TUONGEEKISHKAJI: Dua kwa wasanii wetu wawe na mwisho wa kupendeza

DEAR God, tunatambua mtaani kuna madogo wengi uliowapa vipaji, kuna wanasoka kama Samatta, kuna watu wana rap kumzidi Young Lunya, kuna watu wenye voko kali Damian Soul haoni ndani, kuna waigizaji konki kina JB wakasome, kuna waandishi wa filamu Lamata anaomba poo.

Kuna madairekta matata sana, kuna madansa Mose Iyobo hapati namba na wote hawa wanaamini siku moja watakuja kupata nafasi, wanaamini siku moja watatoboa na wanasubiri kwa hamu siku hiyo ifike na tunaamini umeshaichagua hiyo siku na itafika tu.

Hata hivyo, baba tunaomba wakitoka, usiwaache hapo. Tunaomba uendelee kuwasimamia hata wakishakuwa mastaa kwa sababu baba kuendelea kubaki staa ni ngumu kuliko kuwa staa. Baba tumechoka kuona mastaa wetu wanakuwa na mwisho usiopendeza.

Baba tumechoka kuona marapa wenye sauti nzito zenye panchi kama radi na uwezo mkubwa wa kuandika mashairi na kufreestyle na kurap wanaishia kuwa mifano ya kwanini vijana hatutakiwi kutumia dawa za kulevya.

Baba hao wasanii sio ndugu zetu wa tumbo moja lakini ukweli inaumiza kuona watu ambao tulikuwa tunatoroka ‘home’ kwa kuruka ukuta kwenda kwenye shoo zao, tulikuwa tumejaza ngoma zao kwenye simu na flash na memory card na CD za kuburn huku tukiamini hawa ndiyo mabroo, wanaishia kuwa mateja baba. Inaumuiza sana.

Hiyo baba inafanya hata wazazi huku mtaani waanze kuogopa watoto wao kuwa wasanii.

Hivyo baba tunaomba uwasimamie hawa wasanii, tunaomba uwape nguvu. Tunaomba uwaondoshee pepo la kufulia kwa sababu baba huku mtaani kuna masista umewapa vipaji kama Nandy, kama Vee Money, kama Jide, kama Giggy.

Lakini wazazi wao wanaogopa kuwapa fursa ya kujaribu vipaji vyao kwa sababu hali inaonekana sio nzuri kwa sababu huku mtaani stori ni, msanii wa muziki ili apate pesa ya kuishi kama msanii analazimika kufanya na mambo mengine ambayo muda mwingine hata hayakupendezi baba, hicho ndo kinachowatisha wazazi.

Baba waondolee wasanii wetu pepo la kufulia ili wamalize hadithi zao vizuri. Haipendezi kuona kila msanii hadithi yake inaisha vibaya. Yaani mfano tukitazama wakongwe wa filamu na muziki, asimilia 90 hadithi zao hazijaisha vizuri. Kwa nini iwe hivyo baba? Kwa nini hadithi zao zisiishe kama watu wa kada na taaluma nyingine. Kwa nini hadithi za wasanii zishiishe kwa ushindi.

Kwanini hadithi za wasanii ziishie rehabu wakipatiwa matibabu ya madawa ya kulevya. Kwanini hadithi za wasanii ziishie kufulia kukosa hata pa kulala. Kwa nini hadithi za wasanii ziishie kwa namna hiyo. Kwa nini ziishie wakiwa mabilionea, wakiwa bado ni watu wenye ushawishi mkubwa?

Baba mpaka tumekuja kwako maana yake hili hatuliwezi tena kwa uwezo wetu. Tunaomba wasimamie washikaji zetu.