TUONGEKISHKAJI: Msilalamike kuhusu Grammy, Afrika haina nchi tatu

TUZO za Grammy zilitolewa majuzi na katika kipengele cha Msanii Bora Afrika alishinda Tyla Laura Seethal maarufu Tyla kutoka Afrika Kusini na wimbo wake wa Water.

Na kama kawaida, ushindi wa Tyla ulikuwa ni gia ya masimango kwa wasanii wa Bongo. Watu wakasema, “wasanii wetu wanaimba chapati wanategemea kushinda Grammy† huku wengine wakisema “nyimbo za kushinda Grammy tunazitoa wapi? Nd’o hizi matikiti kudondoka, matikiti kudondokea?â€

Maneno yalikuwa mengi unaweza kudhani kwamba kwenye kipengele hicho kuna msanii wa Tanzania alikuwa amechaguliwa kuwania tuzo, wakati kiuhalisia hakuwepo hata mmoja.

Kipengele hicho kilikuwa na wasanii watano Ayra Starr, Asake, Burna Boy, Olamide ambao wote wanatokea Nigeria halafu nafasi moja iliyobaki ambayo amekaa Tyla ndiyo ilikuwa ya msanii wa nje ya Nigeria. Hii inatoa picha kwamba kama huu ulikuwa msiba basi haukuwa  wa Tanzania pekee, ulikuwa wa Afrika nzima. Bara la Afrika lina nchi 54 na zote zimejaa wasanii wanaofanya muziki kwa kiwango sawa au cha kukaribiana na wale wa Nigeria.  Kwa hiyo inashangaza kuona tuzo ya kimataifa kwa ajili ya wasanii wa Afrika ina wasanii wanne kutoka taifa moja. Sitaki kusema chochote kuhusu tetesi za kwamba Wanaijeria wana kawaida ya kupita milango ya nyuma yanapokuja masuala ya kupambania ‘platform’ kubwa kama hizo. Na sitaki kusema chochote kwa sababu sina ushahidi. Hizo ni stori ambazo mimi na washkaji huwa tunapiga tukiwa maskani, lakini kisemwacho  pengine kina ukweli.

Nachotaka kusema ni kwamba tusiwalaumu sana wasanii wetu. Wanafanya makubwa kwa kweli. Ukitaja mataifa matano  yanayofanya vizuri katika muziki Afrika ni lazima uitaje Tanzania. Hiyo ni kwamba kama Grammy wangekata kuwa na mchanganyiko, basi kungekuwa na nafasi kubwa zaidi kwa wasanii wa Tanzania.

Tatizo ni kwamba, Wanaijeria walishajisukuma sana nje ya mipaka ya nchi yao kiasi kwamba inakuwa ngumu kuwakimbiza. Wanaijeria wamejitangaza sana kwenye sanaa kiasi kwamba kila kitu kinachohusiana na biashara ya muziki na filamu kutoka nje ya Afrika lazima kianzie Nigeria.

Pia, Wanaijeria wanakwenda kama Wavietanamu kwenye muvi za zamani za kivita. Wanakwenda wengiwengi. Wana wasanii zaidi ya 10 ambao wana hadhi ya kufanya muziki kimataifa wakati sisi  tuna msanii mmoja, Diamond kwa miaka karibu 10 na imeshindikana kupata mwingine wa hadhi hiyo. Na hata Diamond mwenyewe ameshindwa kutengeneza wasanii wengine wa hadhi hiyo. Tazama wasanii wake wengi wanakuwa wakubwa na kufanya vizuri ndani ya nchi, lakini linapokuja suala la kuvuka mipaka wanaishia Kenya, DR Congo, Uganda na Rwanda. Zuchu bado hana hadhi ya kushindana Ayra Starr na Tyla wakati ukiniuliza mimi linapokuja suala la uandishi na uimbaji, Zuchu ni msanii mzuri kuwazidi niliowataja.

Kwa hiyo, tusiwaseme sana wasanii wetu kutokuwepo kwenye Grammy. Afrika ina nchi zaidi ya 54, tuwauleze Grammy walifikiaje uamuzi wa kuamua kuwa na wasanii wanne kutoka taifa moja la Afrika.