Tarajieni kolabo ya Fally Ipupa na msanii wa bongo

Mwanza. Ukiachana na kolabo maarufu ya "Inama" aliyofanya msanii, Fally Ipupa na Naseeb Abdul "Diamond Platnumz" msanii huyo maarufu kutoka nchini Congo DRC amesema watanzania wakae mkao wa kula kwani hivi karibuni atatoa wimbo mwingine na msanii kutoka Tanzania.

Akizungumza siku moja kabla ya kufanyika shoo ya msanii huyo inayotarajiwa kufanyika usiku wa kuamkia Alhamisi Oktoba 14, 2021 Meneja wa msanii huyo Madina Djobongue amesema Fally Ipupa anaendelea kufatilia ni msanii gani afanye naye kolabo kabla ya kuondoka nchini.

Djobongue ametaja baadhi ya wana muziki ambao Fally Ipupa anawakubali kuwa ni pamoja na Alikiba, Barnaba na Diamond Platinumz.

"Bongofleva ni muziki  unaoonesha asili ya muafrika ndiyo maana Fally yuko tayari kufanya kolabo na msanii kutoka nchini Tanzania, yuko tayari kusikiliza wimbo kutoka kwa msanii yoyote ikitokea ameukubali basi hana shida ataingiza sauti ndani ya hata dakika mbili," amesema Djobongue

Ameongeza kwamba baada ya msanii huyo kumaliza shoo yake jijini Mwanza atatembelea vivutio vya utalii nchini ili kuutangaza utalii wa Tanzania.

"Wakazi wa Kanda ya Ziwa wajitokeze kwa wingi hapa ilipo hoteli ya Malaika tunaamini hawatojutia kutoa kiingilio chao," amesema Djobongue