TUONGEEKISHKAJI: Khaligraph kama Harmorapa tu

KWENYE maisha mikwara ni kitu muhimu. Kuna msemo wa mtaani unasema pesa huna, nguvu huna, hata mkwara? Na hili nimejifunza kutoka kwa watu wengi lakini mtu ninayemkumbuka zaidi alikuwa ni Harmorapa.

Kipindi hicho Harmorapa anatrendi ile mbaya nikawa na jukumu la kumtafuta na kufanya naye mahojiano. Nikaitafuta menejimenti yake nikaipata nikawaeleza nachohitaji wakaniambia haina shida atakuja. Tukapanga siku na muda. Nikaandaa kila mtu anayehitajika ofisini kwa ajili ya kazi hiyo. Kweli kufika saa saba mchana kama tulivyokubaliana nikapokea simu kutoka kwa askari pale getini ofisi za Mwananchi, Tabata, Dar es Salaam. Kamanda akaniuliza kuna mgeni wako hapa unaweza kuja kumpokea? Nikatoka kwenda nilipofika nikakuta bajaji imepaki ndani yake ikiwa na watu wawili upande wa abiria mmoja alikuwa Harmorapa mwingine sikumjua, lakini baadaye nilikuja kufahamu kuwa anaitwa Kiloriti - msanii mwenzake na Harmorapa ambaye walikuwa wanafanya kazi chini ya menejimenti moja.

Nikasalimiana nao kisha nikawaambia askari kuwa nawafahamu. Akawafungulia wakaingia ndani nikawachukua na kuwapeleka hadi ofisini, na kama ilivyo kwa wageni wengine nikawazungusha ofisi nzima kuwatambulisha.Wala sikuhitaji kutumia nguvu sana kwa sababu kila mtu alikuwa anamfahamu Harmorapa. Tukaingia chumba cha mahojiano taa, kamera na maiki vikawashwa. Harmorapa akakaa pale mimi nikakaa hapa. Mahojiano yakaanza. Nikamuuliza Harmorapa maswali mengi sana, lakini mojawapo lilikuwa: “Harmorapa unatrendi sana, bila shaka kutrendi huku kutakuwa kumekupa faida kiuchumi. Tuambie umeshafanya nini kwa kutumia uchumi huo hadi sana?” Harmorapa akajibu kwa kujiamini: “Naweza kumudu maisha yangu nina mjengo, nina gari, nina pesa za kutosha.”

Nikamuuliza: “Umejenga wapi?” Akaniambia ana mjengo wa ghorofa Mbezi Beach.

Nikamuuliza “una gari ya aina gani? Akanijibu, “Murano.” Nikamuuliza, “Iko wapi?” Nikimaanisha mbona hajaja nayo kwa sababu kumbuka, nilipokwenda kumpokea nilimkuta kwenye bajaji. Harmorapa bila uoga, aibu na wasiwasi akanijibu: “Nimekuja nayo. Ipo hapo nje.”

Ingekuwa mtu mwingine mgeni kwenye hii tasnia angehisi kuna bajaji zinaitwa Murano. Kwa sababu haiwezakani mtu umempokea wewe na umemuona anashuka kutoka kwenye bajaji halafu anakwambia ameshuka kwenye Murano.

Anachofanya Kaligraoh Jones, rapa kutoka Kenya kusema kwamba Watanzania hatuna kitu kwenye muziki na kama tuna uwezo, ametoa saa 24 kwa rapa wa Tanzania kuandika ngoma ya kumjibu maneno yake anayoyaongea kwenye mitandao hakina tofauti na mikwara ya Harmorapa. Huo ni mkwara kwa sababu kwenye muziki Watanzania tuko mbele sana ya Wakenya. Top 10 ya ngoma zinazosikilizwa zaidi Kenya kwenye mitandao ya kusikiliza nyimbo zinatoka hapa. Wakenya wanajua ngoma zetu kuliko sisi tunavyojua ngoma zao.

Wakenya wanamjua Diamond, Alikiba, Harmonize, Nandy, Zuchu, Darassa, Aslay, Rayvanny, Lavalava, Rose Muhando, Christina Shusho na zaidi.

Lakini nakupa mtihani waulize Watanzania watano wakutajie wasanii wa Kenya uone watakavyopata tabu na kuishia kuwataja Sauti Sol tu. Kwa hiyo Tanzania ni kubwa kimuziki Kaligraph anajua na sisi tunajua, ila ndo hivyo analeta mikwara ya Harmorapa, ya kujifanya kaja na Murano wakati tumemuona kwenye bajaji.