TUONGEE KISHKAJI: Sio dhambi msanii kufanya kazi nzuri na kuokota maokoto

MTAANI kuna msemo watu huutumia pindi wanapomshindanisha Diamond na Alikiba, wanasema Diamond sio msanii, ni mfanyabiashara na Alikiba ni msanii. Naelewa msemo huu umetokea wapi lakini mimi sikubaliani nao.

Chanzo cha msemo huu unatokana na watu wanaoamini kwamba, mafanikio makubwa ya Diamond kwenye muziki hayatokani na kwamba anajua sana kuimba au labda kwa sababu yeye ni msanii mkubwa sana, hapana.

Kwamba Diamond amefanikiwa sana kwenye gemu kwa sababu tu anajua namna ya kucheza na soko. Anajua kulisoma soko. Anajua watu wanahitaji nini na anawapatia wanachohitaji.

Na kwamba Alikiba ni msanii kwa sababu, hana redio na tv kama Diamond, hana mabiashara makubwa kama tunavyosikia kwa Diamond, hana magari mengi ya bei mbaya kama anayotuonyesha Diamond lakini bado yupo kwenye gemu miaka yote, kinachomuweka hapo ni kwa sababu anajua muziki tu.

Sikubaliani na msemo huu kwa sababu naamini mtu mmoja anaweza kuwa na vyote hivyo. Diamond anaweza kuwa mfanyabiashara na msanii.

Misemo kama hii inakuja kwa sababu kiwanda chetu cha muziki ni kigeni kwenye suala zima la biashara. Tanzania tumekuwa na wasanii wengi wazuri kabla ya enzi za kina Remmy Ongala, baada ya enzi za kina Sikinde na hata mwanzoni mwa enzi za kina Profesa Jay na Bongofleva. Lakini katika kipindi chote hicho wasanii wetu walikuwa wanafanya kazi kwa ajili ya mapenzi waliyokuwa nayo kwenye sanaa.

Msanii ana nyimbo zinashika chati kwenye Top 10 redioni lakini mfukoni hana kitu. Wazee wetu wanakwenda kutumbuiza na bendi, wanapata laki moja laki mbili, wanagawana elfu kumi na tano, wanarudi nyumbani.

Kwa aina hiyo ya maisha, wasanii wetu wakawa wanaamini kwamba msanii sio kupata pesa, msanii ni kufanya sanaa kwa mapenzi, kuwa maarufu, majirani kujua kwamba unapiga gitaa sikinde au Msondo, unafahamiana na TX Moshi Wiliam.

Kwahiyo watu kama kina Diamond na AY walipokuja na kuanza kupiga pesa kupitia muziki tukaanza kuwaona kama vile ni wasaliti.

Yaani ni kama vile tulikubaliana kwamba, tutakuwa tunafanya hii kitu bila kupata pesa, lakini ghafla wenzentu wakapita mlango wa nyuma na kuanza kupata pesa kupitia kitu hiki hiki.

Wanangu, narudia tena, muziki ni biashara na msanii anaweza kuwa vyote, mfanyabiashara na msanii. Hata wasanii wa nje ambao tunaona wana vipaji na uwezo mkubwa wa kufanya sanaa zao, wanapata pesa mbaya mno kupitia hizo hizo sanaa zao.

Kina Beyonce wana pesa chafu kupitia muziki wao, kina Michael Jackson walikuwa ni mamilionea kupitia muziki wao. Kwahiyo tupambane kuwaaminisha wasanii wetu kwamba, unaweza kuwa msanii mzuri ukawa na pesa. Tutawazindua.