TUONGEE KISHKAJI: Media imemuonea Ommy Dimpoz

MTANGAZAJI wa chombo fulani cha habari yuko zake Sumbawanga kwenye majukumu yake ya kiofisi. Mara anakutana na mzee anayejitambulisha kuwa ni baba mzazi wa msanii supastaa wa muziki wa Bongo Fleva, Ommy Dimpoz. Mzee ni dereva wa bajaji yaani sio kwamba mzee anatembelea bajaj, hapana. Mzee mishe zinazompatia riziki ni kuendesha bajaji. Wakati huku Dar mwanaye ni maarufu halafu anaonekana ana pesa vibaya mno.

Ukiingia Instagram ya Ommy Dimpoz utapiga saluti. Jamaa anakula bata sio poa - tena bata za bei mbaya sio bata za kushea chupa za hennessy na kuji-snap za kidimbwi.

Picha zake jamaa ni yuko Dubai, ukishuka kidogo utaona mapicha picha yupo Santorini - Ugiriki. Na majuzi ndiyo alivunja rekodi alikuwa anaposti picha akiwa Old Trafford, Manchester na mastaa karibu wote wa Manchester United. Aliposti picha na Cristiano Ronaldo, Bruno Fernandes na wengine kibao kasoro ya Harry Maguire tu.

Basi mtangazaji akamtazama huyu mzee, kisha akatazama Instagram ya Ommy Dimpoz akasema hapana, hii ishu nikipata video fupi nikaweka mtandaoni itatembea sana. Itapata likes kama zote. Kweli akamrekodi, video ikapanda baada ya muda Watanzania kama unavyotujua tena tukaanza kumshambulia Ommy Dimpoz: “unakulaje bata kiasi kile wakati baba yako ni dereva wa bajaji huko Sumbawanga anagombania wateja wa buku mbilimbili... Yaani unashindwa kumnunulia hata bajaji nne halafu ukawapa vijana wawe wanampelekea hesabu?”

Watu ‘wakam-bully’ sana Ommy bila hata kusikiliza upande wa pili wa kwanini mtoto anatanua halafu baba yake anaendesha bajaji kule Sumbawanga.

Lakini baadaye Ommy akaamua kuvunja ukimya na kueleza kuwa ni kweli yule mliyemuona Sumbawanga ni baba yake mzazi na ni kweli hamsaidii kwa chochote na anafanya hivyo makusudi kwa sababu baba yake huyo hakuwahi kumsaidia kwa lolote tangu azaliwe. Alimtelekeza, Ommy akalelewa na mama yake.

Ommy anasema kauli mbiu yake ni kwamba ‘yeye hutumia na watu ambao walikuwa naye kwenye nyakati ngumu.’

Stori za baba na mtoto mimi naona sio ishu sana kwetu mashabiki. Zimekaa kibinafsi zaidi labda msanii mwenyewe atake kuzifanya za jumuiya kama ilivyofanya familia ya Diamond kwenye ishu yao kuhusu mzee Abdul na mzee Nyange. Mama Diamond alizungumza alipopigiwa simu redioni na kusababisha tatizo la kwenye familia liwe la jumuiya.

Kwa upande wangu nachoona ni miyeyusho. Ni jinsi media tunapolazimisha stori za udaku na skendo kwa wasanii ambao wala hawana muda na aina hiyo ya maisha.

Msanii kama Ommy ni kati ya wasanii wachache sana Tanzania ambao wamejenga majina yao bila kutumia hata punje ya skendo au kiki.

Nakumbuka Ommy amewahi kuwa habari ya mjini kwa mambo yasiyohusisha muziki mara tatu tu. Kwanza alipogombana na Diamond, pili alipogua sana hadi akashindwa kuumwa na tatu ni yale mambo Ney wa Mitego anayomtania nayo. Nadhani vyombo vya habari tujifunze kuwaheshimu watu wasiotaka maisha yao binafsi kuwa sehemu ya kazi zao kuliko kulazimisha kupata ‘content’ kwa njia ya kuwaumiza au kuwasababishia matatizo wengine. Hili la Ommy ni sawa tu na kulazimisha watu wamchukie wakati ndo kwanzaaaa haipo vile.