mavazi kwa wanaume yakiwa ni kanzu na koti au msuli na kwa wanawake nguo za lesi na viatu virefu huku kiingilio kikiwa ni  sh500,00.

Kwa upande wake Hadija Kopa, amesema siku hiyo watu watarajie kusikia nyimbo zake ambazo aliwahi  kuimba  wakati akiwa Zanzibar ikiwemo Gwinji, Daktari na nyinginezo.

Wakati Afua Suleiman amesema ni siku ambayo atawaonyesha watu kwamba bado yupo licha ya kupotea siku nyingi kwenye tasnia hiyo kwa kutoonekana kwenye majukwaa ya burudani.