Tessa wa Huba kuzikwa Dar

Muktasari:
- Akizungumza na Mwanaspoti, semaji wa familia ambaye pia ni mzalishaji wa tamthilia ya Huba inayorushwa kupitia kisumbuzi cha DSTV, Aziz Mohamed alisema Grace amepoteza maisha kutokana na ugonjwa wa homa ya mapafu.
MWIGIZAJI nyota aliyetamba kupitia tamthilia mbalimbali ikiwamo Huba, Grace Mapunda a.k.a Tessa au Mama Kawele amefariki dunia usiku kuamkia jana wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mwananyamala na atazikwa kesho, Jumatatu, kwenye makaburi ya Kinondoni, Dar es Salaam.
Akizungumza na Mwanaspoti, semaji wa familia ambaye pia ni mzalishaji wa tamthilia ya Huba inayorushwa kupitia kisumbuzi cha DSTV, Aziz Mohamed alisema Grace amepoteza maisha kutokana na ugonjwa wa homa ya mapafu.
“Kama wiki alikuwa akiumwa na kifua kidogo, juzi akazidiwa. Juzi kuingia jana hali ikawa siyo nzuri akapelekwa Hospitali ya Mwananyamala, kama wiki hivi alisumbuliwa na nimonia,” alisema Aziz na kuongeza:
“Kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu tutampumzisha Jumatatu saa kumi katika makaburi ya Kinondoni. Kesho mwili wake utaletwa nyumbani. Ibada ndogo zitafanyika hapa kesho-kutwa, siku ya Jumatatu mwili utatoka nyumbani kuelekea Viwanja vya Leaders ambapo viongozi na watu mbalimbali watakuja kumuaga kutoka saa nne mpaka saa tisa, na baada ya hapo tutaelekea makaburi ya Kinondoni kwenda kumsitiri.”
Mkongwe huyo alitambulishwa na kundi la Shirikisho Msanii Afrika lililokuwa na wasanii kadhaa kama Bakar Makuka ‘Beka’, Richard Mshanga ‘Bosi Masinde’, Samson, Vailet, Samofi, Jaji Khamis ‘Kash’, Amanda, Happy Nyatawe na wengineo.
Kifo cha Mama Kawele kimekuja siku chache tangu fani ya uigizaji kupoteza wasanii wawili wakongwe akiwamo Khadija Shaibu ‘Dida’ na Yusuph Kaimu ‘Pembe’ waliowahi kutamba na kundi la Kaole Sanaa.
Mama Kawele aliyewahi kutamba na makundi mbalimbali likiwamo la Shirikisho Msanii Afrika lililowika na michezo katika kituo cha ITV, taarifa za kifo chake zianza kusambazwa na wasanii wenzake Idris Sultan na Jimmy Mafufu kwenye mitandao ya kijamii. Idriss Sultan aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram huku akiposti picha yake kwamba; “Nimechagua kukukumbuka hivi. Innallillah wainna illlaihi rajiighun,” huku Jimmy Mafufu akiandika katika ukurasa wake wa Instagram kwamba “Muigizaji kinara mama yetu Grace Mapunda ametwaliwa na Bwana, ni muigizaji namba moja kwa wamama wote nchini, amekuwa mhimili mkubwa kwa tasnia yetu Mungu amemchukua pumzika kwa amani mama yetu kipenzi.”
Msanii mwingine aliyekuwa akiigiza na Tessa kwenye Huba, Rammy Galis aliandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram ya kwamba: “MAMA (huku akiweka emoji ya picha ya majonzi), Mwenyezi Mungu akusamehe na akujaalie kila chema kwenye safari yako. Nilipokuona jana ICU niliumia sana sikuwa na uwezo wa kubadilisha hali niliyoiona machoni kwangu...”