TUONGEE KISHKAJI: Unamchukulia poa Dulla Makabila? Soma hapa

MACHI 2021 niliandika makala kwenye gazeti hili ikimhusu Dulla Makabila. Makala nzima ilikuwa inaongelea Dulla alivyo ‘genius’ wa maaidia kwenye muziki ambao watu wanauchukulia poa, wanauchukulia wa kihuni muziki wa singeli. Kwa hiyo pengine hata hawamzingatii kwa sababu wanaona ‘aaaah! ndo walewale wa kuimba nakupenda wewe na uyo bwana ako.’
Kwenye hiyo makala nilichambua ngoma zake karibu zote zilivyo na mawazo tofauti. Yaani anaongelea jambo fulani la kawaida kwenye jamii lakini kwa namna isiyokuwa ya kawaida. Anaongea kisanii sana. Na kama ni mtu wa kuchukulia poa muziki wa singeli unaweza usimzingatie. Na kwa sababu hiyo nataka usome hapa pengine mawazo yako yatabadilika.
NIMEGHAIRI KUFA
Wimbo huu aliuachia Desemba 2020 na ndani yake Dulla anaimba kama mtu aliyejiua lakini akaghairi kufa baada ya kuona yaliyojiri baada ya kufa. Ukisikiliza juujuu unaweza kudhani anaimba ili watu wacheze muziki mpaka miguu ijae vumbi kama zilivyo ngoma zingine za singeli, lakini kwa sikio la tatu utaelewa kuwa kupitia wimbo huo Dulla anazungumza kuhusu thamani ya maisha ambayo labda watu hawaioni wakiwa hai.
Anazungumza kuhusu mambo mazuri tunayostahili kuyasheherekea tukiwa hai na jinsi ambavyo tutayamisí siku tutakapomaliza safari ya maisha duniani. Kwa lugha rahisi Dulla anakumbusha watu wanavyotakiwa kuthamini uhai.
NINGEKUWA DEMU
Huu ni wimbo wa Dulla ambao ulipata maoni mengi mabaya kwa sababu alikuwa anazungumza vitu ambavyo angefanya kama angezaliwa mwanamke; watu wakamshambulia kwamba kwanini mtoto wa kiume utamani kuwa demu?
Hata hivyo ukisikiliza kwa makini utagudua meseji katika wimbo huo ilikuwa ni kuzinyooshea kidole tabia mbaya ambazo wanawake wengi wa sasa wanatajwa kuwa nazo kwa mfano vitu kama vile kudanga, umalaya na kutoa mimba.
DUA
Kama lilivyo jina la wimbo ndani Dulla anaimba kama anayeomba dua kwa Mungu ashughulikie mambo fulani fulani ambayo pia yalikuwa gumzo kwenye mitandao ya kijamii.
Vitu kama vile maoni ya baadhi ya mashabiki waliodai msanii Harmonize anaimba kama aliyekuwa bosi wake wa zamani, Diamond Platnumz. Pia anaongelea kuvunjika kwa Yamoto Band, bifu la Diamond na Alikiba, tuhuma za Mkubwa Fella kutapeli wasanii aliokuwa akiwasimamia na mengine.
Baadhi ya mistari kwenye wimbo huo inaimbwa “naomba dua irudi tena Yamoto Band, na namuombea Harmonize asimkopi Diamond, pia Diamond na Ruge mambo yarudi kama zamani.”
NITAKUWAJE
Kwenye wimbo huu Dulla anaimba kama mtu ambaye sio mlevi lakini anataka kujaribu kunywa pombe ili aone atakuwaje. Kupitia mdundo uliotengenezwa na Don Kiwango, Dulla anaimba huku akijaribu kutengeneza picha ya tabia anazodhani atazifanya akilewa.
Hata hivyo, ukisiliza kwa makini kupitia wimbo huo utagundua Dulla anatumia lugha ya kisanii kuonyesha tabia mbaya zinazosababishwa na baadhi ya walevi kama vile kudhalilisha wanawake (wahudumu), kufanya fujo na hata kuikosesha familia amani.
MAKABILA
Wimbo huu ndiyo uliompa jina la Makabila na ndani yake Dulla anaimba kama mshikaji anayewaelezea wenzake kwanini hataki kuoa mpaka ajue kabila la anayetaka kumuoa.
Kwa haraka unaweza kusema ni wimbo unaochochea ukabila, lakini ukweli ni kwamba wimbo huo unaonyesha jinsi Watanzania tulivyofanikiwa kuishi kwa amani bila vita za ukabila licha ya kuwa na makabila tofauti zaidi ya 100.
Huyo ndiye Dulla Makabila. Genius kwenye muziki unaochukuliwa poa.