VIDEO: Siri ya baba mzazi wa Diamond hii hapa

Saturday January 16 2021
diamondpic

Dar es Salaam. Mama mzazi wa msanii wa muziki wa Bongo fleva, Diamond Platnumz, Sanura Kassim, maarufu mama Dangote, ametoa taarifa ya kutikisa mitandao ya kijamii jana kwamba aliyekuwa anafahamika kuwa baba mzazi wa msanii huyo si baba mzazi, bali ni baba mlezi.

Ilikuwa inafahamika na wengi kwamba baba mzazi wa Diamond, ni mzee anayefahamika kwa jina la Abdul Jumaa Issack na ndiyo maana majina halisi ya msanii huyo ni Nasseb Abdul Jumaa.

Lakini jana, mama huyo alisema baba mzazi wa msanii huyo ni Salum Iddy Nyange ambaye ni marehemu.

Awali akizungumza na mtangazaji wa kipindi cha Mashamsham kinachorushwa na redio ya Wasafi, mchambuzi wa masuala ya michezo, Mohamed Nyange au ‘Ricardo Momo’ alieleza kuhusu uhusiano kati yake na Diamond kwamba baba yao ni mmoja na alitambulishwa na baba yake mwaka 1999 wakati huo Diamond akiwa na umri wa miaka 10 .

Mama Diamond alisema Mzee Abdul alimkuta akiwa na ujauzito wa Diamond, alivyomueleza ni mimba yake alikataa.

“Yeye mwenyewe anajua, alikataa mimba akanambia mimba sio yangu. Na hilo ndio kosa lake, ndiyo tunachosema kila siku. Kama angekubali mimba tangu ikiwa ndogo, mtoto angekuwa ni wake. Na tena hajamsaidia Naseeb chochote, kuanzia shule vidudu mpaka sekondari.” alisema.

Advertisement

Mzee Abdul anasemaje?

Kutokana na kauli hiyo, Mwananchi ilimtafuta mzee Abdul ambaye alisema amefurahi kusikia hilo kutoka kwa mhusika ( mama wa Diamond) kwa sababu yeye mwenyewe alikuwa haelewi kitu.

“Kwa kuwa mhusika kashaongea hivyo sawasawa kabisa,”alisema.

Alipoulizwa kwa nini zamani aliwahi kuulizwa suala hilo lakini akakataa, alijibu “Si mmeshapata jibu kwa mwenyewe mnataka mimi niseme nini tena, wakati yeye ndio aliyebeba mimba.

“Tunajua wanawake wengi kwa sasa wana makadi ya kliniki hadi matatu au manne kila moja na baba yake, huku wakiangalia mwanaume mwenye maslahi, lakini huyu kafunguka kuwa mimi si baba halisi wa Diamond mnataka ning’ang’anie ilihali sikubeba mimba?” alihoji.

Pia alisema hata yeye anakubali Diamond si mtoto wake, ingawa amelijua hilo baada ya mama yake kulizungumza na kuongeza kuwa sasa ndio anapata majibu kwa nini kijana huyo alikuwa hamhudumii na kwamba amekubali matokeo.

“Yule mtoto nimembeba tangu anatoka hospitali, tukamlea na tukagombana alipokuwa kidato cha kwanza,”alisema.

Alieleza kuwa hana shida ya kuhudumiwa na Diamond wala kuwa mwanawe, amekubali alichokisikia na kukisoma mitandaoni.

Hivyo, mzee Abdul ametaka msanii huyo kuanzia sasa asitumie jina lake na yeye watu wasimtambue kama mzee Abdul Platnumz na badala yake aitwe mzee Abdul peke yake.

Alisema endapo Diamond ataendelea kutumia jina la Abdul atamshtaki kwenye vyombo vya sheria.

“Nashukuru kama baba mlezi nimepata thawabu kwa kumlea mtoto huyo, japokuwa nilikuwa nikijiuliza kwa nini kwa muda mrefu nikiomba kitu kwa mtoto hanipi, lakini sasa majibu nimeyapata,” alisema. Aliongeza kuwa kauli ya mama Diamond imewapa faida Watanzania waliokuwa wakimuona amepigwa picha akiwa amebeba mizigo na kupanda daladala.

Hata hivyo, alisema mama Diamond amekosea kumwambia mtoto huyo kuwa yeye sio baba yake kwa sasa wakati akiwa na kipato.

“Na mimi leo nazungumza mbele ya umati wa Watanzania kuwa Diamond sio mtoto wangu wabaki na mama yake na maisha yao na ninawatakia kila la heri,” alisema.

Alipoulizwa kuwa hana mpango wa kupima vinasaba kuthibitisha kama msanii huyo ni mtoto wake au la, alisema anachoamaini mtoto hagombaniwi kama ilivyo mpaka wa nyumba, hivyo anamwachia Mungu kwa kuwa kisichokuwa riziki hakiliki na kuongeza kuwa yote hayo ni kwa sababu ya mali.

“Nina imani kama asingekuwa na kitu asingeongea hayo na pia angepaswa kuzungumza mambo hayo kifamilia, lakini sio kwenye vyombo vya habari, kwani kwa alichokifanya amenivunjia heshima,” alieleza.

Licha ya kwamba Waswahili wanasema mama ndiye anayefahamu baba wa mtoto, bado taarifa aliyoitoa mama Dangote imeacha mijadala mingi kwenye mitandao ya kijamii.Baadhi ya maswali yanayohojiwa ni kama kweli mzee huyo alimkataa Diamond, kwa nini alimpa jina la baba mlezi, pia kwa nini Diamond hata baada ya kukua alikubali kutumia jina la mzee huyo badala ya la Nyange ambalo mama yake amethibitisha kuwa ndiye baba yake? Hata hivyo, majibu ya maswali hayakupata majibu kwani alipotafutwa Mama Dangote, Diamond wote hawakupatikana.

Imeandikwa Nasra Abdallah na Kelvin Kagambo

Advertisement