TUONGEE KISHKAJI: Waandishi tunamdisi Dogo Janja kwa vitu ambavyo wenyewe tunaviishi
CHARLES Abel, mwandishi wa gazeti hili ni mmoja wa watu wachache sana sana sana ninaowafahamu duniani wasiokuwa wanafiki hata kidogo. Na neno mnafiki mimi hulitafsiri kama kuzungumza vitu visivyoendana na matendo yako. Ukituambia wewe ni Mchamungu sana halafu ukafanya tofauti na Wachamungu wanavyotarajiwa kufanya huo utakuwa ni unafiki.
Siku moja Charles aliandika kwenye mitandao yake kijamii kuhusu waandishi wanafiki waliokuwa wanaongelea ishu ya Fei Toto pale Yanga aliandika: “Ndugu waandishi wenzangu tukishamaliza kupigania maslahi ya Fei Toto tuanze kupigania na maslahi yetu. Fei analipwa Sh4 milioni tunasaidia kumuonyesha kuwa ni ndogo. Na sisi tuanze kujisaidia kuboreshewa maslahi kwenye sekta yetu maana wengi hatufikii hata robo ya hela anayolipwa Fei.”
Kwangu huo ulikuwa ni ukweli wa kiwango cha juu kabisa na ndiyo maana majuzi nilipoona video ya waandishi wa chombo kimoja cha habari wakimcheka Dogo Janja nikakumbuka sana alichosema Charles.
Waandishi walikuwa wanazungumza kwamba Dogo Janja huko Instagram anaposti mapichapicha akila bata Dubai, Uturuki, lakini nyumbani kwao Arachuga familia yake inaishi kwenye banda. Lakini ukiniuliza mimi hayo ndiyo maisha yetu waandishi, na pengine hata wale waliokuwa wanazungumza hilo ndiyo maisha yao.
Waandishi tuna majina makubwa. Ukitusikia kwenye redio tunavyozungumza kwa machejo tunavyojua kuumba maneno na takwimu zetu za ‘kugugo’ huku tukizipanga kwa vingereza viwili vitatu ili tuonekane wachambuzi kweli utapagawa mwanangu. Tunazungumza utadhani akaunti zetu za benki zina kiasi cha pesa sawa na likes na comments tunazopata kwenye mitandao ya kijamii. Lakini ukweli tunaujua. Ukweli ni kwamba akaunti zetu zina hali mbaya. Zinasomeka utadhani namba za frequency za vituo vya redio tunazotangaza. FM.
Na ukiwa unatutazama kwenye TV ndo usiseme. Tumevaa suti, tumepakwa makeup usoni, wanawake wamesuka vizuri. Tunatangaza habari tukitabasamu utadhani nje
tumepaki gari za milioni 600, wazazi wetu tumewajengea maghorofa Mbezi Beach na kila likizo huwa
tunakwenda Santorini Ugiriki. Kumbe hakuna lolote tukitoka tunadandia daladala wengine kwa aibu tunaamua kuchukua bodaboda. Wazazi wetu wanaishi kwenye hali ya mbaya ya kiuchumi huko Nachingwea na kuhusu likizo ndiyo usiseme, tuna hali mbaya mpaka tunaogopa kuchukua likizo. Utakwenda likizo huna pesa?
Kwenye magazeti hamtuoni lakini mkitusoma mnajisikiaje? Unatuvutia picha gani? Tuko vizuri eeh? Basi endelea kutuona tuko vizuri hivyohivyo.
Ninachosema tu ndugu zangu waandishi tujitahidi kupunguza unafiki. Tujitahidi sana kupunguza moto wa kupigania maslahi ambayo sisi wenyewe hatupati. Nafahamu ni kazi yetu waandishi kufichua changamoto zilizopo kwenye jamii, lakini kama tutakuwa tunafichua zile ambazo huku kwetu zimejaa tele na wala hatuzifanyii chochote huo unakuwa ni unafiki yaani maneno yetu yanapingana na matendo yetu.