TID kaelewa 'assigment', ila awe makini na watoto wa 2000

KAMA wewe ni mtu wa mitandao bila shaka unafahamu kinachotrendi wiki hii ni vita ya maneno kati ya msanii mkongwe wa muziki wa Bongo Fleva, Khalid Mohamed

‘TID’ na msanii wa kisasa wa muziki huo, Abigail Chamungwana maarufu kama Abby Chams. Lakini kama huelewi kinachoendelea, usikonde, nitakupa stori ilivyokuwa. Stori iko hivi. TID akiwa na mwenzake Aboubakary Shaaban Katwila ‘Q Chief’ walikuwa wanahojiwa na moja ya ‘media’ Bongo.

Katika mahojiano hayo mtangazaji alimuuliza TID swali ambalo lilimfanya ajibu kwa kuwatolea mifano wasanii wawili, Marioo na Abby Chams. Alipokuwa anamtolea mfano Abby Chams alisema: “Kwa mfano kuna siku nilikuwa namuona msanii fulani anahojiwa anasema mimi siwezi kupika ugali. Nikasema msanii kama huyu kama hawezi kupika ugali anaijua kweli misingi ya Utanzania, ataiwakilisha vipi Tanzania kupitia kazi zake.”

Kipande hicho cha video kilisambaa na kutrendi na kusababisha media nyingine kumfanyia mahojiano Abby Chams kumuuliza yeye amepokeaje maoni ya TID. Kitu cha kwanza ambacho Abby alichosema ni kwamba, yeye alikuwa hamfahamu hata huyo TID ni nani. Alisema: “Mimi hata nilikuwa simjui ni nani. Nilitumiwa video nikamuona babu mwenye kipara ananiongelea. Nikaambiwa ni msanii wa zamani. Lakini tatizo la wasanii wa zamani wanapenda kutushambulia wasanii wa kisasa, yaani badala ya kutuunga mkono wanapenda kutengeneza mazingira ya sisi kuonekana kama kuna vitu tunakosea.”

Baada ya majibu ya Abby sekeseke likazidi kuwa kubwa, kwani TID aliitwa kwenye intavyuu zingine na akazidi kumuongelea.

Ukiniuliza maoni yangu juu ya kilichotokea na kinachoendelea nitakuambia naona kama vile TID ameelewa ‘assignment’ kwamba muziki wa sasa hautegemei kipaji. Muziki wa sasa hautegemei mtu mwenye sauti kali ya kuimba. Muziki wa sasa hautegemei mashairi makali. Muziki wa sasa unategemea zaidi kuzungumziwa hususan kwa mambo ambayo hayahusu muziki kwa asilimia 100.


Na ndio maana akiwa kwenye intavyuu hiyo, TID alizungumza vitu vingi sana kuhusu wasanii wengine. Alimuongelea Marioo kama nilivyosema, pia alimuongelea Peter Msechu na wengine. Kama wote hao wangemjibu maana yake angetrendi zaidi mitandaoni wiki hii na kukipa thamani kitu ambacho anakifanyia kampeni kwa sasa ambacho ni bendi yao ya TOPBAND ambayo inaundwa na yeye na Q Chief.

Hata hivyo, licha ya kwamba nampongeza TID kuhusu kuelewa jinsi muziki wa sasa unavyohitaji, bado afahamu kwamba anabishana na watoto wa miaka ya 2000, kizazi ambacho kinasifika kwa kukosa adabu hivyo awe makini kwa sababu hao madogo wanaweza kumvunjia heshima dakika yoyote.

Asishangae siku akaamka akakuta video zake za ajabu mtandaoni asijue hata zimerokidiwa lini, wapi na nani. Asishangae siku anaamka anakuta kuna mtu anamuogesha matusi mazito ambayo yatamfanya ajibu na kujikuta anapoteza heshima yake ambayo pengine ameijenga kwa miaka mingi katika tasnia ya burudani nchini.

Kwa kifupi kushindana na madogo wa 2000 mtandaoni ni kama vile kuuza samaki. Tegemea kufuatwa na nzi kwa sana.