TUONGEE KISHKAJI: Kwanini Diamond akiiga wimbo anasemwa

MIEZI tisa iliyopita Nandy aliachia wimbo wa Amapiano unaoitwa Mchumba. Kiitikio kwenye wimbo huo kinaimbwa; ‘Kidege kinaondokaaa! Kidege kinaondokaaa’ kikiwa kimeshawishiwa au tuseme 'inspired' na moja ya nyimbo maarufu za Kilimanjaro Band.

Na sio kiitikio tu, hata mdundo wa nyimbo hizo mbili unafanana utofauti ukiwa ngoma ya Nandy imefanyiwa ubunifu na kuwa Amapiano.

Mbosso, Zuchu, Rayvanny, Mwana FA, Lady Jaydee na wasanii wengine wengi wamewahi kutengeneza nyimbo zinazofanana na nyimbo zilizowahi kuimbwa na wasanii wengine, lakini husikii wakishambuliwa na kubandikwa tuhuma za 'copy and paste'.

Lakini kila Diamond anapofanya hivyo mji huchafuka, watu humuandama kushoto na kulia na kumuita mwizi, aliyeishiwa, aliyekosa ubunifu, mzee wa kopi na kupesti na majina mengine kama hayo. Swali la kujiuliza ni kwanini huwa hivyo kwa Diamond tu? Binafsi nadhani kuna sababu mbili tatu. Nitazitaja.


Anaiga kwa anaoshindana nao

Mnyonge mnyongeni, Diamond ndiye msanii anayewakilisha Tanzania kwenye anga la muziki la kimataifa. Na kama unavyofahamu kwa sasa taifa kubwa linalokimbiza  kwenye anga hilo kwa Afrika ni Nigeria, kwahiyo hiyo ni sawa na kusema, Diamond anashindana vikali na wasanii wa Nigeria.

Sasa kwa bahati mbaya ukiangalia asilimia kubwa ya nyimbo anazotuhumiwa kukopi na kupesti, anazikopi kutoka kwa wasanii wa Nigeria tena wa kisasa ambao ndiyo washindani wake. Kina WizKid, Tiwa Savage na kadhalika. Hilo ni tatizo.


Yeye ni msanii mkubwa

Tumeshakubaliana kwmaba Diamond ndiye msanii mkubwa zaidi kutoka Tanzania kwa sasa. Ukitoka nje ya Tanzania, watu wengi wanadhani muziki wa Tanzania una msanii mmoja tu ambaye ni Diamond.

Hiyo ni sawa na kusema, Diamond amebeba mzigo mkubwa wa kuliwakilisha taifa linapokuja suala la muziki. Hivyo kukopi-kopi kwake kunaufanya muziki wa Bongo uonekane hauna ubunifu. Pengine ndiyo maana Alikiba anasema 'anaaibisha taifa'.


Anakopi sana

Kuwa inspired ni kitu cha kawaida sana kwenye sanaa. Wasanii wakubwa kabisa duniani wamewahi kuiga nyimbo za wasanii wengine na kuzirudia kwa aina yao na zikawa kubwa, kwahiyo tukubaliane kwamba hicho sio kitu kigeni.

Lakini tatizo la Diamond ni kwamba, anazidisha sana, ukianza kufuatalia nyimbo zake za miaka ya hivi karibuni nyingi amefanya kopi pesti. Mbaya zaidi anapofanya hivyo hufanya kwa ubunifu kidogo sana, yaani anaweza kuchukua mdundo na melody akabadilisha maneno tu.


Hatoa mashavu kwa waliomshawishi

Hili sio tatizo lake peke yake, ni la karibu wasanii wote wa tanzania. Wasanii wa Tanzania huwaga hawana utaratibu wa kupeana shavu. Msanii anaweza kuwa aliandikiwa wimbo na mtu mwingine. Lakini atapita kwenye media zote akiongelea wimbo wake bila kumtaja mwandishi wa wimbo. Na ndiyo kinachomkosti Diamond.

Vuta picha kama angekuwa akitoa ngoma ya kukopi na kupesti tu anaweka wazi kwenye media kwamba ngoma hii nime-sample au nimekuwa inspired kutoka kwenye ngoma fulani? Unaanzaje kumsingamanga mtu anayesema ukweli kiasi hicho?