TUONGEEKISHKAJI: Hapa Simba pale Yanga, kule Mondi, Kiba na Nandy

Jumanne wiki hii kabla Simba haijacheza na Wydad Casablanca ya Morocco kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kila shabiki wa Yanga niliyepita karibu yake alikuwa akiiombea Simba ifungwe. Na siku iliyofuata, Jumatano, kabla Yanga haijacheza na Medeama ya Ghana mashabiki wa Simba ninaowafahamu walikuwa wanafanya sala moja tu - kuiombea Yanga ifungwe.

Kisha kuanzia Alhamisi kila upande ulikuwa ukajaribu kumuaminisha mwenzake jinsi gani ushindi walioupata ulikuwa rahisi. Simba wanasema huyo Medeama aliyecheza na Yanga yupo nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi yao, wakati mashabiki wa Yanga nao wanawaambia Simba kuwa kundi lao lilikuwa jepesi kiasi kwamba Asec wanaongeza kundi na pointi 10. Lakini licha ya kuchafuana bado mashabiki wa timu zote mbili wanakubaliana kwamba kwa sasa soka la Tan-zania limekua kwa kiasi kikubwa na hiyo ni kupitia mafanikio ya klabu hizo mbili kwenye michuano ya kimataifa.

Kwa maana hiyo ni sawa na kusema si Simba wala Yanga wote wanaamini kwamba wenzao wamefanikiwa na wanaambiana hilo licha ya kwamba ni wapinzani.

Nadhani hiyo ndiyo moja ya sababu kwanini Simba na Yanga zimekuwa burudani kubwa kwa Watanzania kwa muda mrefu. Watu wanajua ni upinzani, lakini bado wametengeneza chumba cha urafiki, udugu na upendo.

Kama siku wasanii wa muziki Tanzania wataamka na akili kama za Simba na Yanga nadhani tutapiga hatua kubwa zaidi ya tulipo kwenye muziki kwa sababu upinzani wa wasanii wa muziki unatajwa kuwa ‘toxic’ sana. Wasanii wanatajwa kufanyiana mambo ambayo yamevuka ‘level’ ya kuitwa upinzani. Wenyewe wameshafikia kwenye uadui. Kwa mfano,  miaka kadhaa nyuma mmoja wa wasanii wakubwa alikuwa akifanya shoo Mombasa, Kenya kwenye jukwaa moja na msanii wa Marekani, Chriss Brown.

Lakini ilipofika zamu yake kupanda jukwaani inadaiwa kuwa kulitokea hitilafu ya kiufundi na akashindwa kutumbuiza. Baadaye zikasambaa taarifa kwamba msanii huyo na uongozi wake waliamini kwamba alifanyiwa figisu na timu ya mmoja wao.

Na inadaiwa kuwa hiyo ndiyo ilikuwa sababu ya msanii aliyesingiziwa kuweka kibwagizo fulani kwenye wimbo wake ikiwa ni kijembe kwa msanii mwenzake. Na siyo hilo tu, miaka kadhaa mbele meneja wa msanii huyohuyo ali-zungumzia jinsi gani msanii wake asivyotamani hata kidogo kupatanishwa na mpinzani wake kwa sababu kuna kipindi mameneja wa pande mbili walitamani kujaribu kuwasuluhisha. Siyo hivyo tu, mwaka huu mwanadada Nandy alitema cheche kwenye akaunti yake ya Instagram akieleza jinsi kampuni na lebo fulani ya muziki kubwa nchini inavyomfanyia figisu kwenye muziki. Mifano niliyoitaja hapo juu unaweza kuitafakari utakavyo, lakini mwisho wa siku inatoa taswira ya upinzani wa wanamuziki Bongo ulivyovuka mipaka na kuwa uadui na hilo siyo jambo zuri. Upinzani unapendeza uki-wa kama wa Simba na Yanga.