TUONGEE KISHKAJI: Watakaonipokea baada ya Mwanaspoti

NAWAZA siku nikiondoka Mwanaspoti huko nitakapokwenda watataka uhusiano wangu na Mwanaspoti uwe vipi? Je watapenda amani kati yangu na kampuni hii iliyonielea na kunikuza kitaaluma au watataka mimi na Mwanaspoti tuwe kama paka na panya, Simba na Yanga, Harmonize na Diamond, maadui wakubwa, mafahari tusiopikika chungu kimoja.

Nawaza, je wataniruhusu niwe naposti picha zangu za TBT zikinionyesha jinsi gani nilikuwa nafurahia maisha ya hapa au hiyo itawakera na pengine itakuwa inakinzana na sera zao. Kwamba pengine, sera zao zitanilamizisha kila nitakachokizungumza kuhusu Mwanaspoti kiwe ni cha kuwasiliba Mwanaspoti?

Je, washkaji zangu wa hapa Mwanaspoti wakiwa wanaoa, huko nilipokwenda wataniruhusu kuchangia harusi au hata kwenda kwenye harusi? Au kwa kufanya hivyo watakuwa wananiona kama vile nimeenda kuvujisha siri za kampuni na nitaonekana msaliti.

Nawaza, je, kama siku nikiwa nataka kuweka tangazo langu kwenye gazeti la Mwanaspoti kwa sababu linaongoza kwa kuwafikia watanzania wengi, je hiyo kampuni yangu mpya nitakayokuwa nafanyia kazi wataniruhusu kweli? Au ndo watazua mjadala wa kwamba kwanini hukutumia gazeti hili unalofanyia kazi sasa?

Nawaza, kwani ni lazima kila unapohama eneo la kazi kwenda lingine ugombane na ulikohama? Au uwaongelee vibaya? Kwamba hauwezi kuwazungumza vizuri?

Nawaza, hivyo kwa sababu naona ndiyo staili ya wasanii wa Bongofleva wanaohama kutoka ofisi za zamani kwenda zingine aidha iwe kubadilisha lebo ya muziki, kubadilisha prodyuza, kubadilisha menejimenti, kubadilisha studio, kubadilisha dairekta wa video, ni lazima akiondoka tu aanze kumuongelea vibaya mtu aliyekuwa akifanya naye kazi.

Anjella ambaye alikuwa ni msanii wa Konde Gang kaachia wimbo wake mpya wa Blessing, na kwenye video ya wimbo huo tunaona kawatumia watu wenye mfanano wa Harmonize na Kajala ambao walikuwa wapenzi, wakati Anjella anafanya kazi chini ya Konde Gang, lebo ambayo inamilikiwa na Harmonize.

Na stori ya kwenye video ya wimbo huo pamoja na mashairi ya wimbo wenyewe inaonyesha wazi kwamba huenda Anjella alihama lebo hiyo kwa sababu ya mazingira ya kazi kutokuwa na utulivu. Na kukosekana kwa utulivu huko kumesababishwa na mapenzi au mpenzi wa Harmonize  ambaye ni Kajala.

Na hii sio mara ya kwanza msanii kufanya hivi. Harmonize alishafanya kitu cha kufanana na hivyo alipoondoka WCB ambayo iko chini ya Diamond. Binafsi najiuliza kufanya hivyo kuna faida gani za muda mrefu? Naelewa kwamba, ukifanya hivyo utapata faida ya kutrend kwa siku mbili tatu lakini baada ya hapo nini kitafuata? Utafanya nini tena kuendelea kutrend au kuwa pale juu, sehemu ambayo umefika kwa sababu ya kuisema vibaya ofisi yako ya zamani? Au pengine hayo ni moja ya masharti ya sehemu mpya wanazokwenda?

Kama msanii ni msanii mzuri, huhitaji kuwasema vibaya wengine ili kutrend labda kama sanaa yako ni michambo. Lakini kama unafanya muziki, we imba muziki mzuri, tangaza muziki wako, achia mashabiki waamue wakubebe hadi wapi.