TUONGEE KISHKAJI: Ugomvi wa Harmonize na Kajala ni 'full maokoto'

KUNA wazee waliimba, mapenzi yamegawanyika katika sehemu kuu mbili. Sehemu ya kwanza ni faraja, vicheko pamoja na furaha utadhani dunia hii ndugu yote ni yako. Sehemu ya pili ni kasheshe, ugomvi pamoja na chuki, polisi mahakamani watu kufikishana.

Kama wale wazee wangetoa hiyo ngoma leo bila shaka wangeongeza sehemu ya tatu ya mapenzi ambayo fursa ya kutengeneza maokoto na mchele. Nitakwambia kwanini.

Kwa sasa kwenye mitandao ya kijamii hususan Instagram kinachotrendi ni matusi wanayotupiana Kajala na Harmonize. Tunafahamu wameachana. Walikuwa kwenye penzi nzito. Penzi la mfano wa kuigwa. Lakini sasa wamekuwa maadui. Wanatukanana na kuvujiashiana siri. Harmonize anasema “nilikuonea huruma tu, ningetaka kukudhalilisha tulipoachana ningekuchua gari zangu uone ungeendesha nini.” Kajala anajibu, ‘babu usinitoe roho na magari yako kwanza kwa pesa gani? Ungekuwa na pesa ungejenga fensi nyumbani kwa mama ako Kimara.”

Ni drama ambazo ukiziangalia unaweza ukadhani wako ‘siriazi’ na mapenzi lakini usikute hakuna hiyo.Usikute drama zao ndiyo aina ya kujipatia kipato kwenye dunia ya sasa ya teknolojia na mitandao ya kijamii na wala sio kitu kibaya.Na ukiniuliza  nitakuambia hakuna ‘couple’ inayonufaika na ugomvi wa mapenzi kama ya Konde Boy na Kajala.

Harmonize alipokuwa kwenye penzi na Kajala ndio wakati alitoa nyimbo nyingi nzuri. Haina maana kwamba huko nyuma alikuwa anatoa nyimbo mbaya, hapana. Ila alipokuwa na Kajala ni kama vile alikuwa na uwezo wa kutoa ngoma  kila asubuhi kwa sababu mada ya kuimba alikuwa nayo karibu, analala na kuamka nayo. Nyimbo kama Nitaubeba, Mtaje, Wote na nyingine nyingi zote Konde Boy amewapatia mashabiki lakini ni kama vile alimuandikia Kajala na mtaani zimefanya vizuri.

Na walipoachana ni hivyo hivyo, nyimbo kama Single Again moja ya nyimbo za Konde Boy zilizovuka boda, ngoma kama Dear X na Vibaya zote ziliimbwa zikimuongelea Kajala au zikiwa zimechochewa na kuvunjika kwa penzi lake na Kajala. Na upande wa Kajala bila shaka wote tunakubaliana kwamba kwa sasa hatujui kama ni mcheza filamu au mwanamuziki kwa sababu kwa muda sasa hajafanya chochote ambacho kinaweza kumuweka moja ya sehemu hizo. Lakini bado ni staa mkubwa. Tunamfahamu na tunamfuatilia.

Hivi sasa Kajala ana ‘reality show’ yake inayoitwa Behind Gram ambayo inaonyesha maisha ya Kajala hususan pamoja na binti yake Paula. Kwa hiyo ukiniuliza nitakuambia Kajala kuachana kwa staili ya kutukanana mitandaoni inamsaidia kumpa ‘content’ kwa ajili ya kutengeneza kipindi chake.

Pia kuachana kwake kwa ugomvi na Harmonize kunavutia sana dili za ubalozi. Kwa mfano tuliona juzi alikuwa kwenye mkutano na waandishi wa habari wa bidhaa fulani, lakini kwenye tangazo la kuwaalika waandishi hao akasema “nawakaribisha na nitaongea kila kitu”.

Ni wazi kwamba “nitaongea kila kitu” hakumaanisha kuhusu bidhaa anayokwenda kuitangaza, hapana. Bali bidhaa kuhusu kasheshe lake na Harmonize akiamini kwa kusema hivyo waandishi ‘mamilioni’ watapeleka makamera yao kwenye mkutano huo.