Nyuma ya pazia Diamond kushuka shoo za kimataifa

Muktasari:

  • Tangu kushika kasi kwa janga la virusi vya Corona duniani mwaka 2020, idadi ya shoo za Diamond kimataifa zimepungua na hadi sasa hazijarudi kama ilivyokuwa mwanzo.

Mwimbaji wa Bongofleva kutokea WCB Wasafi, Diamond Platnumz anaonekana kuzidi kupunguza shoo za kimataifa kadiri miaka inavyozidi kusonga mbele licha ya kila mara kutangaza thamani yake kupanda katika soko.

Tangu kushika kasi kwa janga la virusi vya Corona duniani mwaka 2020, idadi ya shoo za Diamond kimataifa zimepungua na hadi sasa hazijarudi kama ilivyokuwa mwanzo.

Utakumbuka Diamond alitoka rasmi kimuziki na wimbo wake, Kamwambie (2009) uliobeba jina la albamu yake ya kwanza na mwaka uliofuatia alishinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA), kama Msanii Bora Chipukizi.

Kwa mujibu wa Diamond, hadi kufikia Aprili 2020 alikuwa amepata hasara ya Sh3.5 bilioni kutokana na kuhairishwa kwa shoo zake za kimataifa kufuatia mlipuko wa virusi vya Corona vilivyoathiri shughuli nyingi duniani.

Februari 16, 2020, Diamond alitoa orodha mtandaoni ya shoo zake 19 ambazo alipaswa kuzifanya kuanzia muda huo hadi Julai 19 ambapo shoo ya mwisho ilipaswa kufanyika London, Uingereza.

Shoo nyingi zilipangwa kufanyika Finland, Ujerumani, Ufaransa, Réunion Island, Sweden, Guinea, Ivory Coast, Sudan ya Kusini, Madagascar, Comoro Islands, Mayotte Islands, Marekani, Uholanzi, Ureno, huku baadhi ya nchi akiwa na show kati ya mbili hadi tatu.

Diamond alitangaza kuahirisha shoo zake mnamo Machi 12, 2020 akiwa barani Ulaya, ambapo alipaswa kutumbuiza Brussels, Helsinki, Dortmund, Marseille na Gothenburg.

Mnamo Julai 2021, Meneja wa Diamond na WCB Wasafi kwa ujumla, Sallam SK alitangaza kuwa Diamond huwa anatoza Dola70,000 kwa shoo za kimataifa.

Kwa muktadha huo, kuahirishwa kwa shoo zake 19 barani Ulaya, Diamond alikosa mapato ya takribani Dola1.3 milioni, wastani wa Sh3.4 bilioni kulingana na viwango vya kubadilishia fedha kwa sasa.

Msanii mwingine wa Bongo Fleva aliyeahirisha shoo zake za kimataifa ni Nandy, huyu alifuata maonyesho yake 13 yaliyopangwa kufanyika nchini Marekani katika ziara yake ‘Nandy Na Nusu World Tour 2020’ kuanza Mei 22 hadi Juni 27, 2020.

Kwa mujibu wa ratiba ya awali, Nandy alipaswa kufanya shoo huko Colombus, Houston, Iowa, New York, Boston, Atlanta, Chicago, Los Angeles, Seattle, Nenver, Minnesota, Noth Carolina na Washington DC.

Mwishoni mwa 2020 baada ya nchi nyingi kuruhusu mikusanyiko ya kufuatiwa kuthibitiwa kwa Corona, Diamond alifanya shoo kubwa Malawi na Sudan Kusini.

Na mwaka 2021 Diamond akatoa burudani nchi za Uganda, DR Congo, Guinea-Bissau, Burkina Faso, Ethiopia na Dubai ambapo kote alifanya shoo moja moja.

Baada ya kuhudhuria utoaji wa tuzo ya BET ambazo alikuwa anawania, Diamond chini ya DMK Global Entertainment, alifanya ziara nchini Marekani na kutumbuiza miji kama Arizona, Boston, Louisville, Minneapolis, Washington DC n.k.

Mwaka 2022, ambao Diamond aliuanza kwa kutumbuiza kwenye shoo ya Zuchu ‘Mahaba Ndi Ndi Ndi’ iliyofanyika Febuari 14, 2022 Mlimani City, alifanya shoo Australia, Malawi, Kenya, Denmark, Finland, Sweden, Belgium, Switzerland, Ivory Coast, Ethiopia n.k. 

Hadi inatimia robo ya kwanza ya mwaka 2023, Diamond alikuwa hajafanya shoo yoyote ile, sio ya ndani wala kimataifa, mara ya mwisho kuonekana jukwaani ilikuwa Desemba 31, 2022 katika shoo yake na Zuchu, Cheers.

Shoo ya kwanza ya kimataifa ya Diamond kwa mwaka 2023 alitarajia kuifanya Aprili 29 huko Berlin, Ujerumani lakini iliahirishwa dakika za mwisho kwa madai promota alishindwa kutekeleza baadhi ya makubaliano yao.

Ila Agosti 2023 akatumbuiza Afro Nation nchini Marekani, shoo ambayo ilikosolewa na wengi mtandoni kwa madai haikuwa na mapokezi mazuri kwake, hivyo katika tamasha hilo alikuwa msanii mdogo ukizingantia alituimbuiza mchana wa jua kali.

Diamond alijibu madai hayo Instagram na kusema ni mengi huwa wanapitia katika shoo hizo za nje na kuwataka mashabiki na hasa Wanahabari nao kwenda kuona kuona hali halisi na sio kuripoti vitu nusu nusu.

Vilevile alifanya shoo nyingine katika mataifa ya Rwanda, Uganda na Equatorial Guinea, kwa ufupi kwa mwaka 2023, Diamond hakufikisha hata shoo nane za kimataifa.

Hivyo utaona kabla ya Corona, Diamond alikuwa na shoo nyingi za nje hasa Ulaya na Amerika ila baada ya hapo mambo hayajakaa sawa kwa upande wake. Shoo chache anazopata na ambazo zinakuwa na mapokezi mazuri ni kutokea Afrika. 

Lakini kuna sababu nyingine zinazopelekea Diamond kuwa shoo chache za kimataifa, moja wapo ni kutokuwa na wimbo unaofanya vizuri kimataifa ambao amemshirikisha msanii mkubwa wa nje.

Hata ukitazama shoo zake za kimataifa, nyimbo anazotumbuiza ni zile alizowashirikisha kina Davido, P-Square, Koffi Olomide, Fally Ipupa na Ne-Yo. Na kazi hizi zimetoka kati ya miaka mitatu hadi nane iliyopita. 

Diamond mwenyewe anakiri hilo katika mahojiano yake na Wanahabari hivi karibuni na kusema kolabo yake na Davido, Number One Remix (2014) ilimfungulia milango mingi barani Afrika kipindi ambacho alihitaji hilo.

“Sasa hivi Afrika nafanya shoo nchi yoyote tena kwenye uwanja ndio maana juzi imetoka orodha ya wasanii wanaojaza viwanja nipo namba tatu au nne.” alisema Diamond.

Wakati Diamond na wasanii wengine wa Tanzania wakitafuta kupenya Afrika, wenzao wa Nigeria walikuwa wanasaka tobo duniani maana Afrika tayari walishaimaliza na ndio sababu sasa unaona wao wanajaza viwanja vikubwa duniani kote. 

Mfano Burna Boy wa Nigeria amejaza viwanja kama State Farm Arena, Atlanta, Marekani - watu 21,000, Madison Square Garden, New York, Marekani - 20,700, Accor Arena, Paris, Ufaransa - 20,300, 02 Arena, London, Uingereza - 20,000.

Toyota  Center, Houston, Marekani - 18,300, Hollywood Bowl, Los Angeles, Marekani - 17,500, Ziggo Dome, Amsterdam, Uholanzi - 17,000, Ahoy Arena, Rotterdam, Uholanzi - 16,400.

Je, kwanini shoo za Diamond kimataifa zinazidi kupungua na kwanini hatumuoni katika viwanja hivyo vikubwa, kwa kulichambua hilo, tumezungumza na Promota wa Wasanii wa Afrika nchini Marekani DMK Global amesema kuwa anafikiri shoo za Diamond zimepungua kutokana na kutotoa ngoma kwa ajili ya soko la nje.

“Navyofikira mimi ni kwamba ukiangalia mara nyingi wasanii wanafanya kazi nje wanapokuwa wametoa kazi mpya na siyo singo unakuta ametoa albamu anaipromoti ikihiti ndiyo utaona anatoka nje ya nchi, huwezi kuzunguka ukawa unafanya shoo na nyimbo za zamani.

“Sasa ukiangalia mwaka jana mpaka sasa hivi nafikiri kazi nyingi ambazo Diamond amefanya ni kolabo siyo zake mwenye na hata za kwake ni kwa ajili ya soko la ndani na siyo la nje kwangu mimi hakuna kazi ambazo ametoa zitafanya apate soko la nje kwa ukubwa.” Alisema    

DMK ambaye ndiye amekuwa akiandaa shoo zote alizowahi kufanya Daimond nchini Marekani aliongezea kwa kusema kuwa  wasanii wengi hawapati shoo za nje kwa sababu muziki wao bado haujavuka mipaka ya Tanzania, kwani ili msanii aweze kupafomu kwenye nchi fulani ni lazima muziki uwe umevuka mipaka na kusikilizwa.

 Ikumbukwe kuwa DMK amewahi kuandaa shoo za wasanii mbalimbali kama vile Diamond, Alikiba, Harmonize, Rayvanny , Malaika, Linah Sanga, Vannesa Mdee, Shilole, Ommy Dimpoz, Prof Jay, Mr Nice na wengineo

Mbali na DMK, Mwananchi pia imezungumza na Said Fella maarufu ‘Mkubwa Fella’ ambaye ni moja kati ya mameneja wa mwanamuziki Diamond, amesema kuwa kuna nyimbo na video nyingi  ambazo zipo tayari hivyo anaamini mambo bado yapo palepale.

 “Mimi ninachoamini tulisimama kwa sababu ya mwezi wa Ramadhani lakini huko nje walikuwa wanahitaji sana shoo, ndiyo mwezi umeshabadilika mtaona kazi tena, uzuri mavideo mengi yamerekodiwa na nyimbo nyingi tayari zimefanywa kwa hiyo la msingi mimi naamini mambo bado yapo palepale”. Alisema