TUONGEE KISHKAJI: Mapenzi ya wasanii wa Bongo yanavyoharibu biashara za watu

Ukitaka biashara yako itembee sana tumia wasanii wa Bongo kama mabalozi, sana sana wale ambao wanatrend Instagram. Hao washkaji wana wafuasi wengi sio kitoto, unakuta msanii wa kawaida tu, ana followers zaidi ya milioni na akiposti kitu kwenye akaunti yake watu wanakipapatikia kweli kweli.

Mtu kama Wema Sepetu ana followers zaidi ya milioni 10 na akiposti kitu anapata wastani wa comments elfu 10 na likes zaidi ya 20 elfu.

Kwa wafanyabiashara wanajua mtu kama huyo ukimpa bidhaa yako sahihi aitangaze atakuletea wateja wengi sana.

Nimeshafanya kazi na wasanii kama mabalozi na nimewahi kuona nguvu yao katika kuvuta wateja… lakini moja ya kitu nilichojifunza ni hakikisha unakwepa kabisa kuwatumia mastaa wapenzi kama mabalozi wa pamoja wa bidhaa yako… nitakuelewesha kishkaji na utanielewa.

Unakuta mtu una kampuni ya kuuza bidhaa kama vile sabuni ya kuogea ambayo inaweza kutumiwa na jinsia zote, wanawake na wanaume.

Mmekaa ofisini kwenye vikao mnajadili nani mumtumie kama balozi asaidie kupush bidhaa yenu, jibu linakuja ni msanii mmoja wa kike, tuseme kwa mfano Tunda na mnakubaliana na atawafaa.

Mnawaza sasa jina la msanii mwingine wa kiume ambaye atasaidia kuisukuma sabuni yenu kwa upande wa wanaume.

Mnataja majina weeee, lakini mwishowe mmoja wenu anakuja na wazo anasema; “kwa sababu Tunda na Whozu ni wapenzi, kwa nini tusiwatumie kama sehemu ya matangazo yetu.” Halafu anaongeza, “tena kwa sababu hii sabuni inaogewa na wanawake na wanaume, tunaweza kutengeneza kampeni na kuitangaza kama sabuni ya familia ambayo inasaidia kutatua tatizo la familia moja kuwa sabuni mbili mbili za kuogea, yaani mke na mume mnaweza kutumia sabuni hii hii moja.”

Basi watu mnaona hilo ni bonge la wazo, mnatengeneza kampeni ambayo inawaonyesha Tunda na Whozu kama wapo kwenye familia moja, yaani mume na mke na wanatumia hiyo sabuni. Kwa sababu mnaamini nguvu yao kwenye mitandao ya kijamii mnawapiga mkataba wa mwaka mmoja.

Mnawapeleka photoshoot, mnalipia gharama kubwa za kupiga picha za matangazo na kila kitu, mnatengeneza matangazo ya redio na TV, mnapandisha mabango Tanzania nzima yakiwa na picha ya mabalozi wenu, mke na mume, Tunda na Whozu.

Mabango, matangazo ya redio na Tv na poster za Instagram zinakaa leo, kesho, keshokutwa mnaamka na stori ya mabalozi wenu mke na mume wameachana tena kwa skendo fulani hivi mbaya mbaya.

Kama unavyojua wasanii hawaachani kimya kimya, Tanzania nzima huwa inajua. Hiyo Tanzania nzima ndiyo wateja wenu wa sabuni kwa hiyo tayari hapo biashara yenu inaaanza kuingia doa.

Inaingia doa sio kwa sababu wao wameachana, bali ni kwa sababu sasa matangazo yenu yataonekana kama matangazo tu kwa sababu hayana tena uhalisia. Watu tunajua wameachana, lakini kwenye matangazo tunawaona ni mke na mume. Kwenye utangazaji wa biashara, moja ya kitu cha mwisho kabisa unachokihitaji kwenye tangazo lako ni tangazo lionekane kama tangazo.

Tangazo linatakiwa mtu akilitazama, akisikiliza, asihisi kabisa kama anatazama tangazo.

Hivyo kwa wafanyabiashara, moja ya vitu ambavyo hutakuwi kuvifanya ni kuwatumia wasanii wa bongo wapenzi kwenye matangazo yako, mapenzi ya wasanii wa bongo hayana dhamana, kuacha ni dakika sifuri tu.