TUONGEE KISHKAJI: Mamlaka husika zisiwachukulie ‘serious’ wasanii

SIKU moja mchekeshaji ambaye anavuma kwenye mtandao wa Youtube, Clam Vevo alikuwa anahojiwa na chombo kimoja cha habari. Wakati wa mahojiano akaulizwa kuhusu kipato anachopata kupitia mtandao huo, akasema ameshaingiza zaidi ya bilioni moja za Kitanzania kupitia Youtube.

Unaweza kumbishia, unaweza kumkubalia lakini nakukumbusha tu wakati Clam anahojiwa alikuwa anashikilia rekodi ya kuwa msanii wa vichekesho Tanzania mwenye chaneli ya Youtube inayotazamwa zaidi.

Kisha, miezi kadhaa mbele tukasikia taarifa kwamba Clam amekamatwa na yupo polisi kwa kosa la kukiuka maagizo ya Bodi ya Filamu Tanzania. Maagizo hayo ilidaiwa kuwa dogo alitumiwa ujumbe na bodi kwamba anatakiwa kupeleka kazi zake zikakaguliwe kabla ya kuwa anazipandisha Youtube, lakini akakaidi. Hakupeleka.

Hata hivyo, hekima ikatumika kwa pande zote mbili na sekeseke hilo likaisha kwa meneja wa Clam kufanya mazungumzo na bodi na kupatiwa elimu ya umuhimu wa kupeleka kazi kabla ya kuziachia na faida nyingine za Bodi ya Filamu.

Lakini, wakati sekeseke linarindima watu wengi mitandaoni walikuwa wanadhani kilichomponza Clam sio kupandisha kazi Youtube bila kukaguliwa, bali ni yeye kuropoka kwamba ana bilioni moja aliyoipata kupitia Youtube. Hivyo wazee wa bodi wakaona huyu mtoto ni nani? Mbona anavimba?

Sitaki kuamini kama hicho ndicho bodi walichowaza. Bodi wapo kwa ajili ya kuwasaidia watengeneza filamu nchini. Lakini tufanye kwa mfano kama hiyo ndiyo ilikuwa sababu, kwa mfano tu. Basi ningependa bodi wajitahidi kuwaelewa hawa watu wanaofanya nao kazi - namaanisha wasanii.

Wasanii kuvimba nd’o zao. Kujisifia ni sehemu ya maisha yao. Ni sehemu ya kazi yao. Wenyewe wanaita kujibrandi.

Kuna mwaka, msanii mmoja wa Bongo Movie alisema ameingiza Sh600 milioni kupitia filamu zake. Kisha baada ya kama mwezi udaku ukasambaa kwamba hana hata pa kulala na hadi leo huyo msanii ni kama amepotea.

Diamond akiwa kwenye mkutano wa kujadili maslahi ya wasanii pamoja uliondaliwa na Basata  alisema: “sisi hatuna kitu kama tunavyojionyesha. Hawa mabodigadi wengi tunaotembea nao ni mbwembwe. Kwa hiyo mnapofanya maamuzi muwe mnafikiria hilo.”

Msanii akiulizwa nguo ulizovaa leo ni za gharama gani? Atakwambia T- shirt ya laki nane, jinzi milioni moja na nusu, viatu milioni mbili.

 Wakati kanunua Mwenge na jumla ya vyote alivyovaa haifiki hata laki mbili na nusu. Hayo nd’o maisha yao. Hakuna chochote.

Na ukitaka kuamini hakuna chochote subiri wakati wa matatizo. Msanii akiumwa bakuli za michango zinatembezwa hadi unashindwa kuamini huyu nd’o alisema anaingiza Sh600 milioni kwa mwaka?

Kwa hiyo wazee wangu wa bodi mkisikia wasanii kwenye vyombo vya habari wanaongelea utajiri wala msichukulie ‘serious’. Hawana kitu. Wanafanya usanii tu. Wapeni uhuru wajinafasi na wajibrandi.