VIDEO: Steve Nyerere abwaga manyanga, atoa sababu

Dar es Salaam. Msanii wa filamu, Steven Mengere maarufu Steve Nyerere amejiuzulu nafasi ya usemaji wa Shirikisho la Muziki Tanzania (SMT).
Steve Nyerere ametangaza hilo leo Ijumaa Machi 25, 2022 kwenye mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) jijini humo.
Amesema amefanya hivyo kwa lengo la kuepuka kuwagawa wasanii ambao tayari wengine wameonyesha kutomkubali na wengine kumkubali.
"Sipo tayari kuongoza watu ambao wamegawanyika, kwani malengo yangu ilikuwa kuwaunganisha wasanii na kuwa daraja,"
"Nikiwa na akili timamu nimejiuzulu nafasi hii, ila nitakuwa tayari kushirikiana na wasanii pale watakaponihitaji," amesema Steve
Katika sakata hilo, waliokuwa wanamkubali walikuwa wasanii wa muziki wa dansi, taarabu na injili, huku baadhi wa kizazi kipya wakimkataa.
Kutokana na mgogoro huo, juzi Machi 23, 2022 Basata iliingilia kati na kusitisha Steve kuendelea na kazi hiyo mpaka hapo itakapopitia hoja za pande mbili na kuja na tamko lao.
Kabla hawajatoa majibu hayo, ndio leo msanii huyo kaamua kutangaza kujiuzulu kwa kuitisha mkutano wa waandishi wa habari.