TUONGEE KISHKAJI: Kinachowaponza Bongofleva ni Kiswahili

RAFIKI wa mtoto wangu alikuwa anafanyiwa sherehe ya kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwake 'Birthday party' nyumbani kwao, kwahiyo wazazi wengine ikabidi tuwapeleke watoto wetu kwa ajili ya kuruka debe na kufurahi na mtoto mwenzao.

Tulipofika pale kulikuwa na mapambo, keki, vyakula, michezo lakini moja ya jambo muhimu zaidi ilikuwa ni muziki. Ngoma zilikuwa zinapigwa ile mbaya na watoto walikuwa wanacheza kila wanapopata muda, kwa kifupi walionakena kufurahia muziki na kila kitu kilichokuwa kinaendelea kwenye sherehe hiyo.
Hata hivyo, ngoma nyingi zilizokuwa zinapigwa pale zilikuwa ni za wanaijeria ambazo kimsingi ndiyo zinazotrend siku hizi. Kokote utakapoenda, ukipigwa muziki tu, ngoma nyingi zitakuwa za Kinaijeria. 

Ikapigwa Ta Ta Ta ya Bayanni watoto wakaifurahia, na wazazi tukawa tunarekodi na video kabisa za ukumbusho. Ikapigwa Monalisa ya Lojay na hadi baadae ikapigwa Dame Tu Cosita ambayo yenyewe sio ya kinajeria, lakini watoto waliipenda na walikuwa wanacheza kweli kweli na wazazi tulikuwa tunafurahia.
Wakati yote haya yanaendelea, mimi akilini mwangu ilikuwa inatembea sentensi moja tu, 'Kiswahili kinawaponza wasanii wa Bongofleva' nitakwambia kwanini.

Kwa miaka kadhaa kumekuwa na malalamiko makubwa sana dhidi ya wasanii wa Bongofleva kuimba nyimbo ambazo kiukweli huwezi kuzisikiliza mbele ya watu unaowaheshimu kwa sababu ya lugha wanazotumia wasanii hao. 

Nyimbo zimejaa lugha chafu, matusi, ngono na mambo ya chumbani kiasi kwamba huwezi kuipiga mbele ya mkweo, mama yako, mtoto wako au mtu yoyote ambaye unataka kuwe na heshima kati yenu.

Pengine hiyo ndiyo sababu pia hata kwenye ile birthday ambayo tulienda ngoma za bongofleva zilikuwa zinakwepwa. Lakini tusichokijua wazazi ni kwamba, zaidi ya asilimia hamsini ya ngoma zote zilizokuwa zinapigwa kwenye party ile zilikuwa zinaongelea matusi mambo ya chumbani kama zilivyo ngoma za mastaa fulani wa Bongofleva na wasanii wote wenye itikadi ya kuimba hivyo.

Ngoma kama Monalisa ina mistari mizito ambayo pengine tungekuwa tunaelewa kiingereza cha wanaijeria kwa urahisi pamoja na lugha za kinajeria pengine tusingetaka watoto wetu wasikie hata mdundo wa nyimbo hiyo.

Ngoma kama Ta Ta Ta ya Bannyan ina lugha chafu karibu nusu ya wimbo. Kimsingi, chorus yenyewe tu ya wimbo sio jambo ambalo mzazi unaweza kusimama mbele ya mtoto wako na kuimba, au jambo la kumuona mwanao akicheza na kuimba na wewe ukafurahia.

Wimbo wa Demi Tu Co Sita wa El Chombo, msanii kutoka Panama ni wimbo ambao una mstari mmoja tu wimbo mzima, lakini mstari wenyewe hauna ustaarabu hata kidogo. Kimsingi, sio tu mstari, hata vionjo vilivyowekwa kwenye wimbo huo havina ustaarabu.

Pengine ndugu zetu wasanii wa Bongofleva wangekuwa wanatumia lugha tofauti na Kiswahili ambacho tumekizoea na tunakifamahu kindakindani wasingekutana na sekeseke na lawama za kuambiwa wanaimba matusi.