TUONGEE KISHKAJI: Kifo cha Haitham kiwashtue wasanii

Ijumaa Septemba Mosi kiwanda cha burudani Tanzania kilimpoteza mmoja ya wapambanaji wake. Mwanamuziki wa Bongo Fleva, Haitham Kim alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu kwenye Hospitali ya Rufaa ya Temeke ambako alilazwa kwa zaidi ya siku nne.

Akiwa anapatiwa matibabu zilisambazwa taarifa na mumewe kwenye mitandao ya kijamii akiomba mashabiki kumchangia mkewe kwani gharama za matibabu zilikuwa kubwa sana, si chini ya Sh700,000 kwa siku.

Wasanii wakubwa wengi waliposti tangazo kwenye kurasa za mitandao ya kijamii ili kujaribu kuongeza nguvu ya kuipata michango ya kusaidia afya ya Haitham Kim.

Hayati Ruge Mutahaba aliwahi kusema “ogopa Mungu na teknolojia” na nimeamua kuutumia msemo huo kwa sababu teknolojia au tuseme mitandao haisahau inatembea na kumbukumbu.

Kwanini nasema mitandao haisahau. Ni kwa sababu ukiingia Instagram ukitazama posti ya msanii yeyote ambayo inaongelea kumchangia Haitham ukashuka kwenye ‘comment’ utakutana na Watanzania wameandika vitu vya ajabu sana kuhusu Mtanzania mwenzao.

“Mnakula bata wenyewe mkiumwa mnakuja kutuomba misaada sisi.”; “Mnatuchambaga humu Insta tukiwaambia ukweli kuhusu bata mnazokula mkiumwa mnarudi Insta kutuomba msaada.”; “Mtaumwa sana mapafu msipoacha mishisha na mibangi.”; “Insta mnajifanya mna helaaa mkiumwa laki saba tu zinawashinda.”

Hivyo ndo namna watu wanavyokomenti. Lugha mbaya na chafu kwelikweli, lakini mtaani tuna msemo usemao ‘shida zinadhalilisha’. Yaani siku zote unapokuwa na shida hutoa fursa kwa watu wabaya kukudhalilisha, ndo kama hivi kwa sababu mtu anaumwa, anashindwa kumudu gharama za matibabu, lakini wana nzengo badala ya kumsaidia wanamgeuza ‘punching bag’ wakimwagia matusi.

Hii inanikumbusha makala niliyoandika 2022 kwenye gazeti hili hili kuhusu wasanii kupambana kuwa na mfuko wa kusaidiana wenyewe kwenye nyakati kama hizi.

Niliandika, habari za wasanii kushindwa kumudu gharama za matibabu yao wenyewe ni moja ya viashiria kwamba usanii hapa Tanzania unafanywa kama kitu cha ziada tu. Yaana hata wanaojiita wasanii iwe waigizaji au wanamuziki wanafanya kwa ajili ya kurahisisha michongo yao mingine. Wanatumia usanii kama daraja tu.”

Yaani haiwezekani wasanii wana vyama na mashirikisho kibao, lakini kote huko wameshindwa hata kujitengenezea utaratibu wa kusaidiana kwenye mambo kama haya hadi waanze kupitisha bakuli kwa mashabiki na wadau.

Hatukatai kutoa ni moyo, kwamba kuna nafasi ya mashabiki pia kuchangia wasanii wao wanaowapenda, lakini inapendeza zaidi ikiwa hata mashabiki wasipochangia hakiharibiki kitu msanii bado ana uwezo wa kupata huduma anazohitaji.

Maana yake mambo ya kutegemea michango ya moja kwa moja kutoka kwa mashabiki ndiyo yanasababisha wanawachimba mikwara wasanii huko Instagram.

Mtaani tunasema muda wa Mungu ukifika umefika, kwamba siku ya mtu ikifika hata kama tutamtibia kiasi gani, basi atakwenda tu. Lakini licha ya kulifahamu hilo, bado hatuachi kuwapambania ndugu zetu wanapokutwa na maradhi. Pengine ni muhimu wasanii kuanza kutengeneza njia ya kupambaniana mapema.