KALALA JR: Uwoya, Dogo janja sihusiki... Papii Kocha freshi tu
Muktasari:
- Kalala anamshukuru Mungu kwa mafanikio aliyoyapata akiwa na bendi yake ya Tukuyu Sound na ni moja ya bendi zinazozungumziwa nchini.
NI moja ya majina makubwa kwenye muziki wa dansi. Hakuna ubishi kazi anazozifanya kwenye muziki huo ni maisha yake. Anaishi muziki na anapenda muziki na mwenyewe anasema, sio juzi, tangu akiwa mtoto mdogo alikuwa anaupenda.
Kalala anamshukuru Mungu kwa mafanikio aliyoyapata akiwa na bendi yake ya Tukuyu Sound na ni moja ya bendi zinazozungumziwa nchini.
Anasema baada ya kuondoka Twanga Pepeta mwanzoni mwa mwaka 2021 na alianzisha bendi hiyo Februari 1, 2021 na kusajiliwa Rasmi Februari 18 mwaka huo huo, akiwa na mwanamuziki mwenzake, Papii Kocha na alipewa miezi mitatu na watu kuwa bendi hiyo itakufa kwani hana uwezo wa kuwa mkurugenzi wa bendi na sasa ndiye mkurugenzi wake na inaendelea kufanya vizuri.
Anaamini muziki wa dansi ni bora kuliko mwingine kwa sababu wanamuziki wake wana nidhamu ya hali ya juu jambo ambalo wanalifanya na hasa wakijua muziki ni kazi na sehemu ya maisha yao.
Kwa miaka takribani 13 amekuwa akiajiriwa kufanya kazi na bendi tofauti nchini. Nini kipo nyuma yake kuweza kumiliki bendi hiyo na nini matarajio yake? Mwanaspoti lilifanya naye mahojiano na hapa anafunguka mengi kuhusu bendi hiyo na muziki wa dansi kwa jumla.
Amewezaje kuiendesha?
Kalala Jr: “Nilipotoka Twanga Pepeta na kuanzisha bendi hii ya Tukuyu Sound Band, ilipewa miezi mitatu itakuwa imekufa. Lakini huu ni mwaka wa tatu sasa na sherehe tumefanya ya kutimiza miaka mitatu ya bendi pale Break Point Makumbusho na wewe ndugu yangu mwandishi ulihudhuria na kujionea ukomavu wangu wa kuendesha bendi.”
Matarajio ni yapi?
Kalala Jr: Nia yetu ni kurudisha muziki wa dansi kwenye hadhi yake. Hivyo, namna ya kuongoza bendi na wanamuziki, kunategemeana na uwezo wa kifedha na akili pia, nasema hivyo kwa sababu muziki wetu umekuwa ukiyumba mara kadhaa kutokana na baadhi ya mameneja kuwa wasimamizi wabovu na wengine wanasimamia wakiwa hawana fedha ya kuwaongoza wasanii.
Japo wapo mameneja wanaonyesha njia kubwa ya kuimarisha muziki wa dansi na sasa umeanza kuwa juu kiasi cha watu kuanza kuupenda tofauti na kipindi cha nyuma ulianza kupoteza dira.
Kwa nini alitoka Twanga Pepeta?
Kalala Jr: Huwa sipendi kusema au kuongelea hiki kitu, mimi sikupenda kutoka Twanga Pepeta, ila ilinilazimu kutoka sababu kuna mambo tulishindwa kuelewana, ndio ikawa hivyo tena na kuamua kuanzisha Tukuyu Sound.
Kuna ugumu gani kuiendesha Tukuyu Sound?
Kalala Jr: Tabia za wanamuziki kiukweli hazipishani sana hivyo ukiona mkurugenzi wa bendi yoyote analalamika juu ya wanamuziki, basi ujue matatizo yao mara kadhaa yamekuwa hayapishani sana, ila wanaopishana tabia na namna ya kuongoza.
Mimi nina uzoefu na kuongoza wanamuziki wenzangu. Tangu nikiwa Twanga Pepeta pale hadi naachana nao, nilikuwa kiongozi wa bendi, hivyo bendi yangu hainipi shida kuongoza, kikibwa ni nidhamu ya hali ya juu na kusikiliza matatizo ya wanamuziki wangu pale panapowezekana kuwasaidia basi nafanya hivyo, hilo nimejifunza kwa bendi nilizopitia huko. Mwanamuziki anaweza kuondoka kwenye bendi kwa kitu kidogo tu hasa kutomsikiliza matatizo yake.
Papii Kocha ni mmoja wa waanzilishi wa bendi hiyo, lakini baadaye aliondoka pamoja na wanamuziki wengine na kwenda kuanzisha bendi ya Touwn Classic na kumekuwa na vijembe baina yao wanapopanda stejini.
Pia wanamuziki baadhi wameanza kurudi kwenye bendi yake ila Papii bado. Anasemaje kuhusu hilo? Je wana bifu?
Kalala Jr: Hivi vitu viko wazi bana na kuongea kwa binadamu ni kawaida ila hii mimi sihusishi na Papii kocha kutomrudisha Tukuyu na wala sina bifu naye na wala sitaki kumwongelea. Cha msingi aendelee kupambana na bendi yake huko kwani kila mwanamuziki ana mipango ya maisha yake.
Walioondoka na kurudi imekuaje?
Kalala Jr: Unajua kuna wakati wanamuziki huondoka kwenye bendi kwa kuaga vizuri, ndio maana hata akiomba kurudi kama nafasi ipo unamrudisha, ila wengine uondoka vibaya sana hao kiukweli huwezi kuwarudisha.
Tuhuma za ushirikina anasemaje?
Kalala Jr: Sijawahi kuroga wala kuwa mshirikina kwenye kazi yangu. Ukiona mtu ananiambia mimi natumia ushirikina kwenye kazi yangu, jua alijaribu kutuchezea bendi yetu hivyo ameshindwa na kutukuta sisi ni watoto wa Mungu na tunasali, sana basi lazima aseme natumia mambo ya ushirikina. Niseme tu sijawahi kurogwa kwa sababu sina imani za kishirikina.
Ndoa ya msanii wa filamu, Irene Uwoya na msanii wa Bongo Fleva, Dogo Janja inasemekana ni yeye aliyeivunja. Na vipi kuhusu uhusiano wa kimapenzi na msanii huyo?
Kalala Jr: Mimi huwa sipendi kuzungumzia mambo yangu binafsi kwemye media, ila hiyo skendo pia siwezi kuizungumzia kwa kulinda heshima ya Irene Uwoya na mimi pia japo hatukuwahi kuwa wapenzi ni vitu tu vilihusishwa kati yetu.
Kwenye kuendesha bendi kuna changamoto zake, kuiendesha Tukuyu Sound kuna changamoto gani?
Kalala Jr: Katika kazi changamoto lazima ziwepo sehemu yoyote ya kazi, ila namshukuru mungu napambana nazo hadi nimefika hapa.
Vipi kuhusu kuachia albamu?
Kalala Jr: Sisi Tukuyu huwa hatukurupuki kwenye kutoa nyimbo zetu, yaani hatufuati mihemko ya mashabiki kwa kutaka tu kila siku kutoa nyimbo. Huwa tuna utaratibu wetu kama unaona hadi sasa tuna nyimbo nne ambazo zinafanya vizuri ambazo ni ‘Koti’, ‘Chuki’, ‘Shukrani ya Wema’ na ‘Fumbo’ na mwaka huu tunatarajia kutoa albamu lakini jina tutawatajia baadae.