TUONGEE KISHKAJI: Wasanii wanaotisha mashindano ya vipaji huenda wapi?

NIMEBOREKA naingia Youtube natafuta video za usaili wa Bongo Star Search ili nicheke. Ndiyo, ili nicheke najua Bongo Star Search ni shindano la kusaka vipaji vya waimbaji, lakini kipindi cha usaili BSS huwa ni kama shindano la kutafuta wachekeshaji.

Vituko vinavyofanyika pale sio vya kitoto majaji wenyewe wanashindwa kuvumilia wanakufa kwa vicheko, na mimi kwa nini nisicheke.

Napitia zangu video mbili tatu mara YouTube wananipa mapendekezo ya kutazama video za America's Got Talent ambalo lenyewe ni shindano la kusaka vipaji mbalimbali duniani linalofanyika Marekani.

Nabonyeza video ya msichana mmoja naanza kutazama. Dada anapanda jukwaani, anajitambulisha, anajibu maswali mawili matatu ya majaji kisha anapewa steji, anaambiwa anza kutuonyesha mambo. Anaanza.

Oya, huyo dada anaimba kinoma, anaimba ile yenyewe kabisa, dada ana sauti kuliko wasanii ambao tayari wameshatoka. Wakati sista anaimba mashabiki jukwaani walikuwa wanalia, kama hiyo haitoshi Simon Cowell, jaji mwenye roho mbaya zaidi kwenye mashindano hayo akabonyeza kitufe kinaitwa ‘Golden Buzzer’, yaani jaji yoyote akikubonyezea hiko, maana yake wewe umepitwa bila kupingwa. Na Simon ni jaji ambaye yeye huwa hakitumii kabisa kitufe hiko.

Aisee, huo usaili ulikuwa ni wa kibabe nikasema ngoja nishuke kwenye comment nione wadau wanasemaje. Comment ya kwanza kukutana nayo ilikuwa inasema kwa kizungu, natafsiri; “Inashangaza kuona kuna watu wengi waonajua kuimba, wanakuja kwenye majukwaa kama haya na hata kushinda wanashinda kabisa, lakini wakitoka hapa, huwasikii tena, milele.”

Hiyo comment inanifanya nitafakari sana. Nakumbuka wasanii wakali niliowahi kuwaona kupitia BSS. Unakuta kwenye BSS kuna washkaji wanaimba kuliko Diamond, kuliko Alikiba, kuliko wasanii A LIST wetu wa Tanzania, lakini washkaji wakitoka hapo huwasikii kokote.

Nakumbuka wasanii wakali niliowahi kukutana nao kwenye studio za muziki. Washkaji wanaandika, wanaimba na muziki wanaujua, lakini miaka nenda rudi hawasikiki. Kwanini?

Ni kwa sababu muziki unahitaji zaidi ya kuimba. Yaani kujua kuimba tu peke yake hakukupi uhakika wa kutoka. Kujua kuandika tu peke yake hakukupi uhakika wa kutoboa. Na kujua vyote pia hakukupi uhakika kuwa msanii mkubwa.

Muziki na sanaa karibu zote zina mambo mengi yanayoendelea nyuma ya pazia ambayo sio kila mtu anayaweza . Wengine ni wasanii wazuri sana wakiwa kwenye mashindano kama BSS kwa sababu kwenye mashindano hayo kinachohitajika ni kuimba tu. Lakini wakipewa nafasi na kuingizwa kwenye tasnia, wanagundua kuwa imejaa mambo mengi ambayo hawayapendi au hawayawezi.

Mfano mwepesi, muziki wetu wa sasa bila kiki hauendi. Yaani ili msanii ufanye vizuri ni lazima maisha yako yajae drama. Sasa kuna watu hawawezi maisha hayo. Wenyewe wanapenda maisha ya utulivu, utulivu na kazi za burudani ni mbingu na ardhi.

Moja ya washindi wa mwanzo kabisa wa BSS aliwahi kunambia, yeye bado anafanya muziki chini chini kwa sababu alishindwa maisha ya muziki wa Bongofleva. Anasema yalikuwa yanamnyima amani. Yamejaa drama na matukio ambayo yeye alikuwa akiyafanya mchana, usiku akijifungua ndania analia.