TUONGEEKISHKAJI: Kwanini wasanii wanapenda kusimulia shida?

MTU mmoja aliniuliza, “kwani ni lazima watu maarufu hususan wasanii wanapoongelea maisha yao waseme kwamba walitokea kwenye maisha ya tabu?”

Ni kawaida kusikia stori kwamba “baba yangu alinikataa tangu nikiwa tumboni kwa mama’angu” au “baba yangu alifariki tukabaki na mama ambaye alikuwa akiuza mama ntilie ili kutupeleka shule”. Wapo wengine wanasema “sikuweza kuendelea na shule kwa sababu nilikosa ada” au ‘nilikuwa sina pa kukaa nikawa nalala stendi” ama “nilikuwa sina hata pakula, nilikuwa naenda kwa mama ntilie kuomba ukoko.

Wapo pia utawasikia wakisema “nilikuwa sina nauli hata ya kwenda studio. Nilikuwa natembea kwa miguu kutoka Gongo la Mboto hadi Sinza kila siku kwa ajili ya kwenda studio.”
Ukweli ni kwamba kwa asilimia kubwa hayo yanayosemwa na wasanii si uongo. Wameyapitia. Wapo wanaoweka chumvi kidogo ili kunogesha stori, lakini wengi wanasema ukweli halisi. Swali ni Je, kwanini wanapenda kusema hivi?

Waandishi wa filamu, riwaya na hadithi zingine wanalo jibu la kwanini. Unapoandika filamu, riwaya au hadithi yoyote ile kitu  muhimu zaidi huwa ni mhusika mkuu a.k.a steringi. Ni muhimu kwa sababu hadithi au filamu huwa inamfuatilia steringi kwa ukaribu zaidi kuliko mhusika mwingine yeyote.

Sasa moja ya vitu muhimu vya kuzingatia unapoandika mhusika mkuu ni kumfanya atie huruma. Tazama muvi zote unazozijua. Kasome riwaya zote maarufu lazima steringi atie huruma.
Kama ni hadithi ya mapenzi steringi asipokuwa mvulana maskini anayependwa na binti kutoka familia ya kitajiri, basi itakuwa ni msichana maskini anayependwa na mvulana kutoka familia ya kitajiri. Ikiwa ni filamu ya kupigana, basi steringi ataanza kama boyaboya asiyejua kupigana, anayeonewa lakini mwisho atakuwa ndiye mpiganaji hodari na kuwapiga wote hasa wanaomuonea.

Watu wanapomuonea mtu huruma kitu cha kwanza ni huwa wanatamani kumsaidia. Lakini unamsaidiaje mhusika kwenye muvi ikiwa wewe ni mtazamaji? Huwezi. Kwa hiyo kinachofanyika ni mtazamaji anajikuta anakuwa timu stering kwa kumuombea dua ashinde. Na filamu inapoisha, steringi akishinda inakuwa furaha kwa mtazamaji.

Lakini moja ya sababu nyingine ya wahusika wakuu kuteseka ni kwa sababu binadamu wengi tunapenda kuwa marafiki na watu tunaofanana nao. Kisaikolojia kila mtu anapotazama filamu au kusoma hadithi anatafuta kitu ambacho anacho na steringi pia anacho.

Sasa kwa sababu watu wengi duniani wanapitia shida na mateso, wanapoona mhusika anapitia hali hiyo wanamuonea huruma na kujiona kama wanaendana, na wanajikuta wanakuwa timu steringi na mwisho wa siku filamu ikiisha kwa mhusika mkuu kushinda wao wanafurahi.

Lakini pia, moja ya sababu muhimu zaidi ni kwamba ili mtu ashinde inahitaji ashindwe. Ili staa aonekane amefanikiwa inatakiwa mwanzo aonekane ameshindwa. Kwa hiyo staa akianza kwa kuteswa kisha mwisho wa picha akawa mshindi kwa kuwashinda waliokuwa wanamtesa inaridhisha sana. Vuta picha unatazama muvi ambayo staa anashinda kuanzia mwanzo hadi mwisho inakuwa hainogi.

Sasa kwa kuyajua yote haya ndiyo maana wasanii na watu wengine maarufu wanapenda kusimulia maisha ya shida waliyokuwa nayo ili kuhakikisha wanawanasa wasikilizaji katika maeneo yote matatu hayo niliyosema hapo juu.

Kwa hiyo siku nyingine ukiona Chino Kidd anaonyesha nyumba ya udongo aliyokulia lengo la lake ni kuhakikisha unamuona mshindi kwa sababu sasa anaishi kwenye nyumba yenye viyoyozi pengine mpaka stoo.